Yafanyike Mashambulizi Mangapi Dhidi ya Watalii Ili Afrika Magharibi Iandae Mkakati wa Pamoja wa Kikanda?

On the way to Grand Bassam beach side, Cote d'Ivoire. PHOTO: Oluniyi Ajao (CC BY-SA 2.0)

Eneo la fukwe huko Grand-Bassam, Côte d'Ivoire, eneo lililoshambuliwa na magaidi Machi 13. Picha: Oluniyi Ajao (CC BY-SA 2.0)

Na Jemila Abdulai. Toleo la makala hii  lilichapishwa kwa mara ya kwanza kwenye Circumspecte.com.

Tujadadili kidogo kuhusu shambulio la kigaidi la Machi 13 nchini Ivory Coast. Hususani kile ambacho nchi ya Ghana pamoja na nchi nyingine za Kiafrika zinaweza kujifunza au kufanya. Kwa wale wasiofahamu, takribani watu 16 walipoteza maisha tarehe 13 Machi katika eneo la  Grand-Bassam, nchini Ivory Coast.

Mji mkuu wa zamani wa Ivory Coast na eneo linalotambulika na UNESCO kama la kihistoria, Grand-Bassam ni moja ya maeneo yanayotembelewa sana na fukwe iliyo umbali wa masaa machache kutoka Abidjan, mji mkuu wa Ivory Coast. Kwa nchi ya Ghana, Grand Bassam ingaliweza kufananishwa na Ada Foah au Ufukwe wa Labadi. Nchini Senegali, Grand Bassam yao ingeweza kuwa ni Kisiwa cha Gorée au moja ya fukwe nyingi zilizopo Dakar. Lakini hakuna hata moja ya haya ni jipya. Muswada wa filamu ni uleule, mwigizaji tofauti. Kuhusu mkakati, washambuliaji (Al-Qaeda, kwa muktadha huu) wameendelea kuwa na mikakati ile ile.

“Kwa nchi ya Ghana, Grand Bassam inaweza kufananishwa na Ada Foah au ufukwe wa Labadi . Nchini Senegali, Grand Bassam yao inaweza kuwa ni Kisiwa cha Gorée au moja ya fukwe nyingi maarufu zilizopo Dakar.”

Mkakati huu upoje haswa? Ni kushambulia maeneo ambayo mara kwa mara yanatembelewa na wageni wa nchi za kigeni na hoteli za kitalii, maeneo yanayotembelewa sana, maduka makubwa na maeneo ya burudani. Wameshafanya hivi huko Burkina Faso na Mali, huko Tunisia na Kenya, na sasa nchini Ivory Coast. Mkakati huu unaweza kuwa na malengo tofauti kidogo kwa kila nchi (kwa mfano kulingana na mahali nchi ilipo), lakini lazima kwa kiasi kikubwa lengo linakuwa ni moja: kuvuta hisia za watu na vyombo vya habari ili kusaidia kusikilizwa kwa matakwa yao ya kisiasa. Ni kwanini maeneo yanayolengwa ni yale ya wageni na watalii? Wanachohitaji ni kuona vyombo vya habari vya kimataifa na si vya ndani vikitangaza matukio hayo. Kushambulia maeneo kama haya inamaana kuwa nchi nyingi zaidi zinahusihwa. Kwa mfano, miongoni mwa wahanga wa shambulizi la Ivory Coast walikuwemo raia wa Ujerumani, Ufaransa, Cameroon, Mali na Burkina Faso. Shambulio moja, nchi sita ziliathirika (na bila ya kuhesabu majeruhi). Shambulio la Januari 2016 lililotokea nchini Burkina Faso lilisababisha vifo vya watu 18 wa mataifa tofauti. Hii ni mbali na kuhesabu idadi kubwa ya raia wazawa ambao pia waliathirika.

Jambo jingine ni kuwa, makundi haya yanaonekana kufuatilia habari zinazotangazwa zaidi kwenye vyombo vya habari. Burkina Faso ilikuwa na machafuko ya wenyewe kwa wenyewe kabla ya kushambuliwa . Mali imekuwa ikitajwa sana kwenye vyombo vya habari tangu kutokea kwa kifo cha Gaddafi, na kuripotiwa kwa kiasi kikubwa kwa maeneo yake ya kihistoria yaliyotambuliwa na umoja wa Mataifa. Na baadae, Ivory Coast ilipata kujadiliwa kwa uzuri sana kwenye vyombo vya habari, hususani tangu wakati wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015. Siku za hivi karibuni, Ivory Coast imeizidi Nigeria kwa kuwa nchi inayopendelewa zaidi kwa masuala ya uwekezaji katika eneo la ukanda wa chini.

Kwa hiyo, kama mfuliozo wa matukio haya upo wazi kabisa na azma yao ni ileile, swali linalofuata ni kuwa serikali za Kiafrika zinafanya nini ili kukomesha hali hii, kukabiliana au kujiandaa kwa mashambulizi? Washambuliaji wapo kimkakati-kwa kiwasngo cha kuwasiliana vyema-ni kwa kiasi gani nasi tunajipanga hivi?

Shambulizi la Novemba 2015 la Paris lilipotokea, maeneo yote ya Ulaya na Marekani waliingia kwenye tahadhari kubwa na kuimarisha ulinzi, kama ambavyo walivyopaswa kufanya kwa mara nyingine mara baada ya kutokea kwa shambulizi la wiki hii huko Brussels. Baada ya kutokea kwa shambulizi la Paris, polisi wa Uingereza walisambaza video na taarifa kwa raia kuhusu kile walichopaswa kukifanya wakati wa shambulizi la kigaidi.

Afrika ya Magharibi imeshakabiliwa na mashambulizi matatu ya kigaidi kwa siku za hivi karibuni (bila kuijumuisha Nigeria). Nchini Ghana, angalao, mbali na dondoo za kwenye vyombo vya habari na majadiliano mafupi ya moja kwa moja kuhusu ulinzi, sijaona taarifa yoyote ya kina ya ufuatiliaji kuhusu mashambulizi ya aina hii, au kipi kifanyike endapo kutatokea mashambulizi kama haya.

“Afrika ya Magharibi imeshakabiliwa na mashambulizi matatu ya kigaidi kwa siku za hivi karibuni (bila kuijumuisha Nigeria). Nchini Ghana, angalao, mbali na dondoo za kwenye vyombo vya habari na majadiliano mafupi ya moja kwa moja kuhusu ulinzi, sijaona taarifa yoyote ya kina ya ufuatiliaji kuhusu mashambulizi ya aina hii, au kipi kifanyike endapo kutatokea mashambulizi kama haya.”

Kwa mfano, ni kwa namna gani tunaweza kutoka kwenye majengo kama vile hoteli au maeneo ya kazi pindi yanapotokea mashambulizi kama haya? Tumeshaainisha maeneo ya kutokea ya miji na majiji mengine makubwa? Kuna mfumo wa Kitaifa au wa kikanda wa ishara za mapema au mkakati wa maeneo yanayoleangwa zaidi kama vile hoteli na maeneo ya vivutio? Tumeshatoa mafunzo kwa wawajibikaji wa kwanza kabisa kama vile polisi na waokoaji? Hivi, mkakati wetu ni upi na uko wapi?

Nimekuwa nikiuliza maswali haya tangu shambulio la 2013 kwenye maduka ya Westgate ya jijini Nairobi nchini Kenya. Upo wapi mkakati wa kikanda wa Afrika kuhusu ulinzi na ugaidi? Kama upo, mamlaka za kikanda kama vile ECOWAS na Umoja wa Afrika zinafanya nini kuhakikisha raia wa nchi wanachama wanaufahamu wa mikakati inayochukuliwa?

Upo wapi makakati wetu unaofanana na ule wa ushirikiano uliofanywa na mataifa ya Ulaya mara baada ya nchi za Ulaya kushambuliwa? Bila shaka Marekani inaweza kuwa na ulinzi imara zaidi huko Afrika ya Magharibi, lakini kuna kandarasi zozote za ushirikiano na serikali za kiafrika?

Mwisho wa siku, taarifa, kuchukua tahadhari na kufanya maandalizi ndio mambo yatakayosaidia kuokoa maisha ya watu. Nchi ya Ghana inapakana na nchi za Burkina Faso na Ivory Coast, kama ulikuwa hujui-zipo karibu sana kwa ajili ya kusaidiana. Senegali ni miongoni mwa nchi ambazo zinapaswa kuwa na tahadhari ya hali ya juu.

Ghana ni miongoni mwa nchi zilizo na maeneo mengi yanayotembelewa sana na wageni na watalii pamoja na watu kutoka katika jamii mbalimbali za kimataifa. Pia, ina jamii za watu wasiotambulika na waliotayari kutumiwa na magaidi wanaotafuta wanachama wapya. Bila kujali ishara matarajio makubwa ya “amani” yetu, huu utabaki kuwa ukweli. Maisha nchini Ghana siyo rafiki kwa kila mmoja. Tupo hatarini kama ilivyo kwa mataifa ambayo tayari yameshashuhudia mashambulizi.

Kipi kinaweza kufanyika? Sihitaji hata kulitazama sana hili kwa undani wake: Katika lugha za makabila ya watu wa Ghana, kama vile Twi, Ewe, Dagbani, Fante, na Ga, neno “gaidi” linaweza kuitwaje? Raia wa kawaida wa Ghana anafahamu kuwa “Al-Kayida”, siyo tu ngoma ya Ashanti iliyozoeleka, lakini pia inaibua hisia na kuwakilisha kitu cha kuogopesha na kilicho cha hatari? Ikitokea mtu akapiga kelele za “Al-Qaeda”, je watu ndio wataendelea kunogesha ngoma, au wataacha kuendelea kucheza na kukimbia?

Raia wa Ghana wamefuatilia kwa ukaribu matukio ya mashambulizi kwenye nchi za jirani? Tumeshaelimishwa au kupata taarifa za kutosha kuelewa mambo ya msingi kama vile kupayuka au kusali “katika jina la Yesu” kunaweza kusiwe ndio namna suluhisho pekee pale watu wanapovamiwa, kwani magaidi mara nyingi wamekuwa wakiwalenga Wakristo? Watu, hususani watoto, watafahamu kuwa wanalazimika kukaa mbali na sauti za risasi, au watafikiri kuwa ni sauti tu za masalia ya wafyatua fataki wakati wa sikukuu ya Krismasi?

Hatari haipo mbali sana kama tunavyoweza kufikiri. Bado hatujakuwa na maandalizi yoyote kama tunavyopaswa kufanya. Na kama alivyotangulia kusema mgombea Urais wa mwaka 2012 nchini Ghana, kuwa mahsambulizi yana nafasi ndogo sana ya kwenye amani ya ndani au uhusiano ulipo kati ya makundi ya kidini. Kuna mambo tunayopaswa kuyafanya kwa haraka. Kama vile watu kuelimishwa, kuwepo na namna za kuelezea matukio ya kigaidi kwa lugha za makabila, kuwatahadharisha watu na kadhalika.

Tunaweza pia kuyachukulia kwa uzito wake matukio ya nchi nyingine kama vile Ivory Coast, Mali na Burkina Faso, badala ya kuzindua kampeni za “kuombea nchi X”. Tunahitaji pia kutofautisha taratibu na alimradi. Kwa nini kwa sasa kuna misururu mingi ya magari ya raia na ya kijeshi? Pale dharura ya kwlei itakapokuwa imejitokeza, tutawezaje kutofautisha? Ugaidi unaenea haraka sana pale kunapokosekana upashanaji wa taarifa na kukosekana kwa maelewano.

Mashambulizi yanapotokea mahali, isiwe ni tukio la kusema “asante Mungu, siyo sisi”. Kinyume chake, matukio haya yanapaswa kuwa ni namna ya kutufanya tuwaze kuwa “sisi tungefanya nini, endapo….”

Video ya YouTube ifuatayo iliandaliwa na mwandishi huyu kwa kumbukumbu ya wote waliotangulia mbele ya haki. Pia ni kwa ajili ya kuzihamasisha nchi za Afrika kuungana pamoja kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi:

Jemila Abdulai ni mwanzilishi na mhariri wa Circumspecte.com, jukwaa la kidigitali linashughulika na uchambuzi na mambo yanayohusiana na Afrika na Waafrika. Kama mtaalam wa masuala ya habari na Maendeleo ya Kimataifaa, amefanya kazi katika maeneo mbalimbali ya Afrika na ana shahada ya uzamili ya Sanaa ya Uchumi wa Kimataifa & Masuala ya Kimataifai kutoka chuo kikuu cha Johns Hopkins University SAIS.

1 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.