Katika lugha karibu 7,000 zinazozungumzwa duniani, ni lugha chache sana zinaweza kupatikana mtandaoni. Kwenye mtandao wa twita kwa mfano, asilimia 85 ya twiti zinaandikwa kwa lugha nane pekee, kwa mujibu wa utafiti mmoja – hata hivyo, utafiti huo unaweza usitoe picha halisi ya wingi wa lugha na tamaduni za dunia kwenye mtandao wa intaneti.
Ingawa jamii zaidi na zaidi zinaanza kugundua uwezekano wa kuweka lugha zao mtandaoni, hatua zaidi na zaidi zinahitajika kufanyika ili kujaribu kukuza uelewa na kutangaza juhudi hizi. Kwa malengo ya Siku ya Kimataifa za Lugha Asili mnamo Februari 21, Rising Voices, kwa kushirikiana na washirika wetu katika maandalizi Taasisi ya Living Tongues , Mradi wa lugha zilizo hatarini kutoweka, na Indigenous Tweets, ikiwa ni pamoja na washirika wengi washiriki, tunaungana kuzindua kampeni ya “Twiti kwa #LughaAsili.”
Kwa kupitia kampeni hii ya mtandaoni, tunahitaji kuwatambua na kuwahamasisha watumiaji wa mtandao wa intaneti wanaotumia lugha zao za asili kwenye mtandao wa Twita hususani kwenye lugha za wenyeji, zilizo kwenye hatari ya kutoweka na zinazozungumzwa na watu wachache, zote zikiwa hazijawakilishwa ipasavyo mtandaoni.
Ni rahisi kushiriki kampeni hii:
Hatua ya 1 – Twiti kwa Lugha yako ya Asili (kilugha)
- Twiti kwa kutumia lugha yako ya asili siku nzima
- Jadili “Kwa nini ni muhimu kutumia lugha yako kwenye mtandao wa intaneti?”
- Twiti salamu au maneno/misemo yako uipendayo kwa lugha yako
- Twiti tafsiri yake kuwahamasisha wazungumzaji wa jamii nyinginezo za lugha za wenyeji na wachache
Hatua ya 2 – Ongeza Alama habari
- Ongeza alama habari #MotherLanguage
- Ongeza alama habari ya lugha husika (mfano #Kichaga, #Kisukuma)
Hatua ya 3 – Jiunge na Mazungumzo!
- Watafute watu wengine kwa kutumia alama habari ya #MotherLanguage na sambaza twiti zao
- Tafuta alama habari ya lugha yako ya asili na wafuatilie wengine wanao-twiti kwa lugha hiyo
- Ungana na watu wengine wanaosherehekea wingi wa lugha
Kwa taarifa zaidi kuhusu namna ya kushiriki, pitia tovuti ya kampeni hiyo.
Kwa nini Utwiti kwa #LughaAsili?
Pamoja na kuongezeka kwa idadi ya lugha zinazotumiwa mtandaoni, jamii nyingi bado zinakabiliana na changamoto zinapojaribu kuwasiliana kupitia mitandao za kijamii. Baadhi za lugha zinakosa herufi za kompyuta zinazowasaidia watumiaji kuandika kwa lugha zao, na sehemu nyingine za dunia bado hazina mtandao wa intaneti, hali inayowafanya watengwe na mazungumzo ya mtandaoni.
Hata hivyo, mawasiliano ya mtandao yamethibitisha kuwa sehemu za muhimu ya utunzaji na uhuishaji wa lugha. Zana za kidijitali zilizorahisi kutumia zinasaidia watu kutengeneza maudhui kwa lugha zao, na kusaidia upatikanaji wa mtandao wa wazungumzaji wa lugha hizi, bila kujali sehemu za kijiografia.
Kampeni hii itamulika kazi za watu mbalimbali na makundi yaliyojitoa kutumia lugha zao kwenye mtandao wa intaneti, wengi wanaoweza kutambuliwa kama “wanaharakati wa kidijitali wa lugha” kwa nafasi zao katika kuunganisha pengo hili na kuhamasisha kizazi kipya cha wazungumzaji. Tunayo bahati kupata uungwaji mkono na “mabalozi” kama Rodrigo Pérez (@ISF_MX) kutoka Mexico, ambaye hu-twiti kwa lugha ya ki-Zapoteki na Ignacio Tomichá Chuve (@MonkoxBesiro) kutoka Bolivia, anaye-twiti kwa lugha ya Bésiro (Chiquitano), ambao walitenegeza video hizi kualika washiriki katika kampeni hii. Mabalozi wengine wataongezwa kwenye orodha:
Shukrani nyingi kwa msaada wa watu wengi duniani kote, na tovuti ya kampeni tayari imetafsiriwa kwenye lugha zipatazo 25, ikiwa ni pamoja na Odia, Sena, na ki-Lezgia. Nyingi za tafsiri hizi zimefanywa na wanachama wa Mradi wa Lingua wa Global Voices, Jamii ya watafsiri wanaojitolea.
Kwa msaada wako, tunaweza kufanya mtandao uwe na lugha nyingi kadri iwezekanavyo wenye kushamiri lugha tofauti tofauti, na sio kubagua baadhi ya lugha. Kinachohitajika tu ni kutwiti au kutangaza twiti za wengine!