Syria: Mafunzo ya Silaha na Namna ya Kupigana Katika Mtandao wa Intaneti

Makala hii ni sehemu ya makala zetu maalumu kuhusiana na mapinduzi nchini Syria 2011/12.
Waasi wa Syria wameanza kutumia wavuti kwa ajili ya kufundisha mbinu mbalimbali za mapigano ya kivita. Hili ni jambo jipya kabisa katika mitandao ya kijamii ambavyo hadi sasa vimeshajizolea umaarufu mkubwa mahali mbalimbali duniani kwa kufanya kazi kubwa ya kusambaza habari na kuwaunganisha raia kwa urahisi hasa katika zama hizi za Mageuzi katika nchi za Kiarabu.
Chaneli ya You tube yenye jina FSAHelp (Msaada kwa Jeshi la Kuikomboa Syria) ina takribani video 80 zenye lengo la kuwapa mbinu mbalimbali wanamapinduzi wa Syria-kuanzia yale ya mapigano yasiyohitaji silaha hadi yale ya kuunda mabomu ya kutupa kwa mkono pamoja na ujanja kwa kumnyemelea na kumshambulia adui kwa kificho.
Katika blogu yake, mwandishi wa Gary’s Reflectionaliandika:

Nafikiri jambo hili lisingeweza kuepukika. Ni “ishara ya nyakati tunazoishi.” Jeshi la Ukombozi wa Syria (FSA) limeanza kutumia mitandao ya YouTube na Facebook ili kuwafunza wale wanaojiunga nalo. Waasi hawa hawana silaha nyingi wala wapiganaji wa kutosha, na kwa kiasi kikubwa wao siyo wanajeshi kwa taaluma. Kwa hiyo wamepata njia mpya, njia waliyoigundua ya kuwapa raia ujuzi wa kuwa wapiganaji kupitia mafunzo yanayotolewa kwa njia ya mitandao ya kijamii hasa kuhusu namna ya kutumia vema silaha zao.

Ifuatayo ni moja ya video hizo, hii inaonyesha jinsi ya kusafisha na kuunga upya bunduki ya Kibelgiji:

Maoni yaliyowekwa katika video hizi kwa kiasi kikubwa ni ya kuliunga mkono Jeshi la Ukombozi wa Syria (FSA) ikiwa ni pamoja na uungwaji mkono kwa kukabiliana na utawala wa mabavu nchini Syria. Mfano ni mtoa maoni huyu[ar]:

الله يعينكم وينصركم على أعدائكم الأنجاس
salooooooo7y: Mungu awe pamoja nanyi, na awasaidie muwashinde maadui zenu.

Wengine waliwapa mbinu zaidi huku wakisahihisha baadhi ya taarifa katika video hizo:

وضعية الأنبطاح من أخطر الوضعيات خاصةً فالشوارع
أذا حد رمى عليك قنبلة يدوية ما تقدر تهرب بسرعة
sa3ood16: Mlalo wa kifudifudi ni wa hatari sana, hasa kwa mapigano ya mitaani. Iwapo mtu atakurushia bomu la mkono, itakuwia vigumu sana kukimbia haraka kutoka eneo hilo.

Pia inaonekana kuwa wafuatiliaji wengi wa kutokea Libya na Yemen wana uzoefu mkubwa kuhusu mambo haya na wana mengi ya kuongeza. Hii ni kweli pia kwa wale wanaocheza michezo ya video kama Metala Gear .
Wakati watu wanaingiza vita katika michezo ya video, watoto wa Syria wameathiriwa moja kwa moja kutokana na vita inayoendelea nchini mwao. Katika mitaa ya Taftanaz, wanacheza “FSA dhidi ya Assad”, kwa kutumia miti kama bunduki, , kama inavyoonekana katika video ifuatayo:

Je, kupandisha video kama hizi mtandaoni inakubalika kisheria?
Watu wengi wanahoji uhalali wa uwekwaji wa video za aina hii.
Kwa mujibu wa makala iliyowekwa mtandaoni, kuna uwezekano kuwa video hizo ziliandaliwa marekani (au Kanada)), na kisha zikawekewa tafsiri ya Kiarabu.
Katika blogu yake, iliyo mahsusi kwa ajili ya silaha za moto, Steve Johnson alijiuliza kuhusiana na uhalali wa video hizo kulingana na sheria za Marekani:

Je, ni halali kwa raia wa Marekani kutoa msaada kwa kijeshi kwa nchi ya kigeni au kundi la waasi? Sina hakika. Kimsingi, uhuru wa kujieleza huishia mipakani. Ni halali kabisa kuandaa video inayotoa mafunzo ya jinsi ya kutumia silaha na kisha kuyaweka kwenye YouTube kwa ajili ya matumizi ya ndani ya Marekani, lakini wataalamu wa kuandaa video za kufundishia matumizi ya silaha kama Magpul wanasema kuwa video zao za mafunzo huwa zinakaaguliwa kwanza na ITR na kuhitaji ruhusa kutoka Mamlaka za Ndani kabla ya kuruhusiwa kupelekwa nje ya Marekani.

Evakatrina alizifananisha video hizo na swala lile la Bradley Manning, ambaye ni mwanajeshi wa Marekani, aliyekamatwa mwezi Mei 2010 nchini Iraki akishukiwa kutoa taarifa za siri kwenye wavuti wa WikiLeaks unaoweka mambo yote hadharani.

@evakatrina: Kwa hiyo #Manning “aliwasaidia maadui” lakini hawawezi kuthibitisha jambo hilo kuwa lilisababisha madhara. Lakini papo hapo tunaona sawa kwamba mafunzo ya mapigano ya msituni kwa kila mtu hakuna shida?

Na vipi kuhusu Mwenendo wa Usalama katika mtandao wa Youtube?
Katika “ Kanuni ya Mwenendo wao wa Usalama na Vitu vya Hatari “, Youtube wameelezea kwenye kipengele kinachoihusu Marekani (ujumbe kama huo wameuweka kwenye sehemu ya taarifa zinazoihusu Kanada):

[W] Tunazuia vitu ambavyo vinaweza kuchochea machafuko, vinavyoshinikiza au kuonyesha hali ya hatari au mambo ambayo si halali kwa mujibu wa sheria au yanayoonyesha kila dalili ya kuumiza au kusababisha watu kupoteza maisha. Hii ina maana kuwa, hairuhusiwi kupandisha video zinazohusiana na vitu kama maelekezo ya namna ya kutengeneza mabomu, maelekezo ya namna ya kutumia mihadarati, mafunzo ya udunguzi kwa kutumia risasi, au dondoo kuhusiana na harakati za mitaani zisizo halali.

Msaada kwa FSA pia unapatikana katika mitandao ya Facebook na Twita; hata hivyo ukurasa wao wa Fecebook wa awali ulishafutwa, lakini ukurasa mwingine ulifunguliwa siku chache baadae [Ar]. Wanaohusika na ukurasa huu mpya wanahisi kuwa ukurasa huu mpya pamoja na ule wa Youtube, zinaweza kufutwa wakati wowote. Wanasema kuwa:

بعد اعلان القناة الروسية عن صفحتنا، تم اغلاقها و لا نستبعد اغلاق قناة اليوتوب. نرجو من الجميع تنزيل الفيديوهات في حال تم ذلك.
Baada ya televisheni ya nchini Urusi kuuzungumzia ukurasa wetu, ulifutwa mara moja, na tunafikiri kuwa hata video za Youtube zinaweza kufutwa muda wowote, hivyo tunawasihi kuzipakua video hizi kwa mara moja kama sehemu ya tahadhari.

Mwisho, swali linabaki kuwa, sheria zipindishwe ili kuendelea kuwasaidia waasi wa Syria katika vita yao dhidi ya mfumo wa ukandamizaji? Au sheria zisimamiwe ipasavyo ikizingatiwa kuwa video hizo zinaweza kutumiwa na kundi lolote la kigaidi duniani? Je? Je, taarifa za kiusalama za Ujerumani kuhusiana na uwepo wa Al-Qaida nchini Syria kutaongeza hofu hizo?

Picha ndogo iliyotumika katika makala hii ni picha iliyopigwa kutoka kwenye video iliyopandishwa kwenye mtandao wa Youtube wa msaada wa FSA ikionyesha namna ya kusafisha na kuunda bunduki.

Makala hii ni sehemu ya makala zetu maalumu kuhusiana na mapinduzi nchini Syria 2011/12.

3 maoni

jiunge na Mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.