Walimu nchini Tanzania wamekuwa kwenye mgomo kuishinikiza serikali kuwalipa madai yao na kuboresha maslahi yao ikiwa ni pamoja na mishahara. Mgomo huo uliofanyika baada ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), kupitia Rais wake Bw. Gratian Mukoba kutoa notisi ya masaa 48 kwa Serikali tarehe 28 Julai 2012, ulianza Jumatatu ya tarehe 30 Julai 2012 na kudumu kwa siku takribani nne. Kwa mujibu wa Chama cha Walimu, mgomo huo uliungwa mkono na asilimia 95.7 ya walimu wa shule za msingi, sekondari na vyuo vya ualimu.
Watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania wamekuwa ikifuatilia kwa karibu mgomo huo kutathimini madhara ya mgomo huo unaofanyika siku chache kabla ya zoezi la sensa ya watu na makazi lililopangwa kufanyika Agosti 26, 2012.
Mtandao wa JamiiForums unaotumiwa na wastani wa watu 10,000 kwa kila dakika, ulikuwa na posti inayokusanya habari za maendeleo ya mgomo huo nchini kote. Baadhi ya watumiaji wa mtandao huo walisumulia yaliyokuwa yanaendelea katika maeneo yao:
Mtumiaji anayetumia jina la Rymg akiwa Mwanza alisema:
Sasa hivi wanafunzi kata ya ilemela mkoa wa mwanza wapo katika maandamano wakiwa na mabango tofauti yenye maandishi “tunataka haki zetu” wakielekea mahakama ya mwanzo wilaya ya ilemela kufungua kesi zidi ya waalimu kwa kukataa kuwafundisha…
Agapetc aliyedai kuwa Korogwe naye alisimulia:
Hayawi hayawi sasa yamekuwa, walimu wa Halmashauri za Mji na Wilaya ya Korogwe wamegoma kwenda shule kwa kuunga mkono viongozi wao walioutangaza.
Shule nyingi zimeonekana walimu wakuu na wakuu wa shule tu ndiyo waliohudhuria maofisini, pia imebainika kuwa walimu wa sekondari wanaongoza kwa kutoenda kazini wakati shule za msingi imebainika walimu ktk shule chache wameenda kazini.
Katika sehemu nyingine, habari za maandamano ya wanafunzi kuvamiwa na vyombo vya dola hazikukosekana. Naytsory alisimulia yanayotokea Hanang:
Hanang’ shule ya sekondari Mahu wanafunzi wamefunga barabara ya kwenda Singida kwa kutumia madawati, hivi sasa polisi na ofisi ya elimu wamekwenda kule kutuliza hali.
Walimu wameitikia mgomo kwa zaidi ya 90% kwani shuleni wapo wapo wakuu wa shule na walimu wa field na wale wa kujitolea, shule za msingi wapo walimu wakuu tu.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Patrick Lusiano Tsere, alipinga hatua ya walimu kugoma, akiamini hatua hiyo inalenga kuhujumu zoezi na sensa ya watu linalotarajiwa kufanyika nchini kote kuanzia tarehe 26 Agosti 2012. Walimu wanatarajiwa kuwa makarani wakuu wa kuwezesha zoezi hilo:
Hivi hamjui zoezi la sensa linagharimu fedha nyingi kitaifa?! Hutaki hilo zoezi lifanyike unaelewa maana yake?!
Kama wewe mwalimu badala ya kufuata barabara ya kisheria ya kudai haki zako, unaamua kuhamasisha walimu wahujumu zoezi la sensa, je katika taratibu zenu za madai ambazo zimeainishwa kisheria, kuna kipengere au kifungu kinachowapa nyie nguvu ya kisheria to resort to blackmailing the government? Kama hio ndio attitude yenu walimu basi bila ya shaka watoto wetu watadumaa kimaadili.
John Mughobi Sagatti alikuwa na maoni tofauti na hayo kwenye ukurasa huo huo:
Hivi Balozi serikali yetu imeshagoma mara ngapi? Mi naona kila siku inagoma tu na hakuna pa kuipeleka…Iwajibike uone kama matatizo haya yatajitokeza…Corrupt government will never ever deliver! itatumia ubabe tu kuendesha mambo yake…Let the ‘legitimate government’ play its Part…
Yasinta Ngonyani, mwanablogu wa Maisha na Mafanikio aliweka picha inayomwonyesha mwanafunzi mmoja akiwafundisha wenzake kufuatia mgomo wa walimu wa shule hiyo, naakaiwekea maelezo yafuatayo:
Mwanafunzi anapoamua kuchukua nafasi ya ualimu. Hakika hapa ndipo inapoonekana walimu ni watu/walezi muhimu sana….
Ramadhani Msangi, mwanablogu wa JukwaaHuru aliweka mkususanyiko wa video za mgomo huo.
Katika mtandao wa twita, majadiliano yaliendelea:
Yericko Nyerere alitwiti:
Nasubiri hotuba ya rais wangu @jmkikwete sijui atasema nini, mwezi jana alisema serikali yake haihusiki ya Ulimboka, Je mgomo huu wa Walimu?
Haki Elimuwalikusanya habari za mgomo huo kutoka maeneo mbalimbali nchini. @HakiElimu walitwiti:
Angalia madhara ya mgomo wa walimu mkoani tabora hapa tafadhali #okoaelimu #changetanzania
Rama S Msangi @mchambuzi alitwiti:
I uploaded a @YouTube video Mgomo wa walimu huko Musoma
Wakati mgomo wa walimu ukiendelea, Rais Jakaya Kikwete alizungumza na wahariri wa vyombo vikuu vya habari tarehe 1 Agosti, 2012.
Irenei Kiria alihoji kwa twiti:
Naombeni msaada kwa mliofuatilia. Rais kafanya uamuzi gani kuhusu mgomo wa walimu?
Mtumiaji mmoja wa mtandao wa JamiiForums aliripoti mtandaoni kuwa Rais amesema madai ya walimu hayatekelezeki. Dada Subi wa blogu ya wavuti aliweka hotuba hiyo ya Rais pamoja na sauti katika Blogu yake.
Blogu ya TheHabari iliandika muhtasari wa tamko la Haki Elimu @HakiElimu Shirika linalojishughulisha na utetezi wa masuala ya elimu nchini Tanzania, kuhusu mgomo huo:
HakiElimu inasisitiza kwamba nchi itafanikiwa kuboresha elimu endapo tu itawekeza kwa walimu kwa kuboresha mazingira ya kazi, maslahi ya walimu, kuwashirikisha walimu katika maamuzi kuhusu masuala ya elimu na kuwapa walimu mafunzo kazini. Elimu bora haiwezi kuletwa na walimu walio hoi
Blogu hiyo iliendelea:
Viongozi wa Serikali wasiwabeze walimu; kwa kufanya hivyo wanawakatisha tamaa. Hata kama baadhi ya walimu hawakusoma kwa miaka mingi kama ilivyo kwa fani nyingine, wana umuhimu mkubwa sana. Ndio wanaowaandaa watanzania wa leo na kesho kimtazamo na kimaarifa. Hivyo, kudai kuboreshewa mazingira ya kazi ni haki yao; na Serikali inaweza kutimiza wajibu wake kwa kuwasikiliza na kushauriana nao bila ubabe na kejeli
Alhamisi ya tarehe 2 Agosti, 2012 Mahakama Kuu kitengo cha Kazi ilisitisha mgomo huo wa walimu kwa kwa maelezo kuwa haukuzingatia sheria. MjengwaBlogu iliripoti:
Mahakama leo imetengua mgomo wa walimu uliokuwa ukiendelea nchi kwa madai kwamba mgomo siyo halali
mahakama pia imeiamuru CWT kuwalipa fidia wanafunzi walioathirika na mgomo wa walimu
Mgomo wa walimu ulifanyika katika kipindi kifupi baada ya mgomo mwingine wa Madaktari kuibua mjadala mkali katika jamii. Wapo wanaodhani mgomo huo wa Madaktari haukutatuliwa.