Wakati vuguvugu la mapinduzi likiendelea Uarabuni matukio kadhaa ya vijana wenye hasirayamezuka katika tovuti za Senegal. Tangu mwanzoni mwa mwezi wa tatu, uanaharakati huo umeachana na ulimwengu wa mtandao na kundi linalojiita “Y'en a marre” (Imetosha Sasa Basi) sasa limegeuka na kuwa alama ya vuguvugu la upinzani.
Kundi la Imetosha Sasa Basi lilioundwa mwezi Januari 2011, liliibuka kutokana na kukata tamaa kulikojengeka baada yamgawo wa umeme ambao uliisababisha nchi ya Senegal ikwame. Kundi hilo (la harakati) linatokea katika vitongoji vya Dakar na linaongozwa na wanamuziki wa ughanii wa kufoka, wakiwemo Fou Malad, Thiat (wa kikundi cha Keur Gui) pamoja na Matador. Makala kwenye Afrik.com inaelezea habari za vuguvugu hilo [habari hii na viungo vyote vinavyofuata ni vya lugha ya Kifaransa].
Kundi hilo halifichi kitu chochote kwenye ukurasa wake wa Facebook:
Muda wa kulalamika mabarazani kwenu au kulalamika kusikozaa matunda juu ya kukatika kwa umeme umeshapita. Tunakataa kukubali mgawo wa kimfumo wa umeme unaolazimishwa kwenye nyumba zetu. Tumechoka mno. IMETOSHA SASA BASI.
Kundi hilo hivi sasa limegeuza manung’uniko yake juu ya mgawo wa umeme kuwa vuguvugu la kuwahamasisha vijana. Linashambulia ukosekanaji mkubwa wa ajira, unyama wa polisi na ufisadi. Lakini zaidi ya yote linawataka watu wajitokeze kushiriki.
Mnamo tarehe 19 Machi, kundi la Imetosha Sasa Basi lilifanya maandamano kwenye Place de l'Obélisque (Viwanja vya Obelisk) jijini Dakar, na lilitumia tovuti yake kuwaalika vijana wa Dakar. Waandaaji bila ya shaka walijua jinsi ya kufikisha ujumbe wao: fulana nyeusi zenye maandishi meupe “y'en a marre” ziligawanywa kwenye umati. Pia palikuwa na kauli mbiu zenye vina katika mtindo wa ughanii wa kufoka, na pia misemo ya vijana pamoja na lugha ya Wolof pia vilisikika.
Matokeo yake: mamia kadhaa ya vijana wenye shauku, lakini walioonekana zaidi, polisi – ambao waliokuwa doria chini ya mnara – hawakutumia mabomu ya machozi (Video):
Ili kudumisha mwamko huo, kundi hilo limejipa lengo jipya: kuhamasisha vijana na kuwapa sauti katika uchaguzi mkuu ujao wa 2012.Waandaji pia wameboresha ujumbe wao na kuja na kauli mbiu mpya: “ma carte d'electeur, mon vote” (”kadi yangu ya uchaguzi, kura yangu”).
Siku ya tarehe 15 Aprili walizindua kampeni ya taifa waliyoiita Daas Fanaanal (neno la ki-Wolof linalomaanisha “kujilinda”), kampeni ambayo ina shabaha ya kuwapa moyo vijana wapige kura bila ya kutoa kiapo au kujihusisha na chama chochote.
Vijana wa Senegal wameonesha kuunga mkono kampeni hiyo kwenye Facebook na Twita, kama inavyoeleza makala hii ya Mamadou Dieye:
Imetosha pia inatosha kwa sababu sehemu kubwa ya vijana wapatao milioni 1.4 wenye umri wa kupiga kura hawatajiandikisha kwenye daftari ya wapiga kura. (Vijana) hulalamika kwa haraka lakini huwa hawafanyi lolote kuhusu malalamiko yao. Imetosha Sasa Basi itafanikiwa kwenye changamoto iliyojiwekea ikiwa tu itasaidia kuharibu mpango wa Waziri wa mambo ya Ndani wa kuwaacha nje ya orodha ya wapiga kura vijana wote wasioiunga mkono serikali.
Imetosha Sasa Basi haisiti kuichachafya serikali ya Rais Abdoulaye Wade, na serikali haijaketi ubwete. Kundi hilo linadai kuwa limewekewa shinikizo kubwa sana, na linasema kuwa limepokea vitisho kutoka vyombo vya mamlaka. Mkutano mmoja na waandishi wa habari ulisitishwa baada ya mmiliki wa Janeer, mgahawa ambamo mkutano huo ulikuwa ufanyike, kushinikizwa na polisi.
Polisi pia walikamata vipaza sauti katika mkutano wa hadhara wa tarehe 19 Machi, 2011, kwenye mji wa Rifisque, karibu na Dakar, bila kujali ukweli wa kwamba kundi hilo lilipewa kibali rasmi cha kufanya tukio lile.
Thiat, mmoja wa viongozi wa kundi hilo, anaeleza kuwa kwanza na kabla ya yote kundi hilo ni kundi la wananchi, na si kundi la kumpinga Wade:
Hatupo upande wa Rais wala ule wa upinzani, tupo upande wa wananchi na tunatengeneza kundi la harakati ambalo linalinda na kudumisha heshima ya demokrasi na taasisi za Senegal. Ikiwa kundi la “imetosha Sasa Basi” lipo karibu na upinzani hivi sasa, waanzilishi wake wamesema kuwa hilo linasababishwa na kuwa tumechukua kero za raia.
Kundi hilo linataka mabadiliko. Mwisho. Umaarufu wake unaoongezeka umekuwa kana kwamba mavuo ya mwezi Aprili . Kundi hilo lilijibu mara moja:
Imetosha Sasa Basi sio samaki.
Samaki mdogo kwenye bwawa kubwa, au mapinduzi madogo? Upeo wa athari zake katika kampeni ya uchaguzi wa rais wa 2012 utajulikana mara. Ukweli unabaki kuwa, ni waghanii wafokaji wa vitongoji vya Dakar pekee ambao wanajitokeza kusema. Wakati wa uchaguzi wa rais uliopita wa mwaka 2007, masuala ya vijana yalitajwa kidogo tu kutokana na kundi la harakati la “Kizazi cha Zege”. Kiongozi wake alikuwa Karim Wade, ambaye alikuwa ni kijana wa umri wa miaka 39 ambaye pia ni mwana wa Rais Wade. Kusema kwamba vijana hawamo katika siasa za Senegal ni kupunguza makali ya ukweli.
Imetosha Sasa Basi Imetosha Sasa Basi sio wito wa kuiangusha serikali, na unaongelea msimamo wa demokrasi na amani. Mapinduzi yake yataathiri kila sanduku la kura nchini Senegal. Matukio haya yanathibitisha kuwa watu wa Senegal wanaamini katika nguvu ya karatasi za kura, lakini zaidi ya yote kwamba kampeni ya uchaguzi ujao wa rais imeshaanza, na wakati huu, vijana wa Senegal hawatakubali nafasi ya kuwa watazamaji tu.