Bahrain: Waandishi wa Habari Wazuiwa Kuingia Wakiwa Uwanja wa Ndege

Makala hii ni sehemu ya Makala zetu maalumu kuhusu Maandamano ya Upinzani Bahrain 2011.

Bahrain iliingia kwenye vurugu kubwa zilizoambatana na polisi kutumia nguvu dhidi ya waandamanaji waliopiga kambi katika eneo muhimu la wazi linalohusudiwa sana liitwalo Lulu Jumatano iliyopita.

Mchana wa siku hiyo nilipanda ndege inayotoka Doha, nchini Qatar, kwenda Bahrain, kwa upande mmoja nikitaka kujionea mwenyewe nini kilikuwa kikitokea katika nchi hii ya kisiwa ambayo ilipata kuwa nyumbani kwangu. Saa kadhaa baadaye nilijikuta kwenye ndege ya kurudi Doha, baada ya kunyimwa ruhusa ya kupita pale uwanja wa ndege.

Hivi ndivyo habari hii yangu ilivyotokea:

View from Bahrain International Airport. Image by Flickr user stephen_bostock (CC BY-NC 2.0).

Mandhari ya nje kutokea Uwanja wa Kimataifa wa Bahrain. Picha ya Flickr na stephen_bostock (CC BY-NC 2.0).

@omarc: Ala! twita kupitia ujumbe mfupi wa maneno hazifanyi kazi … nipo uwanja wa ndege wa Doha, kuelekea Bahrain. Nina imani tutajionea kwa macho yetu kama kweli serikali inawazuia watu kuingia

@omarc: Baada ya kufika naamriwa kuketi ofisi ya Uhamiaji ya Bahrain. Sielezwi sababu, naendelea kusubiri watasema nini …

Sina uhakika nini kiliwafanya wanitilie shaka – mchanganyiko wangu wa damu, viza kwenye pasi yangu ya kusafiria kutoka Oman kwenda Iraki, au mhisani wangu katika makazi yangu ya zamani kule Doha …

@omarc: Nipo uhamiaji hapa Bahrain kwa saa 1, wananiuliza ninfanya kazi kwa nani… “Uliwahi kufanya kazi Al Jazeera, au siyo?” Ndiyo, je, kuna tatizo? “Hakuna tatizo.”

@omarc: Tayari imeshatimu saa 2 bado nipo hapa @ dawati la uhamiaji Bahrain ili niruhusiwe kuingia nchini. Waandishi wa habari kutoka Uingereza, Ufaransa na Japani nao pia wapo wameketi.

@omarc: Wanawake wanaofanya kazi Ch 4 & wale wa Redio Ufaransa (mmoja baada ya mwingine) na yule kijana Mjapani wameruhusiwa kuingia Bahrain. Naendelea kusubiri…

Wakati baadhi ya waandishi wa habari waliruhusiwa kuingia, wengine – ikiwa ni pamoja na wale wa BBC ya Kiarabu na Al Hurra inayopata ufadhili wa Marekani hawa inasemekana walizuiwa kuingia. Mohammed Jamjoom, ambaye ni mwandishi wa CNN aliamriwa na Wizara ya Habari kuondoka nchini.

@JamjoomCNN: Mimi nilitimuliwa kutoka Bahrain … sasa nimerejea Abu Dhabi … #bahrain

@JamjoomCNN: wala sikuelezwa sababu za kutimuliwa kwangu kutoka Bahrain … nilielezwa tu kuwa mimi ndiye mwandishi pekee katika timu ya wenzangu wa CNN niliyetakiwa kuondoka … #Bahrain

Jamjoom anaweza kuonekana kwenye taarifa hii ya CNN akizungumzia kuhusu kile alichokionja kule Bahrain.

Alex Delmar-Morgan, ambaye ni mwandishi wa WSJ aliye nchini Doha, naye alishikiliwa kwa muda karibu na makutano ya barabara pale Lulu (Pearl) katika Manama, wakati mwandishi wa CBS Toula Vlahou ilitutolewa taarifa kwamba alikuwa akilengwa na mamlaka.

Kwa upande wangu:

@omarc: Ni saa ya tatu bado nipo uhamiaji Bahrain – sasa wanasema kwamba wageni hawaruhusiwi kuingia nchini, Manama si salama, na sina budi kurudi nyumbani.

@omarc: Maofisa wa uhamiaji wa Bahrain wananitaka radhi kwa kutoniruhusu kuingia nchini humo, lakini wanasema, “mambo yatakuwa shwari baada ya siku 2 hadi 3″.

@omarc: Napata pasi yangu ya kusafiria baada ya saa 5, pamoja na kadi ya kuniruhusu kupanda ndege inayoonyesha saa 11.30 alfajiri … QA ilinifanyia utaratibu wa kusafiri kwa ndege ya saa 5.25

Nikiwa pale kwenye dawati la uhamiaji Bahrain, sikuwa na mawasiliano ya intaneti, badala yake niliendelea kutuma twita kupitia ujumbe mfupi wa siku kutokea palepale. Baada ya kuwasili Doha, nilikuta msururu wa miitiko ya twita kuhusu tukio lililonipata,
zikitoka kwa wale walioguswa:

@realrogerbird: @omarc Tunakuombea usalama

Zikitoka kwa waungaji mkono:

@nabeelalmahari: @omarc nakutakia heri rafiki yangu, tunatumaini mtafaulu

@bhrabroad: @omarc tunaweza kukupa taarifa zote unazotaka hapo uwanja wa ndege #Bahrain

Wapo waliokuwa na mashaka:

@Nninanina: @omarc hiyo inadhihirisha utawala hautaki yeyote aone uhalifu wanaoufanya dhidi ya waandamanaji wasio na silaha, je, kuna tofauti gani kati ya #Bahrain na Qaddafi ambaye ametumia silaha dhidi ya watu wake

@maljaya3: @omarc Utakaporudi tena, watakuwa wameshaandaa kitu ambacho watataka wewe ukione – maigizo fulani hivi

Na wengine walikuwa hawana adabu:

@HubiBahrain: @omarc pata ukweli wa mambo …. ninyi nyote HAMRUHUSIWI kuingia ninyi ni kundi la walaghai watupu

Asante sana kwa wote mliotaka kusaidia, na nawatakia kila la heri waandishi wa habari mliofaulu kuingia nchini humo ili kutuma taarifa kuhusu yanayoendelea nchini Bahrain hasa katika kipindi hiki kigumu.

Unaweza kusoma nakala iliyo katika muundo wa simulizi ya habari hii kupitia Boing Boing, na vilevile seti kamili ta twita & miitiko kupitia Doha News.

Makala hii ni sehemu ya Makala zetu maalumu kuhusu Maandamano ya Upinzani Bahrain 2011.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.