Rwanda: Wanaomuunga Mkono wa Paul Kagame Wabaini Nguvu ya Twitter, Facebook na Blogu

Waungaji mkono wa rais Paul Kagame wa Rwanda wameanza kutumia nguvu ya ushawishi ya Facebook, Twitter na blogu ili kumsaidia kushinda uchaguzi wa rais unaotarajiwa kufanyika tarehe 9 Agosti 2010.

MyKagame ni ukurasa wa klabu ya marafiki wa Paul Kagame. Haya ndiyo mambo ambayo klabu hii inajihusisha nayo:

Kama kiongozi wa dola wa muda, mwenye historia nzuri na orodha ndefu ya mafanikio, Rais Paul Kagame ana wafuasi wengi wanaomchunuku na ambao wanamchukulia kama shujaa anayewapa uongozi katika maisha yao. Ukurasa huu ndiyo jukwaa lao. Ukurasa huo wa Marafiki/Wapenzi wa Kagame inaendeshwa na mashabiki hao kama kundi lenye lengo, kusudio na mwelekeo mmoja.

Kama shabiki wa Rais Kagame, kampeni hii ya Agosti inakuhusu. Uchaguzi wako ni wa maana sana. Hili ndiyo jukwaa lako la kuweka bayana mawazo yako kuhusu masuala ya kushughulikia wakati na baada ya uchaguzi wa rais. Simama imara katika yale unayoyaamini, ifanye Rwanda iwe nchi ya kujivunia!

Unaweza kujihusisha kwa njia mbalimbali:

Unaweza kujiunganisha na waungaji mkono wengine kupitia blugu za Klabu hii ya Marafiki.

Unaweza kuunga mkono juhudi zinazofanywa na watu wa kawaida za kuunga mkono kampeni za Rais.

Unaweza kueneza habari juu ya Klabu hii ya Marafiki na agenda za Shujaa wetu huyu wa Rwanda hasa kuhusiana na kampeni za Urais zinazokuja mbele yetu hivi karibuni.

Kwa kupasha moto mori wa watu wanaoamini katika mambo tunayoyathamani na wanaoipenda Rwanda.

Zaidi ya tovuti yake, klabu hiyo pia ina blogu. Zifuatazo hapa chini ni makala mbili katika zile zilizotumwa hivi karibuni kwenye blogu:

1. Rwanda yapiga hatua kubwa kuunda kiini cha TEKNOHAMA katika ukanda mzima:

Rwanda imejiimarisha vema kama kiini cha teknolojia, habari na mawasiliano (TEKNOHAMA) katika ukanda huu, hasa baada ya kuwa na mfumo madhubuti wa tasnia ya TEKNOHAMA, ikiwemo ufanyaji biashara, utoaji huduma vyote kwa njia ya mtandao, lakini pia uendelezaji utumiaji zana za kisasa na teknolojia katika kushughulikia mambo mbalimbali. Inaaminika kwamba TEKNOHAMA itatumiwa ili kutengeneza utajiri na kuwa kama ufunguo madhubuti wa kiuchumi. Kama sehemu ya lengo lake la kisera ili kuibadili Rwanda hatua kwa hatua kutoka kuwa yenye uchumi unaotegemea sana kilimo na kwenda kuwa nchi inayotegemea uchumi wa habari na maarifa (PIKE), Serikali ilijitosa kimkakati katika kutekeleza vipengele vinne vya Mipango ya Kimaendeleo (NICI/ICT4D) katika kipindi chote cha Kutekeleza Visheni ya 2020 na Sera ya ICT4D(TEKNOHAMA kwa ajili ya Maendeleo).

2. Shujaa wetu apata kibali cha NEC ili kugombea:

Kama ilivyokuwa imetarajiwa na marafiki wengi, Rais Paul Kagame, alikuwa ni mmoja kati ya wagombea wanne waliopata kibali jana cha Tume ya Taifa ya Uchaguzi kugombea katika uchaguzi utakaofanyika tarehe 9 Agosti mwaka huu.

NEC imepokea maombi ya Kagame kugombea katika kinyang'anyiro hicho baada ya chama cha RPF kumpitisha kupeperusha bendera yake kwa ajili ya awamu ya pili na ya mwisho kama inavyoruhusiwa na katiba.

Katika awamu hii, Rais Kagame ameahidi kuweka uongozi mikononi mwa wananchi. Hatua hiyo itaimarisha mshikamano miongoni mwa vijana, wanawake, makundi ya watu walio kwenye hali ngumu na vyama vya kijamii. Pia anaahidi kuimarisha njia za usambazaji habari na kuimarisha zaidi usalama wa nchi na nafasi yake kama dola.

Kuna ukurasa wa Facebook unaojulikana kwa jina la Paul Kagame will win 2010 presidential elections, yaani Rais Paul Kagame atashinda uchaguzi wa rais wa 2010. Mpaka tunakwenda mitamboni kulikuwa na jumla ya wafuasi 3,408. Baadhi ya ujumbe uliotumwa kwenye ukurasa wa mbele ni:

Moses Ndayisenga anasema:

Mungu na ambariki Paul Kagame wa Rwanda katika ushindi wake kwani tayari amekwishashinda uchaguzi wa 2010. VIVA KPAUL. Mzee WETU.

Siriba AbdulKarim anasema:

Mungu awe nawe katika kuwaongoza Wanyarwanda katika ustawi wa jamii yao. Endelea na moyo huohuo!

Sangano Gentle anaongeza kwa kusema:

Ndiyo, mpendwa RAIS wetu atashinda UCHAGUZI wa 2010. Hakuna kama yeye.

Kuna kurasa nyingine mbili za Facebook zinazomwunga mkono Kagame: PaulKagame yenye wafuasi 6,327 na Paul Kagame yenye wafuasi 8,169 (mpaka wakati tulipokuwa tunakwenda mitamboni).

Ujumbe wa mwisho katika ukurasa wa PaulKagame ulisomeka:

Leo akiwa mwenyekiti mwenza katika mkutano wa Kamisheni ya Broadband kwa ajili ya Maendeleo ya Kidijitali uliofanyika kule Geneva, Uswisi.
Alisema: “Hakuna mashaka yoyote kwamba matumizi ya Broadband ili kuamsha vipawa kamili vya watu ni jambo la lazima kiuchumi ili kuhakikisha kwamba jamii ya kiuchumi ya walimwengu wote inafikiwa na inamjumuisha kila mmoja … viongozi wa serikali, wafanyabiashara, asasi za kiraia hazina budi kuwajibika ili kufikia matokeo yanayoonekana.”

Hotuba ya Paul Kagame katika Kumbukumbu za 16 za Mauaji ya Kimbari ni ujumbe wa mwisho katika ukurasa wa PaulKagame.

Moja ya mada kwenye ukurasa huo ni kuhusu mwendeshaji/mtengenezaji wa ukurasa huo. Kulikuwa na wasiwasi kwamba huenda mwendeshaji huyo alifariki pasipo wafuatiliaji wake kuwa na habari:

Mukiza: Nina wasiwasi kwamba mwendeshaji ukurasa huu ambaye hatumjui huenda amekwishakwenda kuonana na muumba wake pasipo sisi kufahamu.
Maana kuna ukweli unaoonyesha kwamba ukurasa huu haujafanyiwa marekebisho mapya tangu mwezi Agosti 2009. Kipindi hicho ni kirefu mno kwa mtu aliye hai kuwa kimya hivyo kwenye ukurasa wake.

Kama mashaka yangu yana msingi, basi nawasilisha rambirambi zangu.

Mwendeshaji aliingia kwenye majadiliano hayo na kuelezea kuhusu ukimya wake:

Paul Kagame bado yupo, ondoeni mashaka;)

Hivi karibuni nimehama kutoka mji mmoja kwenda mwingine na mara nyingi nimekuwa sipati huduma ya Intaneti kwa miezi 3 iliyopita, na vilevile kutengana na mwenzi wangu wa kimaisha kwa zaidi ya mwaka. Samahani kwa kuwaacheni gizani kipindi chote hicho, lakini kila ninapopata fursa, huwa ninafungua na kusoma yale yanayoendelea. Kwa bahati mbaya hata waendeshaji wa kurasa za mtandaoni nao ni binadamu.

Kama kuna yeyote mwenye malalamiko, anachopaswa kufanya ni kuanzisha tu mada na mimi nitaiona.

Kuhusu ukurasa huu, ama kwa hakika unaonekana kwamba umekuwa ukiendelea kujitunza wenyewe, walau ndivyo mimi ninavyouona. Lakini nitapita ili kuusafishasafisha.

Inawezekana pia kwamba mimi nimeshika upande usio sahihi hapa, je, kumetokea mapinduzi? Je, jumuiya ya wachangiaji ingependa mimi niache kuendelea kuendesha ukurasa huu?:)

~ Mwendeshaji

Wanaomwunga mkono Kagame pia wanafahamika kwa kuendesha wavuti ndogondogo za kublogu za Twitter. Kuna paulkagame, ambayo ni ya faragha (ina wafuasi 196) na PaulKagame yenye wafuasi 964.

Twiti ya mwisho katika PaulKagame inasomeka:

katika Jimbo la Mashariki jana, suala la ugawaji ardhi na mazao ya ziada ya kilimo ni jambo lililopongezwa -ahadi ilitolewa kwa msaada zaidi wa serikali

Pia kuna ukurasa wa picha wa Paul Kagame katika Flickr na podikast za Paul Kagame na blogu za pK kwenye paulkagame.com

Itatupasa kusubiri na kuona upana wa athari ya vyombo hivi huria vya kijamii vya habari vya mtandaoni hasa kupitia uchaguzi wa rais wa 2010 nchini Rwanda.

Paul Kagame

Paul Kagame

4 maoni

  • DUSABEMUNGU Ange de la Victoire

    Wanablogu hawa nawashukuru kwa mchango mzuri huwo.Lakini ninachotaka kuomba mzee wetu Paul KAGAME ni kubolesha hali ya utangazaji habari na mawasiliano nchini.Sisi sote tunajuwa kwamba mgombea huyu atateuliwa ,kutokana na kura ya maoni iliyofanyika.Na atakapoingia madarakani kwa muhura ujawo tunamuomba ashughurikie nchi nzima ili kuboresha sekta ya habari,kwani mwanakijiji hatajua nini kinachoendelea katika uboreshaji wa kilimo bila kupata habari kuhusu hilo jambo.Wanahabari wapatiwe habari iwezekanavyo,hapa namaanisha access to information,kutoka kwa viongozi mbalimbali.Habari ni njia inayoelekea kwa maendeleo.Kagame endelea na kampeni UTASHINDA,natakia pia wapinzani wako amaani na kukubari matokeo kwani asiyekubari kushindwa si mshindani.Asanteni.

  • Ndugu DUSABEMUNGU

    Asante sana kwa maoni yako. Tumefurahi sana jinsi unavyofuatilia matukio mbalimbali kupitia ukurasa huu wa Swahili lingua. Bila shaka maoni yako yatawafikia walengwa na watayafanyia kazi. Tafadhali endelea kusoma ukurasa huu na kutushirikisha maoni yako zaidi.

    Asante

  • clique aqui…

    Rwanda: Wanaomuunga Mkono wa Paul Kagame Wabaini Nguvu ya Twitter, Facebook na Blogu…

  • juegos infantiles de habilidad…

    Rwanda: Wanaomuunga Mkono wa Paul Kagame Wabaini Nguvu ya Twitter, Facebook na Blogu…

Sitisha majibu

jiunge na Mazungumzo -> DUSABEMUNGU Ange de la Victoire

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.