Ghana: Je Una Chumba cha Ziada kwa Ajili ya Rais wa Zamani Rawlings?

Former president of Ghana Jerry Rawlings, spea...
Picha kwa kupitia Wikipedia

Nilisikitishwa kidogo jana pale nilipoona kichwa kikubwa cha habari katika tovuti ya Modern Ghana “Rawlings Hana pa Kuishi”.  Jerry Rawlings ni rais wa zamani wa Ghana. Nilishtushwa sana baada ya kusoma kipande kidogo tu cha habari hiyo.Mwezi Februari, 2010 moto mkali ulioelezwa kama ‘wa ghafla na haraka” uliteketeza makazi ya Rais wa zamani Jerry Rawlings na haukubakisha kitu chochote kilichoweza kuokolewa kutoka kwenye mabaki ya moto huo.

Moto huo ulielezwa kuwa ulianza mnamo majira ya 10 na dakika 20 Saa za GMT wakati wa mvua kubwa iliyombatana na kukatikakatika kwa umeme. Wakati hakuna maisha yaliyopotea, janga hilo liliacha “sura ya kusikitisha” ya mabaki ya nyumba ambayo wazima moto walijaribu bila mafanikio kuyaokoa kwa masaa matatu.

Moto huo uliunguza Karibu kila kitu chenye thamani na wakati wazima moto walipomaliza kuuzima moto huo; kila kitu kilikuwa ni majivu isipokuwa kuta za zege na nguzo.

Kwa mujibu wa tovuti ya Modern Ghana kiongozi huyo wa zamani wa Ghana pamoja na mkewe hawana makazi na wanatafuta kwa haraka sehemu ya kupanga mjini Accra.

Kadhalika inaripotiwa kwamba rais huyo wa zamani alipaswa kusafiri kutoka katika “nyumba ndogo ya vijijini” Tefle katika mkoa wa Volta mpaka kwenye mji mkuu wa Ghana, Accra kwa ajili ya mikutano pale anapohitajika wakati mkewe kwa wakati huu anaishi na mama yake katika kitongoji cha Janiba; hali ambayo inaathiri ndoa yao.

Kwa mujibu wa mke wa rais huyo wa zamani, Nana Konadu; wakati makazi yao ya huko Ridge yalipoungua tarehe 14, februari; serikali iliahidi kutafuta makazi mbadala kwa ajili yao lakini miezi 5 baadaye, ahadi hiyo ya serikali iko mbali na kutimizwa. Pia alilalamika kuwa makazi ya Ridge yangeweza kuokolewa kama nyumba ingekuwa na upatikanaji wa maji wa uhakika kwani wakati wazima moto walipowasili, walikuwa na maji kidogo tu kwenye mitungi yao na walifikiri kuwa wangeliweza kupata maji zaidi pale nyumbani.

Hebu tuangalie maoni ya wanablogu wa Ghana na wasomaji wao kuhusu suala hili. Obed Nanayaw Sarpong haelewi kwa nini familia hiyo ya kwanza ya zamani inadai nyumba kutoka kwa serikali:

Mapema wiki iliyopita, mke wa rais wa zamani, Nana Konadu Agyemang Rawlings alikuwa na mahojiano na Joy FM mjini Accra ambayo kwayo aliongelea kwa upana kuhusu jinsi ambavyo maisha yake ya kifamilia yalivyoathirika baada ya kupoteza makazi yao ya Ridge. Sikuweza kujizuia kucheka. Nilichukia kwamba utabiri wangu wa takriban miezi 5 kuwa familia ya rais wa zamani ingedai nyumba mpya kutoka kwa serikali, na watu wan chi hii, ungetimia. Mengine yote, tutayaona.

Kama nchi, inatubidi tufute vipengele kwenye katiba ambavyo vinatoa nyumba 3 au zaidi pamoja na magari n.k. kwa watu ambao walilitumikia taifa hili. Maoni yang uni kuwa ikiwa wanaipenda nchi vya kutosha kama ninavyoipenda mimi, wangeruhusu fedha hizo zitumike katika kuhakikisha watu wan chi hii wanapata maji safi na salama ya kunywa, sehemu za ‘kujisaidia’ (ikiwa wote wanakula vizuri), shulke n.k. Vitu ambavyo hawakuweza kuvitoa wakati walipokuwa na rasilimali za kufanya hivyo!

Mike anaijibu makala ya Obed kwa kusema:

Wamepoteza makazi yao ya Ridge? Kwa nini wasiishi katika nyumba yao ya Adjiringanor? Vipi kuhusu ile iliyo Karibu na mto Volta pale Karibu na daraja la Sogakope? Hawazimiliki tena nyumba hizo? Hii ndiyo sababu ya kusisimka kwa waGhana kublogu. Wale waliojaa upuuzi wataonwa. Kama rawlings angelikuwa na blogu mwaka 1978, 1979, tungelikuwa na ushahidi wa kile kilichomsukuma madarakani na kile alichokisimamia. Unafiki katika ngazi fulani umeiumiza nchi hii na bila ya shaka unaendelea kutukwaza.

Obed Nanayaw Sarpong anajibu maoni ya Mike:

@Mike,wanasema kuwa nyumba haijamalizika kujengwa – kuna ukuta wenye urefu wa mita 10 unaozunguka nyumba hiyo. Mke wae anasema kuwa Bw. Rawlings anaishi kwnye nyumba ya Tefle n ani tatizo kwao.
Ninasikitishwa sana wakati hawa watu bila aibu wanapotaka kutunyonya.

Mwandishi mwenye kejeli wa Ghana: Ato Kwamena Dadzie “Chukua mkopo wa nyumba, Bw. Rawlings”:

Karibu kila kitu alichosema Bi. Rawlings katika mahojiano yale kilionekana kulenga kuwarubuni Waghana wafikirie kuwa familia yake imo kwenye hali mbaya na kulazimisha mkono wa serikali kupandisha dau lake, huku akijua fika kuwa amekataa serikali kila dau la makazi mbadala lilitolewa na serikali. Nilianguka kijinga kwenye hila zake. Niliketi kando ya redio na kusema serikali haikuwa na kisingizio kwa kushindwa kwake kutoa makazi mbadala kwa familia ya Rawlings – miezi mitano baada ya kitu (au mtu) kuiunguza nyumba yao. Sikuwa peke yangu. Wengine pia walikasirishwa na serikali haikuwa na jingine la kufanya isipokuwa kujitokeza haraka na kukana madai yake kuwa hakuna lolote lililofanywa ili kuipatia familia yake nyumba”

Pamoja na hilo, swali moja lilikuwa mbele zaidi ya akili za Waghana. “Ah, Rawlings,” mtu mmoja aliuliza. “Baada ya miaka 19 madarakani kama mtawala wa kiimla, je anasema kuwa hajajijengea nyumba?”

Ato anamshauri Rawlings aende kwenye Shirika la Mikopo ya Nyumba la Ghana ili akachukue mkopo::

Hapo ndio pengine inabidi tufike. Ni mshahara mzuri tu anaoupata rawlings. Kama jumba lake la kifahari la Mashariki ya Legon halifai kwa ajili ya kuwa makazi yake ya kimapinduzi, basi inampasa aende Kwenye Shirika la Mikopo ya Nyumba la Ghana akachukue mkopo wa nyumba. Mara ya mwisho nilipoangalia, mwanawe wa kiume, Kimathi, anafanya kazi na Benki ya Fidelity. Nao pia wanatoa mikopo ya nyumba. Na aende akachukue mkopo.

Nyumba ya kuritaya ya George Bush haikutolewa na serikali ya Marekani. Tony Blair na Gordon Brown wanaishi katika nyumba zao wenyewe. Na Kufuor pia. Siyo kama ni jambo lisilowezekana kwa Rawlings kuhamia katika nyumba yake mwenyewe. Ana bahati sana tu kwamba ile nyumba yake inayoitwa “nyumba ya vijijini” kule Tefle ipo kwenye kingo za mto. Gordon Brown angeua ili aipate hiyo nyumba.

Kama unakuwa rais wa taifa hili, unachukua mshahara pamoja na marupurupu mengine kadhaa ambayo yanafanya pasiwe na ulazima kwako kutumia pesa zako mwenyewe na hauwezi kujenga nyumba yako mwenyewe kasha unageuka na kutegemea kuwa serikali ikupatie makazi wakati ukiritaya, basi wewe si mwingine zaidi ya mjinga mkubwa.

Palikuwa na wasomaji 40 ambao waliacha maoni wakati tunaandika makala hii. Yafuatayo ni baadhi ya maoni ambayo wasomaji waliyaacha:

Banske anamchukulia Rawlings kama Mghana mrubuni na mvivu zaidi ya wengine wote:

Hmmmmm!!!
Kwaku Baako anasema kuwa rawlings ni Mghana mwenye bahati zaidi hilo ni kweli na kwa nyongeza ninasema kuwa Rawlings ni Mghana mrubuni na mvivu zaidi ya wengine wote. Kwa wale ambao mnaendelea kurubuniwa (kama ni kweli au mnajishaua) na akina Rawlings, hivi sasa vitendo vyao vya ulaghai vimewekwa wazi, je hamkubaliani na mimi kuwa kuwa Rawlings ni mtu mbaya zaidi kutokea katika uwanja wa siasa wa Ghana?
Anafanya nini na pesa zilizoketi katika akaunti yake huko Uswisi? Mshenzi asiye na aibu. Yule anyechoma nyumba moto ataungua kwa moto!!!

Anna G anasema:

Kwangu, haileti maana kabisa kwamba pesa za walipa kodi wadogo zitumike kuwapa makazi marais wa zamani. Kwanza, walikuwa wanalala wapi kabla ya kuwa marais? Angalia mapendekezo ya ajabu aliyoyatoa Kuffuor kwamba afanyiwe pale atakapo sio rais tena. Kwangu wote wanafanana: wabinafsi, kwa ni wanafahamu fika kwamba kodi inayokusanywa hapa nchini haitoshi. Ikiwa wanasiasa na viongozi wataendelea kuwa wabinafsi namna hii, basi nachelea kuwa uchumi mbaya wa Ghana hautagomboka kamwe na tutaendelea kuwa nchi maskini ya ulimwengu wa tatu.

Frank Anderson anaafikiana na msimamo wa Ato:

Ato siwezi kufanya vingine zaidi ya kuafikiana na wewe.
Sioni maana yoyote ya kutumia pesa za walipa kodi ili kujenga nyumba za marais wa zamani ati kwa sababu tu kwamba waliwahi kuwa vingozi wan chi. Inaudhi n ani jambo la kusikitisha. Na suala hili limetawala mijadala kwa majuma? Yesu Kristu!!! Ndio kisifa cha viongozi wa Afrika. Hata vijana wadogo wa miaka 23 wanaanza kufikiria hatua watakazochukua ili kujijengea nyumba je iweje basi kwa rais wa zamani. Familia ya Rawlings wajiepushe na aibu hii kwa kumalizia nyumba yao.

Kweku Diyifo anasema kuwa huku ni kujindanganya:

Nilipomsikia Bi. Rawlings kwa mara ya kwanza katika redio kwamba wanatafuta sehemu ya kupanga, nilijiuliza, “je ni kujindanganya kwa namna gani huku?” baada ya kukaa madarakani kwa miaka 20? Baada ya kulipia ushuru wa GHC90,000 kwa ajili ya magari yaliyoagizwa kutoka nje, papo hapo? Baada ya kuwalipi watoto wa marafiki zao karo za masomo nje ya nchi? Na orodha hiyo inaendelea bila kikomo. Waghana wengi wanaweza hata kuamini, n ani sawa tu, kwamba Rawlings ana zaidi ya majumba mawili makubwa ambayo wamepata shida kukubali kwamba wanayo.
Ninafahamu kutokana na uzoefu wangu mdogo kwenye biashara kuwa, kutokana na nguvu zao za kiushawishi kote nyumbani na nchi za nje, ingechukua sim utu kwa akina Rawlings ili kupata nyumba yenye heshima na ya kufaa sehemu yoyote nchini Ghana. Kama unacho na unasema kwamba huna, hilo ni shauri lako. Lakini mimi, na wengine wengi kama mimi hawawezi kudanganywa.

Sero anahitimisha suala zima kwa neno moja tu:

… kwa neno moja, huu ni upuuzi

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.