China: Uchi Ulio Rasmi

Serikali moja ya mji huko katika Jimbo la Sichuan sasa inaitwa “Serikali ya Kwanza nchini China Iliyo Uchi kabisa” baada ya kuwa maafisa wa mji huo kuweka mishahara na matumizi ya serikali kwenye tovuti. Kutajwa kwa suala la ‘uchi au utupu’ katika machapisho mengi ya Kichina katika siku za karibuni kunaelezea kiwango kikubwa ajabu cha uwazi katika serikali ya mji.

Serikali ya mji wa Baimiao upande wa kaskazini mashariki mwa Sichuani uliweka hadharani mpango wake wa matumizi ya mwaka 2010 mnamo Machi 12, ikiwa ni pamoja na kuweka bayana mishahara ya watumishi wake pamoja na taarifa za matumizi ya mwaka 2009, ripoti hii ni kwa mujibu wa Southern Weekend.

Kwa mujibu wa gazeti la The Sichuan Daily Post, taarifa zilizo kwenye tovuti ni zaina mbalimbali kuanzia magari, burudani na malipo ya makulaji, vikombe vya karatasi, vifaa vya ofisi, bahasha, na taarifa zote hizi zimewekwa kwenye tovuti ya mji huo.

Maafisa katika ngazi zote za serikali nchini China wanasifika kwa kuja na malipo ya juu sana hasa pale wanapowaandalia hafla wageni na makada wengine wa ngazi za juu. Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali katika vyombo vya habari vya China, hatua hizi za kuweka mambo wazi huenda zitawasaidia raia kusimamia matumizi yanayofanywa na serikali yao.

Maendeleo haya yamekuja katika kipindi ambacho mikoa nchini China imeanza kufanya majaribio ya mfumo kama huo unaohitaji maafisa kutoa taarifa kuhusu vipato vya familia zao na miradi wanayoendesha. Mkoa wa Altai katika jimbo la Xinjiang ilitekeleza mfumo wa kutoa taarifa yakipato katika mwezi Januari 2009.

Lakini Mkoa wa Baimiao ni serikali ya kwanza ya ngazi hiyo kuweka ripoti kamilifu ya matumizi, kwa hiyo imejipatia jina la “Serikali Iliyo Uchi Kabisa”. Kwa mujibu wa maoni ya mtandaoni, maendeleo haya huenda yakazisukuma serikali za mikoa mingine nazo kutoa taarifa kamili za mapato yao na kuongeza uwazi. Wengine wameeleza hatua hiyo kama kanya boya.

Makala iliyochapishwa katika Qingming na Guyu imeisifu hatua ya “serikali hiyo iliyo uchi” kama inayothubutu kufanya jambo gumu lakini makala ilidai mabadiliko yaliyo ya uhakika zaidi.

Ingawa bado hawajavua nguo kabisa, mwandishi angependa kupongeza ujasiri wa Baimiao. Kwa vyovyote vile, kama kuthubutu kuweka hadharani gharama za burudani zinazofanywa na maafisa wa ngazi za juu ni jambo linaloweza kuitwa kanya boya, basi natumaini tu kwamba ni afadhali tuwe na maafisa kama hawa wengi hata kama ni kanya boya.

Mwanablogu Cao Rongxiang amefurahishwa na maendeleo haya katika uwazi serikalini. Mwandishi huyu anazipa changamoto serikali nyingine kuiga mfano huo lakini anasema kwamba zinakosa viungo muhimu vya kufanya mageuzi kama hayo.

Licha ya kutoa pongezi zangu kwa serikali ya Baimiao kwa hatua hiyo ya kijasiri, ningependa sana kutoa wito kwa serikali za mikoa nchini kote kuweka hadharani masuala yao ya fedha kama njia ya kweli ya kudhibiti ufisadi katika matumizi ya fedha za serikali. Lakini baada ya kutafakari sana, sababu iliyoisukuma serikali ya Baimiao kuthubutu kuweka hadharani matumizi yao kwa kina ni kwa sababu maofisa wao wanamiliki [vionjo vinne]. Na huenda jambo hilo lisiwezekane kila mahali nchini, au katika kila ngazi ya serikali, si rahisi kumiliki [vionjo hivi vinne].

Mwandishi huyo anaviorodhesha vionjo hivyo kuwa ni hasira, mgandamizo, nguvu na ujasiri na kuongeza kuwa uwekaji huu hadharani wa siku za karibuni ni matokeo ya serikali ya mkoa kuonja kutoridhishwa kwa watu na nguvu waliyo nayo.

Makala katika Gaoyuan zhixin inasema mabadiliko hayo katika Mji wa Baimiao yatakuza kiwango cha maelewano kati ya serikali na watu.

Serikali haikuwa na ujasiri wa kuweka taarifa hizi hadharani. Kuimarisha usimamizi wa watu kuhusu mali yao imekuwa ni msemo uliojaa utupu…Serikali kutangaza hadharani masuala yake na kupokea kwa mikono miwili usimamizi wa watu siyo tu kwamba hali hiyo inapunguza mgawanyiko uliopo kati ya serikali na watu, lakini pia jambo hili litawafanya watu waelewe vizuri na kuiunga mkono serikali yao hasa pale ambapo kutakuwa na matatizo.

Si maoni yote yaliyotumwa mtandaoni yako chanya kiasi hicho. Mwanablogu Liu Changfeng ana mashaka na uwazi ulioonyeshwa na serikali ya Baimiao.

Bila shaka hakuna tatizo kwa kuita kitendo hiki kama kanya boya. Ukiachilia mbali kutilia shaka hali hii kuwa kama kanya boya, unaweza kabisa kutilia mashaka uhalali wa uwekaji huu bayana wa mambo. Unaweza pia kusema wazi kabisa kwamba huenda hakuna lolote hapa zaidi ya kuweka habari iliyotengenezwatengenezwa na kupunguzwa hapa na pale kisha unamwonyesha kila mtu, huenda data zenyewe hasa wala haziko hivi.

Katika makala nyingine inayoeleza kitu kinachofanana na hiyo nyingine, hiyo ilichapishwa katika Southern Weekend yenyewe ilisema matumizi ya burudani na kuandaa hafla yaliyodaiwa kufanywa na serikali ya Baimiao katika uwekaji wake bayana hivi karibuni ilikuwa ni asilimia moja tu ya matumizi halisi yaliyopendekezwa. Kiasi hicho kimeibua mashaka kutoka kwa maafisa walio na tabisa za kuandaa hafla.

Mageuzi nchini China daima yamekuwa ni mchakato wa kutoka chini kwenda juu. Mfumo wa Uwajibikaji wa Kaya, ambao ndiyo ulikomesha kilimo cha pamoja na ambao ndiyo ulisaidia kuleta mavuno makubwa, ulianzishwa na wakulima mwaka 1978 na hatimaye kuingizwa katika sheria mwaka 1981. Mikoa katika majimbo ya Xinjiang, Zhejiang, na Hunan hivi sasa inafanya majaribio ya mfumo wa kutolea taarifa vipato kwa ajili ya maafisa wakati ambapo nchi nzima kwa ujumla wake imekuwa ikisita kukazia kanuni za aina hiyo.

Huku ikiwa imepata usikivu wa vyombo vya habari vya Kichina na kupata uungaji mkono mkubwa kutoka kwa watu, “Serikali iliyo uchi” ya Baimiao huenda ikawa ndiyo mwanzilishi serikali zinazoanzia ngazi ya chini miongoni mwa watu.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.