Somalia: Je Serikali Inawaandikisha Vijana Wa Kikenya Kwa Ajili Ya Vita?

Huu ni muhtasari wa kwanza wa blogu za Kisomali mwaka 2009. Naam, ni zaidi ya mwaka mmoja tangu nilipochukua likizo ya muda mrefu kutoka kwenye shughuli za kublogu lakini sasa nimerudi, moja kwa moja. Hii ni makala ya kwanza na tarajieni makala zaidi zinazohusu ulimwengu wa blogu za Kisomali.

Mwanablogu Royale Somalia anatoa wasifu wa daktari mdogo wa kike jijini Mogadishu ambaye alimaliza masomo mwaka jana, anaandika:

Mwezi Desemba mwaka 2008, wanafunzi 20 walishinda vigezo vikubwa na kufuzu kutoka chuo cha uganga huko Mogadishu – kundi la kwanza kufanya hivyo katika takriban miongo miwili ndani ya nchi iliyoshindwa katika pembe ya Afrika.

Dr. Hafsa Abdurrahman Mohamed, 26, alikuwa ni mmoja wa waliopokea stashada kutoka katika Chuo Kikuu cha Benadir jijini humo. Wakati anamaliza masomo yake aliamua kufanya kazi kwa Waganga Wasio na Mipaka/ Médecins Sans Frontières (MSF), kwa kutumia ujuzi wake ili kutoa huduma za bure za afya nchini Somalia.

Mwanafalsafa wa Afrika ya Mashariki anatoa maoni juu ya ziara ya Rais Sharif Ahmed nchini Marekani na mabadiliko ya sera ya serikali ya Marekani katika mahusiano yake na Sharif:

Mwezi Desemba 2006, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, ambaye hivi sasa ni rais-kwa-jina-tu wa Serikali ya Mpito ya Shirikisho la Somalia, alikuwa analikimbia jeshi la Ethiopia, CIA, pamoja na wanamgambo wa Marekani.


Mwanafalsafa wa Afrika ya Mashariki
anaendelea:

Wiki hii Sheikh Sharif yuko Minneapolis, MN (na nyumbani kwa mbunge mwendawazimu wa kike wa bunge la chini la Marekani) anakutana na wabunge, Gavana na madiwani/Meya. Miezi miwili iliyopita alikuwa na mkutano na Katibu Clinton jijini Naorobi wakati wa ziara yake ya Afrika. Kutokea gaidi mpaka kuwa rais kwa Sheikh Sharif katika miaka miwili. Jambo hilo, marafiki, ni lazima limetokea kwa mara ya kwanza. Kwangu mimi hili linaongea vikubwa kuhusu sera mbaya ya nchi za nje ya Marekani zaidi ya jingine lolote.

The Kenya Somali Blog anasema kuwa Serikali ya Somalia inawaandikisha vijana wa Kisomali kutoka Kenya:

Serikali ya Somalia inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa imewaandikisha zadi ya vijana 170 wa Kikenya na wanamgambo wa zamani ili wakasaidie kupigana na waasi katika nchi iliyoshindwa ya pembe ya Afrika, viongozi walio katika maeneo ya mashariki ya Kenya wamesema.

Mohamed Gabow, Meya wa Garissa, aliiambia Reuters kuwa uandikishaji huo wa vijana wa Kikenya wenye asili ya Kisomali ulikuwa unafanywa katika nyumba moja kwenye kijiji cha Bulla Iftin, kilichopo pembezoni mwa mji wake.

Uandikishaji huo sio siri. Wanaohusika hawaogopi. Wanakwenda vijijini kote kutangaza zoezi hilo,” Gabow alisema katika mahojiano siku ya Alhamis.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.