Uganda: Blogu,Twita Zaipasha Habari Dunia Wakati Machafuko Yanaendelea Mjini Kampala

Wakati machafuko yalipoitingisha Kampala, mji mkuu wa Uganda, kwa siku ya pili, wanablogu na watumiaji wa intaneti waliungana ili kuupasha ulimwengu habari.

Katika masaa 24 ya machafuko ya kwanza, wananchi wa Kampala waliizindua Mashahidi wa Uganda, tovuti inayoripoti machafuko na ambamo Waganda wanaweza kupashana habari za vifo, uporaji, uwepo wa maaskari wa serikali na habari nyingine zinazohusiana na machafuko hayo. Mpaka ilipofika Ijumaa mchana (saa 9 za GMT) tovuti hiyo ilipokea ripoti nyingi za machafuko katikati ya jiji la Kampala na vitongoji vingine vya jiji hilo.

Picha kutoka UgandaWitness.net inayoonyesha sehemu yaliporipotiwa machafuko

Picha kutoka UgandaWitness.net inayoonyesha sehemu yaliporipotiwa machafuko


Katika miezi michache iliyopita mwanablogu wa Kiganda The 27th Comrade amekuwa akitengeneza mfumo wa huduma ya kutuma ujumbe wa twita na kuandika Facebook kwa kutumia njia ya simu za Uganda Telecom. Kutokana na machafuko siku ya Ijumaa, aliizindua huduma hiyo mapema kwa kutuma maelekezo kwenye blogu ya jamii The Kampalan, huku akiwahakikishia uwepo wa faragha kwa watumiaji:

Sasa, hali katika mji wa Kampala imesababisha kutangazwa mapema kwa huduma hii. Nini cha kufanya? Binaadamu hupanga mipango, miungu inaamua.

Kwa ufupi, hakuna kuchujwa kwa habari, hakuna woga, na hakuna upendeleo. Tumeni habari. :0) Mazungumzo hayatanaswa kwenye mfumo kiasi cha kuidhuru faragha, na kwa kweli mambo mengi ni magumu (kama vile kujiandikisha, kuandika ujumbe) kutokana na ukweli kuwa faragha yako inapewa heshima.

Ujumbe wa twita kutoka kwa mkazi wa Kampala na mtumiaji mpya wa twita dgel unaowaasa watu watumie huduma ya Twita kueneza habari za machafuko umekuwa ukisambazwa katika jamii ya watumiaji wa twita. Anaandika:

@dgel: “ kwa yeyote aliye Kampala, tafadhali mfundishe japo mtu mwingine mmoja kutumia twita, na wapeni moyo wa kutupasha habari kama zinavyotokea. #kamplala

Habari kutoka katika vyombo vikubwa vya habari zimezidi kuwa adimu baada ya serikali kuwakamata wanahabari na kufunga stesheni za redio jijini kote. Joe katika Uganda Talks anafafanua:

Jana usiku wasomaji walifahamu kuwa stesheni maarufu ya Kiganda CBS iliondolewa hewani kwa madai kuwa ilikuwa ikichochea machafuko na kuwahamasisha wanaofanya ghasia. Leo hii kadhalika, Serikali imesitisha leseni za Suubi FM, Radio Sapientia na Radio Two Akaboozi Kubiri kwa madai hayo hayo.

Mwanablogu Fresh Apples ambaye amekuwa akituma habari kadri zinavyotokea tangu machafuko yaanze, anaripoti kuwa serikali imeweka walinzi katika milingoti ya kurusha matangazo ya redio CBS huko Buziga Hill jijini Kampala:

Redio CBS haipo hewani – inasemekana imefungwa na serikali

Redio CBS haipo hewani – Maaskari wa jeshi wanailinda milingoti huko Buziga

Ripoti nyingine za twita zinazotokea kwa Waganda mjini Kampala zinaashiria kuwa serikali inawalenga pia wanahabari:

@magamuya: “mwanahabari wa VoA (Idhaa ya ndani ya masafa ya FM) amekamatwa huko Kayunga baada ya machafuko ya Kampala, pengine yuko kwenye selo ya polisi mahali fulani. Mwanahabari wa NTV alikamatwa kwa muda mfupi”

@uginsimniac: Moses Kibuuka (NTV) & Yahaya Iga Muyigo (Sauti ya Afrika) walikamatwa huko Kayunga leo na wameachiwa kwa dhamana. Vifaa vyao bado vimeshikiliwa. #Kampala

Kwa mujibu wa wakazi wa Kampala, idhaa za televisheni na redio ambazo bado zipo hewani zinatangaza habari kidogo au hazitangazi kabisa kuhusu machafuko. Tumwijuke anaandika katika Ugandan Insomniac:

Je redio ni za nini kama si kwa ajili ya kutangaza habari mpya mara moja? Je zilikuwa wapi huduma za kupiga simu redioni? Kwa nini hakuna mijadala juu ya ushenzi wa waaandamanaji wengi? Yako wapi mahojiano na Ufalme wa Buganda, polisi na serikali? Zikowapi huduma za kupiga simu redioni kutoka miji ya Masaka, Nyendo, Kayunga na Mukono ambako machafuko yalitokea. Kwa nini hakuna mjadala juu ya uhuru wa vyombo vya habari? Kwa nini hakuna mjadala juu ya kwa nini kuna Baraza la Utangazaji?

Kila habari ninayopokea kuhusu hali ya mjini Kampala ninaipata kutoka kwenye Twita, Facebook na blogu.

Sara wa blogu ya The Malan Family anaandika:

Idhaa ya televisheni ya TV Uganda inaonyesha video za muziki na NTV inaonyesha “That’s So Raven” *anavingirisha macho yake kwa kejeli*. BBC ina mwanahabari anayeripoti (…. Kutokea Nairobi) kwa hiyo nina hakika anazo *habari zinazotokea kila dakika* kwa ajili yetu!!!!!

Watumiaji wa Twita nchini Uganda pia waling’amua uchache wa habari zinazohusu machafuko:

@CamaraAfrica: “Wow… kila mtu aharakishe na kuwasha NBS kwa ajili ya ripoti ya kusisimua inayohusu… jinsi ya kucheza gofu. #kampala

@solomonking: Aaagh!! UBC inaonyesha programu fupi inayokera ya NLP na Ethan Mussolini kwa mara karibu 5 katika masaa mawili na bila ya kutangaza chochote juu ya machafuko!! #kampala

Jon Gos mwanzilishi wa kampuni ya nyenzo za kompyuta nchini Uganda Appfrica na mdhaminiwa wa TED, alishangazwa na kasi ambayo Waganda waliitumia Twita kusambaza habari:

Moja ya mambo yaliyonishangaza ni jinsi ambavyo watumiaji wachache wa Twita walivyoweza kuendesha uenezaji wa habari ambao watu wengi waliutumia. Kama vile ambavyo mimi na wengine kama @camaraafrica, @mugumya, @solomonking tulivyokuwa tukisikia habari mpya hapa Uganda, tuliandika mara moja kwenye twita na Facebook, njia yetu pekee ya kuufikia ulimwengu wa nje.

Katika makala nyingine kwenye blogu ya Appfrica, Jon anaandika:

Vyombo vikuu vya habari vinafahamu nini kinachoendelea lakini vyombo vilivyopo ndani ya nchi vimefungwa. Ama kutokana na msululu mkubwa (kwenye mtandao) au vinginevyo. Wengi wetu, walio nje au la wanaitegemea twita kwa ajili ya kupata habari.

Picha kwa hisani ya Sarah wa a href=http://themalans.blogspot.com/2009/09/never-dull-moment.htmlThe Malan Family/a. Anaandika: “Tumefikia hitimisho kwamba lilikuwa am ani bomu la machozi au bomu la moshi kwa sababu tuliona watu wakikimbia kuelekea pande tofauti baada ya mlipuko.”

Picha kwa hisani ya Sarah wa <a href="http://themalans.blogspot.com/2009/09/never-dull-moment.html">The Malan Family</a>. Anaandika: “Tumefikia hitimisho kwamba lilikuwa am ani bomu la machozi au bomu la moshi kwa sababu tuliona watu wakikimbia kuelekea pande tofauti baada ya mlipuko.”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.