Rais wa Marekani Barack Obama alitoa hotuba yake Ghana ambayo inaweza kuchukuliwa kuwa kama hotuba ya sera yake ya Afrika. Wakameruni wa nyumbani na wale wa ughaibuni wamekuwa wakijadili maneno yaliyotamkwa na Kiongozi wa Marekani mwenye asili ya Afrika kwa kupitia ulimwengu wa blogu.
Hotuba yote ilichapishwa kwenye blogu ya Up Station Mount Club ambayo ni maarufu sana kwa wanablogu wa Kikameruni wanoblogu kwa Kiingereza. Maoni yanatoa picha ya kuwa watu wameikubali hotuba hiyo angavu lakini wana wasiwasi na kauli tamu.
Augustine S, Mkameruni anayeishi Kanada anaonekana kuridhishwa na hotuba hiyo iliyokemea ufisadi moja kwa moja pamoja na utawala mbovu lakini anataka zaidi:
Hotuba ilitolewa vizuri. Ilizidi matarajio. Alizungumzia ufisadi na Utawala mzuri, ndicho ambacho nilipenda kukisikia. Viongozi wa Afrika wanakuwa kikwazo cha maendeleo ya nchi zao. Ninatamani Uongozi wake uende mbele zaidi kuwaumbua viongozi mafisadi wa Kiafika, uwaadhibu kwa kushikilia mali zao na kuwazuia wao na familia zao kusafiri. Obama ni aina ya kiongozi tunayemuhitaji katika dunia ya leo.
Bado akiwa kwenye suala la kupambana na rushwa na ufujaji wa viongozi wa Afrika, Oyez ana ushauri kwa viongozi wa Magharibi kama Obama:
Ni mambo mawili tu yanahitajika, na tutafika mbali:
1) Wanyimeni Viongozi wa Kiafrika, na familia zao na maswahiba wao haki ya kuwa na akaunti za benki na mali ya aina yoyote nje ya nchi.
2) Wazuieni watawala wa Afrika kupata matibabu aina yoyote nje ya Afrika.Hayo ni masuala mawili pekee tunayoomba Wamagharibi wayafanye, na sisi tutayashughulikia yaliyobaki.
Maoni yaliyoachwa hapo na Nnokko Johnson yanaisogeza hotuba ya Obama mlangoni mwa Kameruni kwa kumkumbusha Rais wa nchi hiyo, Paul Biya, ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1982 na mwaka 2008 alibadili katiba ili kuondoa ukomo wa vipindi vya Rais kukaa madarakani:
Afrika haiwahitaji viongozi wababe, inahitaji taasisi shupavu.
Bw. Biya tafadhali iangalie sana sentensi hii na ujifunze, hatusemi uondoke, lakini tunahitaji taasisi zenye nguvu, tafadhali, tafadhali…
Hatahivyo, kwa kusoma maoni mengi yaliyowekwa pale, mtu anaweza kuondoka na wazo kuwa Wakameruni wanaiona hotuba ya Obama kama “mazungumzo mazuri” ambayo hayawezi kuwatatulia matatizo yao. Emmanuel anasema:
Mbio za nyumbani (goli la kisigino). Sema, sema, sema, mambo ya kizamani, yasiyosaidia. Ni lazima muwe wawili ili kucheza tango, na Waafrika ni wazembe kusikiliza mihadhara inayohusu ufisadi kutoka kwa kiongozi wa Ufisadi wa kiuchumi, kimaadili, na kisiasa; ilihitaji watu wawili kuendesha biashara ya utumwa, ukoloni, na sasa kwenye kipindi hiki kipya cha “Ushirikiano.” Angalia, haya mazungumzo ya “ushirikiano” ni uwongo. Ni walio sawa kiukweli, na sio waliosawa kinadharia ndio wanaoweza kuingia katika ubia.
Hayo hayo…Ninajiuliza ni lini watu wataapocha kuamini na kuanza kutenda… Hatuhitaji hotuba za matumaini na ahadi –zinazopumbaza watu, kwamba matatizo yao yatatatuliwa –wategemee utatuzi. Mgogoro wa kifedha ulipoikumba Marekani, rais alisema hayo hayo kuhusu wajibu wa Wamarekani kuchukua majukumu… Lakini jamani, Wamarekani wengi hawana mamlaka na utawala wa maisha yao ya kifedha, hawawajibiki kabisa na na anguko la kiuchumi, lililotengenezwa na genge la waroho wa benki…
Naam, Hotuba za Obama huandikwa vizuri na wafanyakazi wanaojua vyema kufanya kazi ya kuleta matumaini. Nini kingine tukitazamie kutoka kwake? Hotuba zinazotoka moyoni kuhusu mambo ya halisi yanayoikabili dunia yetu ya sasa?
Mtiririko wa mawazo unaonekana kuwa huo, ni suala la Waafrika kutatua matatizo yao wenyewe. Kama Reex anavyosema,
…hebu Waafrika na tutafute masuluhisho yetu. Tunaweza baadae kumwalika Obama kula nasi mahindi ya kuchoma na karanga karibu na moto na kujadili siasa zenyewe –siyo mambo kitaaluma ya Ivy League wala mazungumzo ya kinafiki yanayoonyeshwa na Wamagharibi, zile hotuba zingeweza kuhifadhiwa kwa ajili ya nyakati nyingine, ambapo kila tumbo lenye njaa Afrika litakuwa limeshibishwa!
Maoni ya mtembeleaji anayeitwa Isat hayana diplomasia:
Tunachotakiwa kukitunza kama kikumbushi ni maneno haya: “Mustakabali wa Afrika uko kwa Waafrika wenyewe.
Halafu angalia: Obama si Mwafrika. Babu yake aliyewapikia Waingereza na baba yake walikuwa Waafrika. Yeye ni Mmarekani na anatetea maslahi ya nchi yake –haijalishi nyimbo ngapi tunaimba kumsifia.
Man wey yi get ear make yi hear.[msemo wa Kikameruni maana yake: neno kwa mwenye hekima linatosha]
Blogu ya pamoja ya Up Station Mountain Club, pia ina makala nyingine – Barack Obama akiwa Afrika: “Zaidi Ya Ndio Tunaweza”, ndio tunalazimika, kutoka kwa mwanablogu wa Kikameruni Aloysius Agendia anayewasihi Waafrika wafanye mabadiliko:
Ndio, Afrika inaweza kufanya mapinduzi dhidi ya uongozi potofu wa sasa na mipango yao isiyoeleweka ambayo imelisababishia bara zima umasikini. Zaidi ya ndio, tunaweza, ndio, ni lazima tufanyie kazi mabadiliko yanayosemwa ili kwenda mbele.
Blogu hii ina vionjo vya mirindimo vya ziara hii kama video inayomwonyesha mwanamuziki wa Kikameruni akimshabikia Barack Obama kwenye uchaguzi imewekwa pale. Wimbo ulitolewa na Tata Kingue kabla tu ya kuapishwa kwa Obama mwezi Januari 2009 na Gef’s Outlook imetoa tafsiri kidogo pale.