Papa Nchini Kameruni (2): Wazee Wa Kanisa, Upotofu na Siasa

Ziara ya kiongozi wa Kanisa La Katoliki nchini Kameruni mwezi huu wa Machi 2009 imepelekea baadhi ya wanablogu wa Kikameruni kuelekeza tochi zao kwenye matokeo ya kisiasa (kama yapo) yatakayotokana na ziara hiyo ya Papa nchini humo. Neba Fuh anayeblogu kwenye Voice of The Oppressed ni mmoja wa wanablogu hao:

Mara mbili, Hayati Papa Yohane Paulo wa Pili alizuru Kameruni na matokeo ya ziara hizo kwa umma wa watu ambao ni masikini hayakuwa zaidi ya furaha ya kidini iliyowagharimu michango binafsi pamoja na ile ya hazina ya serikali. Maswali yasiyo na majibu kuhusu vitendo vya ukandamizaji vya (rais) Biya yalibaki bila ya majibu.

Aloysius Agendia, mwanahabari ambaye pia ni mseminari wa zamani katika makala aliyoipa kichwa cha Ziara ya Papa Benedikti wa XVI AFRIKA: zaidi ya kauli za kiroho inaonekana kwamba angependa Kanisa lipinge vitendo vya dola na vya wanasiasa ambavyo vinaharibu maslahi ya umma badala ya kuvivika majoho ya kidiplomasia:

Tunalielewa Kanisa na Vatikani kama dola, kadhalika kama chombo cha dini, japokuwa lina maana pia ya kisiasa, na wakati mwingine linapaswa kuwa na diplomasia katika mtazamo wake. Kwa maoni yangu, dini ya kweli haipaswi kufumbia macho maovu, ukandamizaji, unyonyaji, ukoloni katika mifumo yake yote pamoja na maovu mengine. Kanisa Katoliki limefanya mengi na linaendelea kufanya lakini mengi zaidi bado yanapaswa kufanywa. Hata hivyo, diplomasia hata kama ni nzuri katika namna yake, haitakiwi kutumika sana katika Kanisa kwa sababu, beleshi ni lazima liitwe beleshi. Katika kujaribu kutumia mbinu “laini” ili kufafanua masuala mazito, ujumbe huweza kupotea au maana/na umuhimu, unaweza kuchujwa sana. Viongozi wa kanisa hawapaswi kuchagua kufanya karamu na wale walio madarakani, matajiri na wenye nguvu. Siyo lazima wawe na pamoja na wapinzani, lakini, inawabidi wasimame pamoja na wanyonge, wanaokandamizwa, wagonjwa n.k

Anajua wazi ni nini anachotegemea kutoka kwa Papa:

Kama kiongozi wa kiroho anayewakilisha matumaini, hatakiwi kutuambia tuendelee kungoja na kutumaini. Tunatumaini kuwa atakuwa na ujasiri wa kutosha kuwaaambia wale wanaokinza matumaini ya Wakameruni na Waafrika wawe angalau na hisia kwa wanaadamu wenzao au wananchi wenzao.

Kwenye upande mwingine, Voice of the Oppressed anajiuliza kama wazee wa kanisa hasa wale wa Kameruni wana maadili ya kutaka mabadiliko kutoka kwa wale wanaotawala nchi wakati wao wenyewe sio mifano angavu:

Ni somo gani ambalo jamii iliyopotoka kimaadili inaweza kujifunza kutoka kwa askofu au padri ambaye anazaa watoto kiholela katika jamii yake?
Ni somo gani ambalo jamii inaweza kujifunza kutoka kwa padri mwenye wapenzi wa kike kadhaa kwenye jamii, kwa kisingizio kuwa ati “ni mwanaadamu” kama wanaadamu wengine?
Au anayedhamini safari ya rafiki huyo wa kike nje ya nchi, mbali na jamii, ili aweze kumzalia watoto, na pale anapochukua likizo au likizo ya masomo, anakaribishwa huko nje ya nchi na “mke” pamoja na “wanawe”?
Au mkuu wa shule ambaye ni padri, ambaye anafuja fedha za shule kwa kutumia hundi na mahesabu ya kughushi?
Au padri ambaye amegeuka kuwa mwindaji wa watoto wasio na kinga ambao wamewekwa chini ya usimazi wake?

Kwa Aloysius Agendia Papa Benedikti wa XVI anapaswa aongelee mwenendo wa hovyo wa viongozi wa Kikatoliki nchini Kameruni:

Wakati Baba Mtakatifu anapozuru Kameruni na Afrika, ni lazima akumbuke hili. Kwanza kabisa, Kanisa Katoliki na wengi wa (wachungaji) wake katika Kameruni wanahitaji “kurekebishwa” au “kukarabatiwa”. Habari nyingi zinazohusu uzinzi, ufujaji na tabia za utongozaji kwa baadhi ya mapadri wetu wakiwamo maaskofu, ambao wengine wanafika mbali hata kuzaa watoto, wengine wanafanya ngono na wanafunzi wao, wake za watu, wanaparokia n.k, ni lazima viongelewe…

Mwanablogu huyu anaamini kuwa kama masuala ya upotofu ndani ya Kanisa la Kikatoliki la Roma nchini Kameruni hatashughulikiwa na Papa, ziara hiyo haitakuwa na maana yoyote kwake:

Kuliweka rehani Kanisa na mali zake kwa ajili ya kuchukua “mikopo”, kama vile kumuuza Yesu Kristu tena kwa Faranga 950.000.000 kama vile Yuda alivyofanya kwa vipande 30 vya fedha. Hii inatokana na kanisa linalojulikana sana nchini Kameruni kuwekwa kama dhamana kwa ajili ya mkopo aliochukua mmoja wa maaskofu wake. Kuna kesi za kutisha za ufujaji ambazo zinabidi kutupiwa macho na Papa. Haya ni masuala ambayo ikiwa Papa atashindwa kuyashughulikia hata katika faragha na mapadri wake, basi ziara yake nchini Kameruni, ni lazima nikubali, kwamba itakuwa imeanguka chini ya matarajio.

Je Papa atathubutu? Hilo litakuwa ndio suala linafuatia kwenye ulimwengu wa blogu wa Kameruni.

Tafadhali Angalia: Sehemu ya kwanza ya makala hii inapatikana hapa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.