Haiti: Fanmi Lavalas na Uchaguzi Ujao

Mwishoni mwa juma lililopita, ulimwengu wa wanablogu wa Kihaiti ulikuwa umejaa habari za kutengwa kwa vyama vya siasa na Tume ya muda mfupi ya uchaguzi kwenye uchaguzi wa maseneta utakaofanyika mwezi Aprili 2009 , na siku ya tarehe 6 Januari, tume hiyo, CEP, ilichapisha orodha ya wagombea ubunge watakaokwaana kwenye uchaguzi ujao wa bunge nchini Haiti. Kwenye blogu ya Alterpresse [Fr], Vario Serant ameweka orodha ya wagombea walioachwa:

Mgombea mwingine aliyetemwa ni Mkurugenzi wa “Coeurs Unis” David Chery, ambaye amejiandikisha kwa tiketi ya chama cha Alyans (“Alliance pour l’avancement d’Haïti”).

Pia umefika mwisho wa kiongozi wa Chama cha Ujenzi wa Taifa au “Front pour la reconstruction nationale” (the National Reconstruction Front), Guy Philippe.

Katika orodha iliyochapishwa na Tume ya Muda ya Uchaguzi, ni theluthi mbili tu ya wagombea waliojiandikisha ambao wamekubaliwa kuingia kwenye kinyang’anyiro, lakini jambo la kustaajabisha zaidi ni hili la kuwakataa wagombea wote wa chama cha Fanmi Lavalas. Alwatan Radiokiskeya anaonglea uamuzi huo hapa [Fr]:

Usiku wa Alhamisi, Tume ya Muda ya Uchaguzi ilichapisha orodha ya wagombea 65 kati ya 105, ambao wamepitishwa ili kugombea uchaguzi wa maseneta tarehe 19 Aprili 2009.

Hakuna mgombea wa chama cha Fanmi Lavalas aliyeorodheshwa. (Fanmi Lavalas ni chama cha aliyekuwa Rais wa nchi hiyo, Jean Bertrand Aristide) Orodha zote mbili ziliwasilishwa na matawi mawili yanayoshindana kutokea chama cha Lavalas.

Kuna sababu nyingi zilizotolewa kuhusu kutoorodheshwa, kama hii kutoka radiokiskeya:

Wengi wa wagombea waliotemwa na Tume ya Muda ya Uchaguzi wanatuhumiwa kuhusika na vitendo vya uhalifu na biashara haramu ya mihadarati, ama na jumuiya ya kitaifa ya haki za binaadamu, au na Jeshi la Polisi la Haiti.

Katika blogu ya HaitiRectoVerso, Decky Lakyel anaripoti kuhusu maneno ya Frantz Verret, rais wa Baraza la Uchaguzi, kama alivyofafanua uamuzi wa kuwaacha wagombea wote wa chama cha Lavalas [Fr]:

‘Tuliangalia maombi kama yalivyowasilishwa na kila mgombea,’ aliongeza. Wagombea wa chama cha Fanmi Lavalas hawakuwasilisha hati zozote za ushahidi kutoka kwenye chama chao’, alifafanua bila ya kueleza matatizo mengine ya ndani ya chama hicho cha siasa cha Aristide.

Lakini ni katika sehemu ya mwisho ya makala ambako moja ya maelezo tata yanapatikana [Fr]:

Tumefuata sheria za uchaguzi na zile za katiba,’ anaapa Bwana Verret, ambaye anafikiri kuwa wahusika wanapaswa wajitahidi kuheshimu sheria za uchaguzi nchini Haiti. Vilevile, rais wa Baraza la Uchaguzi anasisistiza kuwa rais wa Haiti, [Rene Preval] hajapindisha uamuzi wa baraza hilo kwa namna yoyote.

Ukweli kwamba Verret anapinga kuwepo kwa mkono wa rais kwenye suala hili si jambo lilijitokeza tu, kwani wengi wanafikiri kuwa alifanya hivyo dhidi ya rais wa zamani wa nchi hiyo Jean-Bertrand Aristide.

Kuachwa kwa wagombea 40 (miongoni mwao wakiwemo wagombea 11 wa chama cha Lavalas) kumesababisha mijadala kadhaa – na yenye umuhimu – kama tunavyosoma kwenye mlolongo huu unaotoka kwenye Forum haiti [Fr/Creole]. Kwa mujibu wa radiokiskeya, ambaye amenukuliwa mara kadhaa, wote, Marekani na Kanada [Fr] wameonyesha kukerwa kwao kutokana na upendeleo uliofanywa wa kuwaacha wagombea kadhaa:

Balozi wa Marekani nchini Haiti, Janet Ann Sanderson […] anasisitiza ukweli kwamba katika mataifa ya kidemokrasia ‘uwazi na uchaguzi wa kidemokrasi ni mambo yanayojumisha na siyo kutenganisha’ na hulenga kwenye kuunga mkono ‘umoja wa kidemokrasia’ ambao unajumuisha vyama vyote vikuu vya kisiasa.

Pengine baada ya kuimarishwa na kuungwa mkono na watu wa nje, Chama cha Lavalas kimeamua kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa Tume ya Muda ya Uchaguzi, japokuwa tume hiyo imekwishatangaza kwamba uamuzi wake ni wa mwisho:

Msemaji wa Tume ya muda ya Uchaguzi, Frantz Bernadin, aliwaambia wanahabari siku ya Ijumaa [Januari 6] kwa kuwa baraza ndio mahakama ya mwisho ya rufaa, uamuzi wake kuhusu wagombea walioandikishwa hauwezi kukatiwa rufaa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.