HiviSasa, ni mradi wa kidigitali wa kukusanya na kuchapisha habari na picha kutoka kwa waandishi/watoa habari wa kiraia na kwa kila makala inayochapishwa katika tovuti ya mradi huo, mwandishi hulipwa hadi dola $85 kwa wiki. Malipo hayo hulipwa kupitia huduma ya M-Pesa, ambayo ni mfumo wa malipo malipo kupitia simu za kiganjani.
Kwa kila wiki, mradi huu huwatunukia waandishi zawadi za fedha taslimu ikiwa makala zao zimeweza kuvutia idadi kubwa ya wasomaji au kutembelewa zaidi na wasomaji wa kurasa zao.
Tovuti hii kwa sasa imeweza kufikia kaunti (Wilaya kwa Tanzania) zipatayo kumi nchini ambazo ni: Nakuru, Kiambu, Machakos, Kisii, Nyamira, Kisumu, Uasin Gishu, Garissa, Mombasa na Kibera.
HiviSasa inaelezea misingi yake kwenye tovuti yake kuwa ni:
Inapatikana kirahisi, inavutia watu wa makundi tofauti, ina uwazi na kumwezesha mwananchi na serikali ujumla. Wananchi wenye taarifa sahihi hufanya maamuzi bora na sahihi kwa ajili ya maisha yao na kwa serikali yao.
Usajili wa kujiunga ili uweze kuchangia katika tovuti hii hauchukui zaidi ya dakika moja na haiihitaji mtu kuwa mwandishi aliyesomea ili aweze kuiandikia HiviSasa:
Unaweza kuwa Mtaalam, Shirika binafsi, Mwanafunzi, Afisa wa Serikali, Mwanasiasa, mwananchi anayejali mwenendo wa mambo, Mchoraji wa vibonzo, Mfanyabiashara, mtazamaji…… n.k. Pia, waandishi wengi kitaaluma wamekuwa wakichangia katika tovuti hii hivyo kuongeza na kuukuza ujuzi wao na kuwaongezea wigo mpana na uzoefu wa masuala ya mtandaoni.
Andika habari yenye maneno 200 (au tuma picha mpya ikiwa na maelezo machache) ukijibu maswali yafuatayo: Ni tukio gani hilo? Limetokea wapi na lini? Ni nani mhusika au wahusika wa tukio hilo? Tukio hilo lilitokeaje? Kwa nini inastahili kupewa kipaumbele?
Wavuti hii imeonesha mifano mitatu ya habari nzuri za wenyeji kutoka kwa waandishi wapya. Moja kati ya habari hizo ni ile inayohusu mwanaume mmoja wa Kenya Lawrence Gekonge, aliyemzika mkewe jikoni baada ya kuaga dunia; kwa sababu, mkewe alipenda kutumia muda wake mwingi akiwa jikoni. Mwanaume huyo ameusia kuwa naye pia akiaga dunia angependa azikwe katika sebule ya nyumba yake kubwa.
Habari ya pili ni kuhusu mwandishi mzawa, Dickens Luvanda, aliyeweza kuandika kwa mfululizo na kwa bidii kubwa habari zipatazo 50 kwa wiki. Na habari ya tatu ilihusu hati miliki za ardhi zipatazo 1,200 zilizorundikwa na kuachwa bila kuchukuliwa na wenyewe katika ofisi za Usajili wa Ardhi huko Thika.
Mhariri Kiongozi wa mradi ndugu Enoch Nyariki aliiambia Global Voices kupitia mahojiano yaliyofanyika kwa njia ya email kuwa; tovuti hii imeshachapisha habari na makala zipatayo 61,000. Alisema kuwa moja kati ya kichocheo kikubwa walicho nacho katika mradi huu ni waandishi wa kiraia kuchangamkia fursa ya bure ya Chuo cha HiviSasa kilichoanzishwa kwa ajili ya kuwawezesha waandishi kuwa na ujuzi na msingi wa awali katika uandishi wa habari.
Video kutoka YouTube inayooneshwa hapo chini inaelezea kwa kifupi chuo cha Sheng, ambayo inatumia mchanganyiko wa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.
Chuo kinatoa masomo kadhaa bure kama vile Jinsi ya Kufanya Mahojiano, Jinsi ya Kuripoti Habari kutoka Mahakamani, Uandishi wa Kisheria- Wizi wa Maandishi, Uandishi wa Kisheria- Maandishi ya Kukashifu/Maandishi ya Kutweza, Makala za Chuki, n.k.
Mradi huu ulianzishwa kwa majaribio mwaka 2012 kwa hisani na ushirikiano wa 88mph, ambao iwaliwekeza kwa kuanzia na mradi ulizinduliwa rasmi Januari 2014. Wawekezaji wengine katika mradi huu ni pamoja na Omidyar Network na Novastar Ventures.