Rais Mzee Kuliko wote Duniani, Robert Mugabe wa Zimbabwe Atimiza Miaka 92

Zimbabwe's president Robert Mugabe turned 92 this month. Public Domain photo by the U.S. Air Force.

Rais wa Zimbabwe Robert Mugabe atimiza miaka 92 mwezi huu. Picha ya Wazi na U.S. Air Force.

Rais wa Zimbambwe Robert Mugabe, akifahamika kwa jina la utani ‘Anko Bob’, alitimiza miaka 92 tarehe 21 Februari mwaka huu. Yeye ndiye Rais aliyekula chumvi nyingi kuliko Marais wengine wote duniani , na amekuwa madarakani tangu mwaka 1987. Muda wake wa kutumikia nyadhifa za juu serikalini haukomei tu kwenye miaka 30 akiwa kama Rais. Aliwahi pia kuwa waziri mkuu wa Zimbabwe kati ya mwaka 1980 na 1987.

Kwa mujibu wa mashirika ya kutetea haki za binadamu ya Amnesty International na Human Rights Watch, Serikali ya Mugabe mara kwa mara imekuwa ikiwatendea isivyo wapinzani na wafuasi wao, waandishi wa habari, mashirika ya kiraia pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu.

Taarifa ya kimataifa ya shirika la Human Rights Watch ya mwaka 2015 ilibainisha kuwa , “Serikali ya Rais Robert Mugabe ilibobea katika kukiuka haki za binadamu katika kipindi cha mwaka 2014 bila kujali kifungu cha sheria kwenye katiba mpya ya Zimbabwe kinacholinda haki za raia. Serikali ya Mugabe haijawahi kusimamia utekelezaji wa kisheria uliotarajiwa sambamba na sheria mpya au zilizoboreshwa kwa minajili ya kusimamia haki za binadamu kulingana na matakwa ya katiba.”

Kadhalika, Mugabe analaumiwa na wapinzani wa nchi hiyo pamoja na Jamii za Kimataifa kwa mwendelezo wa Udanganyifu wa Kimfumo wakati wa Chaguzi za Kisiasa.

Kwenye mitandao ya kijamii, watumiaji wa Twitter wamekuwa wakisambaza taarifa na nukuu za Mhe Mugabe anayeulikana sana kwa uwezo wa kuzungumza, hasira, vichekesho, chuki dhidi ya wapenzi wa jinsia moja na utamaduni wa ki-Magaharibi.

“Nimeshafariki mara nyingi sana. Na kwa kweli, nimemshinda hata Yesu Kristo kwa kuwa yeye alikufa mara moja tu.” Robert Mugabe. Heri ya siku ya kuzaliwa mjomba

Mugabe alitoa kauli hii wakati wa sherehe yake ya kukumbuka miaka 88 ya kuzaliwa, kufuatia kuzushiwa kifo mara kwa mara.

“Hatukuwafukuza wazungu, tulichokifanya ni kuchukua ardhi yetu” Rais Robert Mugabe

Mugabe aliwafukuza wakulima wazungu raia wa Zimbabwe waliokuwa wakihodhi ardhi nchini humo mwaka 2000 ikiwa ni mpango wake wa mageuzi ya ardhi na utoaji fursa kwa raia weusi. Jumla ya  wakulima wazungu 4,000 walipoteza mashamba yao.

Nitaendelea kutawala hadi pale Mungu mwenyewe atakaponiita -alisema Rais Robert Mugabe kwenye maadhimisho ya 92 ya siku ya kuzaliwa kwake

Mugabe hakukosa cha kusema kujibu kauli ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon ya kuwataka Marais wa Afrika kuacha kung'ang'ania madaraka.

“Nitakuoa wewe kwanza kisha niruhusu mahusiano ya kishoga nchini mwangu.” Robert Mugabe alipomjibu Barak Obama.

Imetaarifiwa kuwa, Mugabe alitoa kauli hii kufuatia Rais wa Marekani Barack Obama kuwataka viongozi Afrika kutoa haki sawa kwa wanaume na wanawake wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja. Mwaka 2011, Mugabe aliwaelezea watu wanaoshiriki mapenzi ya jinsia moja kuwa ni “wa hovyo kuliko hata mbwa na nguruwe.”

‘Nchini kwetu Mzungu ni raia daraja la pili. Mzungu pekee unayeweza kumwamini ni yule aliyekwisha fariki.’ ~Robert Mugabe

Vyanzo vingi vya mtandaoni ikiwa ni pamoja na Makala ya 2015 iliyoandikwa na Meya wa London Boris Johnson, vinamuhusisha Rais Mugabe na msemo huu.

“Kimsingi makao makuu ya Umoja wa Mataifa yamehamishwa” 😂😂 Robert Mugabe leo ametimiza miaka 92!

Akiongea kwenye mkutano wa kila mwaka wa Umoja wa Afrika huko Addis Ababa, Ethiopia, mwezi uliopita, Mugabe alisema makao makuu ya Umoja wa Mataifa uliopo New York yalipaswa yajengwe kwenye nchi zilizo na idadi kubwa zaidi ya watu kama vile China, India au barani Afrika.

“Kwa hiyo Blair, ilinde nchi yako Uingereza na mimi niache niilinde nchi yangu Zimbabwe”. – Robert Mugabe

Mugabe alisema hayo kwenye Mkutano wa Dunia pale alipojibu ukosoaji wa kiongozi huyo wa zamani wa Uingereza kuhusu mpango wa Mugabe wa utaifishaji ardhi.

“Afrika ianzishe mahakama yake ya Kimataifa ya Makosa ya Kihalifu na kisha iitumie kuwashitaki wazungu” -Robert Mugabe

Akiongea na waandishi wa habari kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Harare, Mugabe alisema , ” Viongozi wa nchi za Magharibi walifanya makosa ya kihalifu, makosa yaliyokithiri wakati wa ukoloni- kuchinjwa kwa watu wetu wetu pamoja na kufungwa gerezani… ninalo shitaka moja dhidi yao, kwa nini nilifungwa jela miaka 11? Tumewasamehe, lakini pengine hatujajitendea haki… Mliunda ICC [Mahakama ya Kimataifa ya makosa ya Uhalifu], nasi hatuna budi kuanzisha mahakama yetu ya kuwashitaki wazungu, kuwashitaki akina [George] Bush na [Tony] Blair.”

Ukweli unaofurahisha: Kipindi Robert Mugabe alipozaliwa, Milki ya Khalifa ya Uturuki bado ilikuwepo. Pia, amekuwa madarakani kwa miaka 6 zaidi ya miaka aliyoishi Steve Biko.

Milki ya Kahalifa ya Uturuki ilikuwa ndio Milki ya Khalifa ya mwisho ya Kiislam ya dhehebu la Sunni ya kipindi cha mwisho za zama za kati na kipindi cha mapema cha zama mpya. Bunge la Uturuki lilikomesha milki ya Khalifa ya Uturuki mnamo tarehe 3 Machi, 1924. Steve Biko alikuwa ni mwanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika ya Kusini ambaye alifariki mwaka 1977 akiwa na umri wa miaka 30.

Robert Mugabe ndiye Rais aliyesoma zaidi kuliko Marais wengine wote duniani. Hakuna Rais mwingine aliye na idadi kubwa ya shahada za vyuo vikuu kama yeye.

Mugabe ana shahada saba. Alihitimu shahada ya sanaa katika chuo kikuu cha Fort Hare, Afrika Kusini kabla ya kuhitimu tena shahada nne na shahada mbili za umahiri kwa njia ya elimu kwa masafa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.