Kwa siku mbili, mamlaka husika hazikuweza kujitokeza kwa ajili ya kutoa msaada. Hatimaye, siku ya Alhamisi, Septemba 24, wapangaji kadhaa waliamua kuchukua hatua kwa kuyaondoa matofali na kisha kumtoa mbwa huyo na ambaye aligundulika kuwa alikuwa na mimba. Picha za uokozi kwa haraka zilipata umaarufu katika mitandao ya kijamii, ambapo kwa chini ya masaa 48, zilikwisha kutazamwa na watu zaidi ya 77,000.
Jumuia ya wazawa ya kutetea haki za wanyama inayofahamika kama “Right to Life (Haki ya Maisha”)” imechukua jukumu la kumhifadhi mbwa huyo kwa muda, na pia kuanzisha kampeni ya kumpatia mbwa huyo makazi yake mapya. Kwa bahati mbaya watoto wa mbwa huyo(aliyepewa jina la Belka, au “Kichakoro/Kuchakoro”) walipoteza maisha kutokana na msongo pamoja na kupoteza maji mengi baada ya kunaswa ardhini. Kwa sasa, mbwa huyo yupo kwenye kliniki kwa ajili ya ungalizi wa karibu, ambapo wataalamu wa mifugo walifanya utabibu wa mionzi na kumhasi.