Wiki yote hii jijini Washington, DC, Taasisi ya Transformational Media itafanya mkutano unaowaleta pamoja “waleta mabadiliko, waandishi na wataalam wa vyombo vya habari” kutoka duniani kote “kushirikana kwa nia njema”. Mkutano huo wa TM ni mkutano wa mwaka wa mara ya pili, utakaoendelea kuanzia Oktoba 26 mpaka Novemba 2, 2014. Wiki hiii, matukio yatakayoenda sambamba na mkutano huo yatafanyika jijini humo, na kuhitimishwa na na shamra shamra nyingi ikiwa ni pamoja na Mfuko wa Umoja wa Mataifa, Oktoba 31, na siku ya mkutano wenyewe itafanyika kwenye Chuo Kikuu cha George Washington Novemba 1.
Washiriki wa mkutano huo watajadili uandishi, ubunifu, teknolojia mpya, biashara na maisha endelevu, upigaji picha, filamu na muziki, uandishi wa habari pamoja na masuala mengine mengi. Kwa mujibu wa waandaaji wa mkutano huo:
Mkutano wa TM utajikita kwenye namna habari na uandishi wa habari unavyoweza kuleta mabadiliko chanya kwa kubadili mitazamo, kuleta ufumbuzi wa kiteknolojia, kukuza uelewa, kuhamasisha uwajibikaji, na zaidi kusambaza furaha. Unaleta pamoja wataalam wakubwa kwenye maeneo yao wanaotoka kwenye mashirika mbalimbali kama vile: UN Foundation, Discovery Channel, MTV, na Taasisi ya Jane Goodall.
Global Voices ilizungumza na Jeremy Wickremer, anayeongoza Mkutano huo, kujua machache kuhusiana na mkutano huo. “Suala kuu ni kujenga dunia iliyo bora zaidi,” anasema. “Ni masuala ambayo kimsingi yanahusiana kwa karibu: usawa, umiliki, mazingira, afya na ustawi—yote yanahusiana. Huwezi kushughulikia suala moja likiwa pekee,” anatahadharisha.
Taasisi ya Transformational Media inalenga kuvutia hadhira kubwa kadri inavyowezekana katika mkutano wa mwaka huu jijini Washington. Wickremer anatarajia makundi mbalimbali kushiriki, kuanzia wanafunzi wa sekondari hadi wasanii na mameneja waandamizi. “Hatua ya kuyaita makundi mengi zaidi, ni katika kuliona jambo hili kwa mtazamo mpana zaidi.”
Lengo kuu mojawapo la mkutano huo ni kuwaleta watu ambao vinginevyo wasingekutana, ili kukuza uelewa mpya na kujenga mitandao inayoleta ushirikiano “ili kukuza matokeo ya kijamii yanayoletwa na watu hawa.”
Wasomaji wanaotamani kujua zaidi kuhusu mkutano wa TM na Taasisi ya Transformational Media wanaweza kutembelea tovuti ya mkutano huo na tovuti ya taasisi hiyo, ukurasa wa Facebook, naanuani ya Twita.