Kinachotokea Pale Baba na Mama Wanapokaribia Kufukuzwa Nchini Marekani

“ Ninaelewa ni jinsi gani ilivyo vigumu kuwatunza watoto wadogo,” ndivyo anavyosema kijana wa miaka 19 Luis Duarte, wapili kulia, ambaye anawalea wadogo zake watatu baada ya wazazi wao ambao kwa asili wanatokea Mexico, kuswekwa ndani na mamlaka za uhamiaji za Marekani mwezi Mei mwishoni. Shukrani kwa: Deepa Ferndandes

Habari hii iliyoandikwa na Deepa Fernandes mwanzo ilichapishwa kwenye PRI.org Juni 11, 2017. Imechapishwa tena kama sehemu ya ushirika baina ya PRI na Global Voices.

Kwa jinsi Francisco Duarte 19 alivyoshuhudia wazazi wake wakivalishwa pingu na kuchukuliwa na maafisa wa uhamiaji mwishoni mwa mwezi Mei nje ya nyumba yao huko San Diego, California, kitu pekee alichoweza kufanya ni kuwabembeleza kwa lengo la kuwatuliza wadogo zake mapacha wa kike wenye miaka 12 waliokuwa wamefadhaika.

Kisha aliondoka kwenda kutafuta msaada kwa ajili ya wazazi wake. Katika hali hiyo ni dhahiri wangehitaji mwanasheria wa masuala ya uhamiaji na Fransisco angehitajika kukusanya nyaraka zao.

Mdogo wake wa kiume Luis, 17, alijitolea kuwaangalia wadogo zao, na aliwapikia mayai waliporudi kutoka shuleni siku hiyo.

Kaka hao walitingwa na kupangilia shughuli zote za nyumbani huku wakihakikisha wanawatunza wadogo zao wa kike.

Kisha pigo likawakuta kaka hao. Kodi ya nyumba inaisha ndani ya muda usiozidi juma moja. Pia walikuwa wanatakiwa kulipa bili zote ndani ya familia. Duarte anasema yeye na kaka yake walikusanya fedha yote waliyokuwa nayo wazazi wao. Walipata kiasi cha dola 2,500.

Walihitajika kuongezea kipato cha baba yao kwa namna yoyote. Ndiye aliyekuwa anatafuta mkate wa familia kwa kuendesha biashara ya kuuza barafu. “Mama yangu na baba walikutana wakiuza barafu kwenye vitoroli miaka 20 iliyopita walipokuja nchi hii” alisema Duarte.

Wakati Francisco na Luis walikuwa wakiendesha vitoroli vyao binafsi vya barafu kusaidia familia, hawakuweza kuingiza kipato alichokuwa anaingiza baba yao, alisema Duarte.

Francisco Duarte Sr. na mkewe Rosenda Perez, walikamatwa na maafisa wa uhamiaji Mei 23. Duarte alikuwa ameondoka nyumbani kwake National City, California, kwenda kununua gazeti mtaani. Mke wake alitoka kuja kuangalia ni kitu gani kinaendelea ndipo naye alikamatwa pia. Maafisa wanasema wanatuhumiwa kwa “kukiuka taratibu za uhamiaji” ndani ya Marekani. Hakuna tuhuma za jinai wala rekodi za uhalifu dhidi yao.

Wanandoa hawa wa San Diego ni kati ya idadi kubwa ya watu wasio raia wanaokamatwa kwa makosa ya uhamiaji katika miezi ya mwanzo ya utawala wa Donald Trump. Kuanzia Januari 22 mpaka Aprili 29, zaidi ya watu 41,000 wanashukiwa kuishi nchini Marekani bila vibali halali vya uhamiaji wamekamatwa na maafisa usalama, hili ni ongezeko la karibu asilimia 40 ulikilinganisha na kipindi hicho hicho kwa 2016, na hii ni kulingana na maafisa wa Marekani.

Robo ya waliokamatwa wanashitakiwa kwa makosa ya kutokuwa nchini Marekani kihalali, lakini hawana rekodi za makosa ya jinai ya hapo kabla. Ni kundi ambalo halikulengwa sana na utawala wa Barack Obama. Idadi ya hivi karibuni inaonesha Trump anafanya vyema katika ahadi yake ya wakati wa kampeni ya kubadilisha hilo, kama ilivyoelezwa hivi karibuni na mwanahabari Sacchetti kwenye The Washington Post.

Kabla ya kukamatwa kwake, Duarte alikuwa amekamilisha kuwaweka wanae wadogo chini ya uangalizi wa kijana wake mkubwa Luis.

Kwa watoto, hiki kimekuwa kimbunga kwao. Jumanne ya hivi karibuni, Fransisco aliomba msaada wa jamii kuandika barua za kuwaunga mkono wazazi wao.

Alirudi nyumbani mwenye njaa. ” Nilikuwa nimetoka tangu asubuhi”, alisema Luis. “Tumechoka, tumejitahidi kufanya tulichoweza kwa wazazi wetu, hivyo ndiyo, napata kiamsha kinywa saa 8.37 mchana.

Mark Lane, msaidizi wa kisheria katika ofisi za wanasheria wa masuala ya Uhamiaji LA aliketi na Fransisco, na walijadili ni kitu gani zaidi wanapaswa kukusanya kwa ajili ya kesi ya wazazi wake. Lane ni mmoja wa watu walioitwa na Fransisco kutoa msaada siku wazazi wake walipokamatwa.
“Kabla ya utawala wa Trump labda nilikuwa napokea simu mbili au tatu kwa juma, sasa napokea mpaka simu 10 au 15 kwa siku, alisema Lane. ” Watu wanahofu sana, familia zimetawanyika.”

Lane, ambaye ofisi yake imechukua kesi ya wazazi wa Fransisco, aliongea na watoto kuhusu gharama wanazopaswa kulipa. Watoto wote wanne wako shuleni, wakipata muda kidogo wa kufanya kazi ili kuleta kipato kwa familia. Hivyo waliamua kugeukia uwanja wanaoufahamu vyema: mitandao ya kijamii.

Walitengeneza video fupi kuhusu suala lao na kuiweka YouTube, na kuiunganisha na tovuti ya GoFundMe inayochangisha fedha. Waliweka lengo la kukusanya fedha kiasi cha dola 70,000 na, siku chache baadae walishangaa kuvuka lengo. Michango zaidi ya dola 72,000 ilipatikana.

Wameshangazwa na wanashukuru.

Lakini sio pesa pekee ziliingia kwao, pia watu walituma jumbe wakiwaambia wako pamoja nao.

“Inatia moyo sana kuona kila siku napokea jumbe toka kwa watu wakiniambia wako pamoja nasi na kama kuna lolote tunalohitaji tupige simu au kutuma ujumbe mfupi wa maneno, “alisema Fransisco”

Fransisco mkubwa aliona vigumu sana kukubaliana na kampeni ya mitandaoni watoto wake wanayoifanya kwa niaba yake, kijana wake alisena. Katika mazungumzo ya hivi karibu kwa njia ya simu Fransisco mdogo alimuelewesha baba yake jinsi fedha na misaada inavyomiminika kwao.

Baba yake aliuliza ni nani hasa anayesaidia, “watu wengi” alijibu kijana wake. Waalimu, majirani, marafiki, watu wa sehemu mbalimbali hapa mjini,” alimwambia baba yake wakati wa mazungumzo yao kwenye simu.

Taarifa zilivyoenea mitandaoni, marafiki walianza kufika nyumbani kutoa msaada. Kundi la marafiki wa Luis kutoka shuleni wanasaidia. Luz Maria Castañon alisema hawataki Luis apate tabu akiwa shuleni.

“Anaenda kuwa mwanafunzi mwenye ufaulu wa juu kwa kweli. [Hakuna] cha kufananishwa na GPA yake.”

Huko jikoni, rafiki mwingine, Maria de Jesus, anapika tacos. Alisema ataendelea kuwapikia watoto mpaka wazazi warudi nyumbani.

Wadada mapacha, Aracely and Yarely, waliangalia wazazi wao wakivalishwa pingu na kuchukuliwa na maafisa wa uhamiaji. Ilinichanganya, alisema Aracely, na wanawakumbuka sana wazazi wao. Hasa wanapotoka shuleni.

“Kwa kawaida mama angekuwa hapa na angetuandalia vitafunwa kidogo wakati mwingine,” alisema Yarely.

Wasichana hao sio mapacha wanaofanana, ila wote wana tabasamu tamu, linalohuzunisha namna fulani. Hujishughulisha na kupanga vitu chumbani mwao.

“Wakati mwingine hii ni balaa lakini , um, …” Yarely aliondoka

Luis huwaangalia dada zake kuhakikisha wako sawa, na kisha huondoka. ” Ninaenda kufua nguo kwa sababu shuka zetu ni chafu sana,” alisema.

Je ni kazi yake ya kawaida?

“Hapana, kwa kweli.”

Baada ya kufua, anatakiwa awepo nyumbani kwa ajili ya dada zake. Kaka yake ataendelea kukusanya barua kwa ajili ya kuwaunga mkono wazazi wao.

“Sasa ninaelewa ni kiasi gani ilivyo vigumu kuwalea watoto wadogo,” alisema Luis.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.