Ifuatayo ni makala ya ubia iliyoandikwa na na kuchapishwa kwa mara ya kwanza kwenye tovuti ya OC Media.
Mnamo Machi 22, huko Tbilisi, mama na mtoto wake wa kike wakiwa wamesimama pembezoni mwa barabara waligongwa na gari. Msichana huyu wa miaka 11 alifariki papo hapo na mama yake alikimbizwa hospitali akiwa katika hali mbaya sana.
Mamlaka ya Polisi imeanzisha utaratibu wa uchunguzi dhidi ya ‘ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani hali inayopelekea watu kupoteza maisha’, makosa ambayo adhabu yake ni kati ya kifungo cha miaka minne hadi saba gerezani.
Kwa mujibu wa mashuhuda, mama na mtoto wake walikuwa wamesimama kwenye kituo cha mabasi, na ndipo gari liliacha njia na kugonga kwanza mlingoti wa matangazo na kisha kuwagonga wao.
Mwaka 2015, Shirika la Afya Duniani lilichapisha taarifa iliyoeleza kuwa, kwa kila mwaka watu milioni 1.25 wanapoteza maisha kutokana na ajali za magari. Kwa mujibu wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD), Georgia ilikuwa ndio nchi ya Ulaya iliyokuwa na kiwango kikubwa cha vifo vinavyotokana na ajali za barabarani(163.6 kwa kila wakazi milioni 1). Asilimia 24 ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani nchini Georgia ni vya waenda kwa miguu.
Kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani ya nchini Georgia, (tazama hapa chini), idadi ya ajali ilianza kupungua mwaka 2008, pamoja na kuwa imekuwa ikiendelea tena kupanda tangu mwaka 2011. Wizara ilisema kuwa, mambo makuu yanayosababisha kutokea kwa ajali ni ulevi na mwendo mkali.
Mwaka 2011, ajali 4,500 za barabarani ziliripotiwa nchini Georgia, ambapo ajali 6,000 hazikuwa na mandara makubwa wakati ajali 500 zikiwaacha watu katika hali mbaya sana. Mwaka 2016, takribani ajali 7,000 za barabarani ziliripotiwa, ambapo ajali 10,000 zikiwa si za madhara makubwa na ajali 600 zikiwaacha watu katika hali mbaya.
Adhabu Kidogo Dhidi ya Ukiukwaji wa Sheria za Barabarani
Pamoja na ongezeko la idadi ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani, mwaka 2014 Wizara ya Mambo ya Ndani iliandaa marekebisho ya sheria ya usimamizi iliyopunguza adhabu ya ukiukwaji wa sheria za usalama barabarani. Kwa mujibu wa mswada wa sheria uliopendekezwa, kosa la kukatisha mstari wa katikati itakuwa ni nusu ya tozo ya sasa ambayo ni lari 100($41). Tozo ya makosa ya kujirudia itabadilika kutoka lari 200 ($82) hadi lari 100 ($41). Waliokutwa na makosa ambao hawatoi tozo zao kwa wakati kwa sasa watapaswa kulipa lari 40 ($16) badala ya kiwango cha sasa cha lari 150 ($61).
Mwaka 2016, Seriali ya Georgia ilipitisha Mkakati wa Kitaifa wa Usalama Barabarani. Waandishi waliweka bayana kuwa, mkakati huu umekuja katika wakati muafaka kufuatia ongezeko la idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na ajali za barabarani. Mkakati huu utakaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitano, umekubaliwa kwa pamoja na wizara za Uchumi, Maendeleo ya Kikanda, Kazi na Mambo ya Jamii, Elimu na Sayansi pamoja na Mamlaka ya Jiji la Tbilisi.
Mkakati huu, pamoja na mambo mengine unalenga kuhakikisha usalama wa usafiri wa wanafunzi, huduma za haraka za kimatibabu pamoja na utoaji wa elimu mashuleni kuhusiana na usalama barabarani.
Ili kutimiza malengo ya mradi huu, tume kutoka mamlaka mbalimbali na kikundi maalum viliundwa na Wizara ya Uchumi kwa lengo la kuratibu mradi katika taasisi mbalimbali.
Kwenye ufafanuzi, Waziri Mkuu Giorgi Kvirikashvili alisema kuwa mpango huu umekuja kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na mashirika ya Kimataifa pamoja na wataalam.
‘Taarifa hii ni ya muhimu sana kwa ajili ya kutafuta suluhu ya kudumu na ya mafanikio ya usalama barabarani nchini Georgia’, alisema Rais.
Kwenye mazungumzo na RFE/RL, Gela Kvashilava, mwanzilishi wa Shirika Usalama Barabarani, kampuni ya utetezi ya wazawa, alisema kwamba tatizo la Georgia kuhusu usalama barabarani ni kuwa barabara zilijengwa kwa dhumuni la kupitisha magari badala ya watu.
Mkakati huu wa miaka mitano unalenga kushughulikia masuala kama vile usalama barabarani, msongamano wa magari jijini pamoja na kukosekana kwa maeneo ya maegesho ya magari.