Befeqadu Hailu, Abel Wabela, Atnaf Berahane, Mahlet Fantahun, Zelalem Kibret, na Natnael Feleke (wote wakiwa n wanachama wa mkusanyiko wa wanablogu wa Zone 9) na waandishi wa habari Asmamaw Hailegeorgis, Tesfalem Waldyes pamoja na Edom Kassaye walikamatwa mnamo Aprili 25 na 26, 2014 jijini Addis Ababa. Tangu wakati huo, wamewekwa kizuizini kwenye mahabusu ya Maekelawi huku wakinyimwa haki ya kuonana na wanasheria. Vile vile hawaruhusiwi kuonana kabisa na familia zao.
Tangu mwaka 2012, wanablogu hao wa Zone 9 wamekuwa wakifanya kazi kubwa ya kuwezesha ushirikishwaji wa kiraia pamoja na uchambuzi wa kina kuhusu masuala ya kijamii na kisiasa nchini Ethiopia, wakifanya kazi sambamba na waandishi (ambao nao wamekamatwa) waliokuwa karibu nao ili kufikisha harakati hizo kwenye magazeti. Kukamatwa kwao kimsingi ni uvunjwaji wa haki za kimataifa zinazomlinda raia kujieleza, na haki yao ya kutokuteswa wakiwa chini ya ulinzi, kama Ibara ya 6 ya Makubaliano ya Afrika inavyotamka kuhusiana na masuala ya Haki za Binadamu na Makundi ya watu.
Jumuiya ya Global Voices na mtandao wetu wa marafiki na washirika tunadai kuachiliwa kwa ndugu zetu hao ambao idadi yao ni tisa.