Hsieh-Li Wang alionyesha jinsi [zh] Sheria ya sasa inavyoyaruhusu makampuni ya ujenzi kuendelea na mipango ya ufufuaji miji hata pale ambapo wakazi wengi hawataki kujiunga kwenye mradi huo:
Nyumba ya akina Wang kabla ya kubomolewa. Picha na mtumiaji wa Flickr anayeitwa munch999 (CC BY-NC-SA 2.0).
Mtego wa Sheria hiyo uko hapa: kwa mujibu wa Kifungu cha 10 mstari wa pili ‘Pale ambapo walau asilimia 10 ya wenye nyumba ambao kwa pamoja wanamiliki zaidi ya asilimia 10 ya ardhi wanapokubali kujiunga na mradi, basi hao wanaweza kuomba kujiunga na mradi wa ufufuaji miji.’ Je, kifungu hiki kina maana gani? Chao-Wen Lee, ambaye ni mmoja wa wahanga wa mradi wa ufufuaji miji huko Wufenpu, alisema, ‘hiyo ina maana kwamba kikundi cha watu fulani matajiri au kampuni ya ujenzi inapotaka kutekeleza mpango wa kufufua mji, wanaweza kununua baadhi ya nyumba katika eneo hilo na kuwaweka watu wengi kuwa wamiliki wenza; watu hawa wanapokuwa ndiyo wengi miongoni mwa wamiliki, basi hapo hakuna namna ya kuzuia mpango wa kufufua miji kutekelezwa.’ Mathalani, katika jamii ya Chao-Wen Lee, zaidi ya asilimia 70 ya wakazi waliandikishwa kama wamiliki wa baadhi tu ya nyumba.
Kwa kutumia Kifungu cha 25 cha Sheria ya Ufufuaji Miji, serikali inaruhusiwa kupitisha mradi wa ufufuaji miji pale asilmia 80 ya wakazi waliohusishwa wanapokubali kujiunga na mradi [zh]. Kwa wale watakaopinga kujiunga na mradi, wataadhibiwa kwa kufukuzwa kwa nguvu na serikali. Yo-Yu Hsih, anayesomea sheria aliikosoa sheria hiyo [zh] akisema inasababisha uzandiki wa watu walio wengi kukiuka haki za wachache.
Lengo la mwanzo la uamuzi wa wengi lilikuwa kutumia rasilimali ya ardhi, iliyo haba, kwa ufanisi zaidi. Ililenga pia kuzuia vitendo vinavyoweza kuashiria kupokwa kwa haki ya walio wengi na watu wachache ambao wanataka kuzuina kuendelezwa kwa ufufuaji miji na majiji.
(Hata hivyo) Uamuzi wa wengi unaweza kusababisha uzandiki unaosababisha maslahi ya wachache kupotea … Hivi sasa, Kifungu cha 22, mstari wa 1 wa Sheria ya Ufufuaji Miji kinapitisha uamuzi wa wengi pasipo kutoa kinga yoyote kwa wale walio wachache. Jambo hili litawaweka walio wachache katika hali ya kuonewa huku haki zao zikitishiwa. Ninasikitika kusema kwamba Sheria hii imekiuka kanuni za sheria za kuingilia haki za wengine.
A poster outside Wang's houses. It says ‘my house was bought when I was 40, and it was torn down when I was 70.’ Photo by Flickr User munch999 (CC BY-NC-SA 2.0).
Kuhusika kwa Serikali
Hsieh-Li Wang alihoji [zh] kwa nini Sheria iliruhusu serikali kuwatumia polisi ili kulinda maslahi ya wawekezaji:
Kifungu cha 36 cha Sheria ndiyo chenye utata zaidi: kampuni ya ujenzi inaweza kukata rufaa kwa serikali ili iweze kuvunja nyumba kwa nguvu pale wakazi wake wanapokataa kuondolewa. Wataalamu wengi wanaamini kwamba Sheria, ambayo inahalalisha matumizi ya njia ya uamuzi wa wengi na ushiriki wa serikali katika kuwaunga mkono wawekezaji, imekiuka kinga inayotolewa na Katiba kuhusiana haki za mali za raia.
Chama cha Haki za Binadamu cha Taiwan kilidai ufanyike upitiaji wa kina wa Sheria ya Ufufuaji Miji kwa mujibu wa Katiba. Katika Chombo cha Kutunga Sheria cha Yuan, mbunge Mei-Nyu You alijenga hoja [zh] kwamba Waziri wa Mambo ya Ndani afanyie marekebisho Sheria ya sasa ya Ufufuaji Miji:
Leo hii, kama umempangisha nyumba yako mtu ambaye anagoma kuhama, unaweza kukata rufaa kwa mamlaka ili kumhamisha mpangaji huyo? v…Unahitajika kumfungulia mashtaka mpangaji huyu. Kama ukishinda kesi, basi unaweza kuomba amri ya mahakama itumike kumhamisha. Kwa kawaida, mahakama itampa mpangaji muda maalumu wa kuhama, na hivi ndivyo Katiba yetu inavyotoa kinga kwa haki za ukaazi.
Leo hii nyumba yangu iko katika hali nzuri na wala haizibi nyumba za majirani, barabara au kuhatarisha usalama wa raia. Lakini, mara tu mwekezaji akiitamani ardhi yangu na jinsi inavyoweza kumpa nafasi, anaweza kabisa kuniondoa mimi kutoka kwenye nyumba yangu (pasipo ridhaa yangu). Mwekezaji huyo anaweza hata kuizunguka mahakama kwa kwenda kukata rufani kwa mamlaka za utawala na kupata nguvu ya kuja kubomoa nyumba yangu. Je, hapa kweli kuna haki kwa mujibu wa Katiba?
Sura ya pili ya Katiba yetu inafafanua haki na wajibu wa wa raia, ambazo kwa kiasi kikubwa zimegeuzwa kuwa ngebe kupitia kampeni mbalimbali za kisiasa … Jamii yetu iko kama inayounga mkono uongo unaotolewa na wanasiasa kwa muda mrefu sasa kupita kiasi. Walitueleza kwamba tunaweza, hatimaye, kufurahia haki zote zinazotajwa kwenye Sura ya Pili ya Katiba yetu, yaani baada ya wao [kushinda uchaguzi na] kushika madaraka ya urais kwa mujibu wa Sura ya Nne ya Katiba yetu na baada ya kupata viti vingi kwenye Bunge kwa mujibu wa Sura ya Sita ya Katiba yetu. Lakini, daima huwa wanaibuka na visingizio kibao ili kutotimiza ahadi zao.
Hii ndiyo sababu tunadai yafanyike mabadiliko ya Sheria hii ya Ufufuaji Miji isiyo ya haki, maana tunataka kulinda haki za kila raia kuwa na makazi. Hatuna budi kuhakikisha kwamba tunaifanya Katiba yetu ifanye kazi inavyostahili, isichafuliwe na uongo wote huo wanaotoa kila mara, ili tupate kuandika upya historia ya watu wa Taiwan.