- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

‘Mnao uwezo mkubwa na kuzidi’

Mada za Habari: Nchi za Caribiani, Trinidad na Tobago, Elimu, Uandishi wa Habari za Kiraia, Vijana, The Bridge
[1]

Madawati ya darasani; picha kwenye mtandao wa [1] Flickr [2] na Jack Sem [3], CC BY 2.0 [4].

Maoni ya Mhariri: Mnamo Septemba 9, wanafunzi nchini kote Trinidad na Tobago ambao hivi majuzi walifanya mtihani wa Tathmini ya Kuingia Sekondari (SEA)—jaribio muhimu na gumu linaloamua hatma ya wanafunzi hao kwa maana ya aina ya shule ya sekondari watakayochaguliwa kwenda—walipata matokeo yao. Wastani wa wanafunzi 19,645 [5] walifanya mtihani huo wa 2021, lakini kwa sababu nafasi kwenye shule “maarufu” zilikuwa chache, ushindani ulikuwa mkali. Zaidi ya hayo, kwa kuwa nyingi ya shule hizi zinaendeshwa na bodi za kidini, kuna makubaliano—yanayofahamika kama the Concordat [6]—yanazipa shule hizo uwezo wa kuchukua asimilia 20 ya wanafunzi wapya wanaojiunga na shule zao, bila kuangalia ufaulu wao.

Mfumo [wa elimu nchini Trinidad na Tobago] umekuwa ukilaumiwa kwa kuwabagua watoto [7] na kuwanyima fursa ya kukuza ubunifu katika kujifunza. Mwandishi Shivanee Ramlochan, aliyewahi kupambana na mfumo wa elimu nchini humo, aliandika [8] maoni yake kuhusu mtihani huo [wa kuingia sekondari] kupitia ukurasa wake wa Facebook. Ameturuhusu kuchapisha tena maoni hayo, kama yanavyoonekana hapa chini:

Nilikuwa mtoto asiyeambilika kirahisi.

Ingawa nilikuwa uwezo na haiba yangu iliendana na masomo ya lugha, nikiwa shule ya msingi na sekondari mambo mengi yalinichanganya na kukwamisha mafanikio yangu. Hali hii ilichangiwa na mfumo uliotawaliwa  na mbinu zinazoumiza na kufedhehesha ambazo walimu wangu wengi na uongozi wa shule walizitumia. Nilikuwa, kwa asili, kijana mtundu na labda mwenye kiburi, lakini haikuwa kwangu tu, kibaya zaidi ninachokikumbuka ni walimu—wakubwa, wenye hekima na wenye uzoefu—kuninyanyasa nikajiona sina maana kwa machozi.

Tafsiri ya haya yote ni hii: mbinu zilizotumika kunifundisha zilichangia kuzima ndoto kadhaa mwilini na akili mwangu kabla hata hazijamea. Silengi kuonesha “makosa” hapa; kinyume chake, ninachotaka kukisema ni kwamba kuzimwa kwa  ndoto nilizokuwa nazo wakati huo, kumeniongezea nguvu ya kuwekeza kwenye ndoto hizo vizuri zaidi sasa hivi. Bado, hata hivyo, imekuwa utamaduni wangu kila matokeo ya mtihani wa kuingia sekondari yanapotoka, najikuta siwezi kunyamaza kuzungumzia matarajio makubwa tuliyonayo kwa watoto yanayoenda sambamba na mbinu za upimaji zinazoumiza na kufedhehesha watoto wa taifa hili.

Magazeti leo yatapambwa na habari za “wanafunzi bora zaidi,” wasichana na wavulana waliovalia miwani wenye nyuso zinazotabasamu wakiwa wameshika matokeo yao, wakiambatana na wazazi wao wawili,  ambayo kwa hakika ni taswira ya neema katika familia. Waliofaulu zaidi wataongelea namna walivyoteseka kukesha usiku kucha wakisoma vitabu, watazungumzia umuhimu wa kumtanguliza Mungu, watazungumzia namna walivyotumia muda mwingi kukariri kanuni na milinganyo hata wakiwa uwanjani wakicheza. Watoto hawa watasifiwa, na sikusudii kuwafanya wasione fahari kwa chochote hatika ya hayo.

Wapo watoto wengi zaidi leo wanaojisikia kuumizwa, wakishikilia karatasi inayowatangazia kwamba hawakufanikiwa kuchaguliwa kwa chaguo la kwanza, la pili, la tatu au la nne. Labda, kwa hakika, wataambiwa “wamefeli.” Wazazi wao watalia, watawafokea au kuwachapa mpaka wasijue kama wanalia kwa uchungu au basi tu kwa sababu ya kujisikia kutokupendwa. Marafiki zao watawasalimia kwa huruma na kushukuru kuwa angalau balaa la kukosa shule halijawakumba wao. Maisha yao yataonekana kama yamevurugika kiasi kwamba baadhi yao watajaribu hata kujidhuru kama namna ya kukabiliana na aibu waliyojisababishia. Hawa ndio watoto ninaotamani ningeweza kuwapa kila kitu, kitakachowapa kila aina ya uhakika, kitakachowaongezea kila hali ya kujiamini, waweze kuwa na imani na nguvu na ahadi walizonazo.

Siku kama ya leo, kila wakati matokeo yanapotoka, ninatamani kungekuwa na tuzo na habari zinazopamba kurasa za mbele za magazeti kuhusu msichana anayejisikia fahari kuwa ameweza kumaliza mtihani wake safari hii, au mvulana ambaye, hatimaye, alifanikiwa kuelewa swali ngumu zaidi linalopima uelewa hata hakuweza kubahatisha kulifanya. Kwa watoto waliofikiri wameshindwa mtihani, wakajikuta wanafurahi kuchaguliwa kujiunga na “shule za kata,” lakini zinazowakuza kuwa watu timamu. Kwa mapacha ambao hawakuwahi kuota kuwa na uwezo wa kujiunga na shule maarufu, na walihitaji tu kwenda shule ya sekondari karibu na nyumbani, yenye uwanja mkubwa wenye majani unaofaa kucheza. Hawa watoto wanastahili kupongezwa. Hata mmoja wao hastahili kufanywa ajione hana thamani.

Matarajio magumu ya mafanikio ya kitaaluma yenye chembechembe za ukoloni mambo leo humaanisha njia moja—moja nyembamba na ya kikatili—ya watoto “kufanikiwa.” Mfumo wa elimu unawaaminisha watu kwamba usipoweza kwenda kwenye shule ya chekechea “sahihi”, shule bora ya msingi, shule nzuri ya sekondari, “kupata” ufadhili na kusota ufanikiwe kutokea kwenye upande wa pili ukiwa daktari, mwanasheria, au—ukishindwa kabisa—injinia, hiyo isipokuwa njia yako, basi hustahili kusifiwa kwa vyovyote na familia yako hasa nyakati za Krismasi. Sihitaji kumwambia yeyote kati yenu kwamba mtazamo huu hauko sahihi. Bado wengi wetu, hivi ndivyo tulivyolelewa, na huenda tuliambulia pete ya shaba au tuliacha ipotee.

Ninatamani mfumo wa elimu unaotambua kuwa kila mtu ana akili kwa namna yake. Natamani jamii inayoungwa mkono na vyombo vya habari na asasi za kiraia zinazotambua tofauti hizo za kiakili kwa vitendo. Ninatamani kuwaambia watoto wanaojisikia kukataliwa na waliozidiwa na hatia, wanaowashuhudia wenzao wakienda kwenye shule na vyuo vya kifahari, kwamba kitu muhimu wanachoweza kufanya na maisha yao ni kile kinachowapa utoshelevu kupita wote, na kwamba kitu hicho si lazima kiwe kushona mwili wa binadamu; inaweza, kwa hakika, kuwa ni kuunganisha mabomba ya vyoo, bafu au makaro ya kunawia mikono. Kwamba maisha yasiyohusiana na vitabu au kuvaa yale makofia ya mawakili sio maisha, kwamba kuwa na akili na kuwa bora ina maana ya kutokuendesha maisha yako kwa kutengeneza keki, au kubuni stempu za posta au kuwa dereva wa kuendesha lori kubwa kwa umahiri na umakini kuzunguka nchi nzima ukipita kwenye barabara mbovu zenye mashimo, au kutengeneza kucha kwa ustadi na ubunifu.

Ustawi wa nchi yetu unategemea ujuzi wote huu. Kuanzia ujuzi wa kukusanya takataka, hadi kufanya upasuaji wa mwili wa mwanadamu, tunahitaji kazi zote hizi. Au tunatamani tuwe na mazingira ambayo kila mtu nchi hii ni daktarimwanasheriainjinia tukiangaliana, sisi hao hao tunatengeneza magari, tunatembelea vyumba vya upasuaji, tukisoma vitabu, tukitengeneza vifaa vya vyumbani, tukienda Tobago, au kuchimba kokoto za ujenzi?

Kwa watoto wote wanaojisikia kushindwa:

Hamjashindwa.

Hata kama hamjafaulu mtihani huu.

Thamani yenu haijapungua. Hamjakosa uwezo wowote. Hamjapungukiwa chochote.

Dunia bado ina vingi kwa ajili yetu kama ilivyo kwa kila mtu.

Nyie bado, na mtaendelea kuwa, watu wenye nguvu, wanaoweza kuwa chochote kile mpendacho.

Na ndio, ninawaahidi, nyie ni zaidi ya bora.

 

Mkusanyiko wa mashairi ya Shivanee Ramlochan, uitwao “Everyone Knows I Am a Haunting,” uliwania Tuzo za  Felix Dennis 2018 kwenye kipengele cha mkusanyiko bora wa kwanza.