Watumiaji wa simu za mkononi wanajilinda vya kutosha dhidi ya ukiukwaji wa haki ya faragha?

Portrait photo of French engineer Gaël Duval.

Duval, Mhandisi wa Kifaransa na mwanzilishi wa Taasisi ya Gaël. Picha imetumiwa kwa ruhusa.

Kwa kampuni za mtandao wa intaneti na teknolojia, ukusanyaji wa taarifa za watumiaji wa mtandao wa intaneti umekuwa ni chanzo chao kikuu cha kujipatia kipato. Hata hivyo, namna hii ya kujipatia kipato inawaweka hatarini watumiaji kama inavyojidhihirisha katika matukio ya mara kwa mara ya uwekaji wazi wa taarifa za kibiashara, uvujaji mkubwa wa taarifa na udukuaji. Je, kuna njia muafaka ya kuboresha haki ya faragha ya watumiaji wa mtandao wa intaneti?

Kampuni kama vile Google na Apple zimewekeza nguvu kukusanya kila siku taarifa za wateja wao, haswa kupitia simu za mkononi, na muunganiko wa vitumizi mbalimbali vinavyotumiwa mara kwa mara kama vile kalenda na ajenda. Vitumizi kadha wa kadha vimekuwa vikifuatilia mahali halisi mtu alipo, na kwa upande mwingine vitumizi vya masuala ya afya na michezo vikijikita katika kukusanya taarifa za vinasaba vya wateja. Inaaminika kuwa, taarifa hizi zinakusanywa na kuchanganuliwa kwa lengo la kumrahisishia na kumpatia mtumiaji kile anachokihitaji kwa haraka. Hata hivyo, ukweli ni kwamba, watumiaji wa intaneti na vitumizi vya kiteknolojia hawafahamu kuwa, wanatoa taarifa zao bure bila ya malipo yoyote.

Wanaharakati wa masuala ya sera ya faragha ya mtandaoni kama vile  Raia wa Austria, Max Schrems ameonesha hisia zake kuhusu utaratibu huu wa kampuni za intaneti na vitumizi vya teknolojia wa kujipatia kipato kupitia taarifa za wateja wao. Anaangazia hatari ya ongeseko la matukio ya mara kwa mara ya unyanyasaji na ukiukwaji wa sheria ya haki ya faragha. Moja ya matukio kama haya pengine yameelezwa vizuri sana kupitia tukio la skendo ya Facebook linalofahamika kama kesi ya Cambridge Analytica ambapo Taasisi binafsi ya ushauri ya Cambridge Analytica ilijikusanyia taarifa binafsi za watumiaji milioni 87 wa Facebook bila idhini yao kwa lengo la ” kuwasaidia wagombea kiti cha Urais Ted Cruz na Donald Trump mapema mwaka 2016″.

Schrems anasema kuwa aliwatahadharisha wawakilishi wa Facebook kuhusu matukio ya ukusanyaji taarifa za wateja wao uliokuwa unafanywa na taasisi ya Cambridge Analytica, na hata hivyo, hakuweza kuwashawishi kuchukua hatua:

Wawakilishi wa Facebook bila kumumunya maneno walisema kuwa kwa maoni yao, unapotumia jukwaa la mmiliki fulani unakuwa umeruhusu watu hao wapakie vitumizi vyao [kwenye simu za mkononi na vifaa vingine] kwa ajili ya kukusanya taarifa za mtumiaji.

Hata hivyo, ni kwa nini ujiulize kuhusu haki ya faragha mtandaoni ilhali huna chochote cha kuficha? Mwanaharakati Edward Snowden alikuwa na majibu ya swali hili katika mjadala wa mtandao wa Reddit mwaka 2015:

Kufikiri kuwa hujali chochote kuhusu haki ya faragha mtandaoni kwa kuwa huna cha kuficha ni sawa na kufikiri kuwa hujali chochote kuhusu haki ya kujieleza kwa kuwa huna chochote cha kusema.

Hali halisi ya madhara yatokanayo na matumizi ya majukwaa ya teknolojia ya habari

Mhandisi wa Kifaransa wa vitumizi vya kompyuta na mtaalam wa masuala ya data, Gaël Duval amejihusisha kwa muda mrefu katika uundaji wa vitumizi vya kompyuta ikiwa ni pamoja na kitumizi cha Linux cha Mandrake– ambao ni mfumo endeshi(wenye mrengo wa keneli ya Linux) ambao kila mtu ana haki ya kuuboresha na kisha kutumiwa na wengine.

Duval aliamua kuunda mfumo endeshi ambao unaosaidia kutoa ulinzi wa uhakika wa taarifa za watumiaji wa simu za mkononi: /e/OS.

Global Voices iliongea naye ili kufahamu namna teknolojia ya habari inavyoathiri maisha ya watu, fursa zilizopo na madhara yake. Huu hapa ni mtazamo wake kuhusu maendeleo ya teknolojia hii ya habari: 

Hili ni swali la kifalsafa. Binafsi nina hisia mchanganyiko haswa kuhusu teknolojia ya habari kwa kuwa, mimi wakati wote nina mahaba makubwa kuhusu teknolojia. Hata hivyo, kuna wakati ninahisi kuchoshwa, ninakumbuka nyakati zile ambazo ukihitaji kupiga simu, unaenda sehemu maalum iliyotengwa. Bila shaka yale yalikuwa maisha murua kabisa na yasiyo na haraka.  Vijana wanaweza kushangaa kuwa, hadi nilipofikisha miaka mitano, nyumbani hakukuwa na simu wala runinga. Kuna wakati ninawaza kuwa niliishi maisha ya ulimwengu tofauti kabisa,  na ambayo kwa sasa hayapo kabisa. Kwa upande mwingine, inafurahisha sana haswa tunapojaribu kuwaza ni jambo gani tunaweza kufanya kwa uwepo wa teknolojia za kisasa, kama vile kuwasiliana na mtu aliye sehemu tofauti kabisa ya ulimwengu kupitia picha za video za ubora wa hali ya juu sambamba na kushuhudia magari ya umeme yasiyotumia petroli inayojaza mapafu yetu kwa moshi hatari. 

Kwa wale wanaokumbuka, ukiachilia raha na karaha za miaka ya kipindi cha mfumo wa analogia, kwa sasa tunakabiliana na hatari kubwa ya utegemezi kwenye teknolojia ya habari. – Utafiti uliofanyika mwaka 2018 uliohusisha  matatizo ya kitabia ya watoto na mazoea yaliyopitiliza ya matumizi ya simu janja , ulibaini kuwa, matumizi makubwa ya simu janja hupelekea matatizo kadha wa kadha yakiwemo Tatizo la Kukosa Umakini (ADD) na sonona. Utafiti uliochapishwa mwaka 2020 na Common Sense Media ulibaini kuwa asilimia 50 ya vijana katika jimbo la Los Angeles walisema wasingeweza kukaa bila kutumia simu janja zao .

Madhara yatokanayo na matumizi ya teknolojia hizi hivi karibuni yaliwekwa bayana na vyanzo vya kuaminika katika makala ya Netflix ya  The Social Dilemma, ambayoinayoelezea ushuhuda wa wafanyakazi wa zamani wa kampuni kubwa zikiwemo Google, Twitter na Facebook – wanaoelezea ni kwa namna gani walivyokuwa wanaweka mazingira ya kushawishi mtumiaji kujenga uraibu wa vutumizi kwa minajili ya vipato.

Baadhi ya serikali zimejaribu kukabiliana na tatizo hili kwa kuboresha sheria ili kujenga uelewa wa watumiaji sambamba na kuongeza uwajibikaji kwa makampuni husika. Mwaka 2018, Umoja wa Ulaya (EU) ulipitisha Sheria Mama ya Ulinzi wa Taarifa (GDPR) Sheria hii imeongeza matakwa kadhaa kuhusu utunzaji wa taarifa ikiwamo kupata ridhaa isiyo na shaka ya mtumiaji kuhusu taarifa zake na kuyataka makampuni husika kuondoa taarifa hizi baada ya kipindi cha miaka mitatu bila kushurutishwa. Pia, sheria hii imeweka fidia kubwa kwa wale ambao hawataheshimu kanuni hizi.   Hata hivyo, utekelezaji wake unakabiliwa na ukosefu wa vitendea kazi katika mamlaka za serikali, na pia, sheria hii inayahusu tu mataifa wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Nyenzo ya kuwawezesha watumiaji wa teknolojia ya habari 

Kwa jinsi hali ya mambo ilivyo sasa, Duval alishawishika kuandaa nyenzo itakayowawezesha watu kuchukua jukumu la kulinda taarifa zao wenyewe, kama anavyoelezea: 

Motto wetu ni kuwa “Taarifa zako ni zako,” kwa kuwa taarifa zetu ni mali yetu, na kwa wale wanaodhani kuwa haipaswi kuwa hivyo, hawataki uhuru na amani, au wanamiliki biashara inayoneemeshwa kwa matangazo- kwa kuwa taarifa binafsi za mtu zinaweza kusaidia kuuza matangazo kwa bei ghali zaidi.

Hivi ndivyo mfumo endeshi aliouunda unavyofanya kazi:

/e/ ni mfumo endeshi msawazo wa kidigitali wa simu janja ambao hautumi taarifa yoyote [kwenda Google] kama vile unapoperuzi, mahali ulipo… na unaozingatia faragha ya mtumiaji. Mfumo huu haukagui kwa namna yoyote taarifa binafsi za mtumiaji. Unatoa pia huduma za msingi   za mtandaoni kama vile barua pepe, hifadhi, kalenda, kuhifadhi mawasiliano – kila kitu kinachohusiana na mfumo endeshi wa simu janja. 

Duval anasema kwamba, linapokuja suala la taarifa binafsi za mtu, Google na Apple wana malengo yanayofanana – taarifa hizi zinapalilia mfumo wa kibiashara wa Google, ambao kimsingi unategemea bilioni 8 hadi 12 kila mwaka kwa ajili ya kuweka kitumizi cha kuperuzi cha Google kwenye iPhones na iPads.

Duval aliongeza:

Kwa kutumia iPhone, mtumiaji anatuma wastani wa MB 6 za taarifa zake kwenda Google, kwa siku. Ni mara mbili ya kiasi kinachotumwa na watumiaji wa mfumo endeshi wa Android. Mbali na hivyo, mfumo wa nje wa Apple umefungwa vilivyo, na kukosekana kabisa kwa uwazi wa kinachoendelea ndani. Yapaswa tu kuwaamini. Sisi kwa upande wetu,  tunaruhusu “kubadilisha sera ya faragha”: mifumo yote ya /e/OS na nyenzo za matengenezo za hifadhi ya mtandaoni (vitu vilivyotumiwa katika uundaji wa mfumo huu) zinapatikana bure. Mfumo huu unaweza kuhojiwa na kukaguliwa na wataalam. 

Katika mazingira ya ongezeko kubwa la matumizi ya simu janja, ni dhahiri kuwa sheria pekee hazitoshi katika kujenga uelewa na kuwapatia watumiaji nyenzo sahihi na maarifa ya kulinda taarifa zao – na hapa ndipo unapokuja umuhimu wa nyenzo za kidigitali zinazowasaidia watumiaji kuwajibika zaidi

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.