- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Baada ya Magufuli, Tanzania itarekebisha sheria kandamizi za maudhui ya mtandaoni?

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania, Haki za Binadamu, Sheria, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza, Utawala, GV Utetezi

Wakala wa huduma za kifedha za simu akisubiri wateja jijini Dar es Salaam, Tanzania. Chini ya kanuni za maudhui za 2020, uhuru wa kujieleza umebanwa na ada kubwa na mamlaka ya serikali kuondoa “maudhui yasiyoruhusiwa.” Picha imepigwa na Fiona Graham [1]/WorldRemit kupitia mtandao wa Flickr, CC BY SA 2.0 [2].

Makala haya ni sehemu ya UPROAR [3], mradi wa Vyombo Vidogo vya Habari vinavyoziomba serikali kushughulikia changamoto za haki za kidijitali kwenye jarida la Universal Periodic Review (UPR) [4]

Mwanzoni mwa mwezi Machi, wakati wa-Tanzania walipoanza kuhoji afya na mahali alipo [5] Rais John Magufuli, raia wengi walitumia mitandao ya kijamii kuuliza maswali na hata kuonesha wasiwasi wao.

Katika kujibu maswali hayo, serikali ilitishia kumkamata mtu yeyote aliyetumia mitandao ya kijamii kusambaza taarifa potofu kuhusu rais. Mamlaka za serikali zilirejea Sheria ya Makosa ya Mtandao  [6]ya Tanzania ya mwaka 2015 na Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandao) [7] (EPOCA) zilizotungwa mwaka 2020 kuelezea uwezekano wa kuwakamata na kuwaweka ndani wote waliovunja sheria hizo.

Huu ulikuwa ni mwendelezo wa hatua za serikali, ambayo mara kadhaa, imetumia sheria za makosa ya mtandao na kanuni za maudhui ya mtandaoni kudhibiti na kubana haki za kidijitali na uhuru wa maoni nchini Tanzania.

Mnamo Machi 17, aliyekuwa Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan alitangaza kwenye televisheni ya taifa [8] kwamba John Magufuli amefariki. Siku chache baadae, Hassan aliapishwa kuwa rais wa sita wa Tanzania.

Hadi wakati huo,  watu wasiopungua wanne walikuwa wamekamatwa [9] katika maeneo mbalimbali ya nchi kwa kosa la “kusambaza uvumi wa uongo” kuhusu afya na mahali aliko Magufuli.

Wengi hivi sasa wanajiuliza ikiwa Tanzania itapitia upya kanuni zake zinazodhibiti maudhui ya mtandaoni baada ya utawala wa Magufuli, au ikiwa sheria hizi zitaendelea kutumika mpaka mwaka 2025 – kipindi cha Magufuli kilichobaki kitakachokamilishwa na Rais Samia Hassan.

Mapema mwezi Machi, Innocent Bashungwa, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wa Tanzania, alitoa tahadhari [10] kwa vyombo vya habari kuepuka kusambaza “uvumi” kuhusu  aliko Magufuli, ambaye wakati huo alikuwa hajaonekana hadharani tangu Februari 27.

Aidha, Waziri wa Sheria na Mambo ya Katiba, Mwigulu Nchemba, pia aliwatishia watumiaji wa mitandao adhabu ya kifungo [11] kupitia akaunti yake ya Twita kwa kosa la kusambaza uvumi “wa kijinga,” akirejea Kifungu cha 89 cha Kanuni za Adhabu na Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao.

Mkuu wa Polisi Ramadhani Kingai alionesha nia ya kutaka kuifahamu [12]akaunti ya Twita yenye jina la “Kigogo,” ambayo kwa muda mrefu imejipambanua kuanika mabaya ya serikali.

Wanaharakati wa haki za binadamu wameshutumu hatua hizi zinazochukuliwa na maafisa wa serikali na hali ya woga inayojengwa na kanuni hizi sambamba na vitisho vinavyoambatana na utekelezaji wake.

Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni: Kubanwa zaidi kwa haki za kidijitali

Kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita, Tanzania imefurahia mtandao madhubuti na maendeleo makubwa ya mawasiliano na teknolojia.

Pamoja na maendeleo hayo, serikali imekuwa ikijiwekea mazingira ya kudhibiti makampuni na majukwaa ya majadiliano na kwa sababu hiyo vyombo huru vya habari vinashindwa kujipambanua [13] kwa maana ya aina ya maoni yanayochapishwa na sura ya uwakilishi wake.

Mtandao wa Intaneti umetengeneza jukwaa jipya mtandaoni kwa wanablogu vijana wa Tanzania na wanaharakati wanaotumia mitandao ya kijamii kupaza sauti zao, lakini serikali haionekani kukubaliana na ukweli huu mpya.

Mwaka 2010, Tanzania ilichapisha Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta [14], ambayo ilikuwa ya aina yake nchini humo.

Kufikia 2018, kanuni mahususi zinazodhibiti maudhui ya mtandaoni zilitolewa kupitia Kanuni za Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) 2018 [15]. Serikali ilidai kwamba kanuni hizi zililenga kufuatilia kwa karibu matumizi ya mitandao ya kijamii, hususani, kupambana na tatizo la habari zinazoeneza chuki na uzushi mitandaoni.

Hata hivyo, kanuni hizo si tu zilitumika dhidi ya vyombo vikuu vya habari lakini pia kwa wanablogu mmoja mmoja na watoa huduma za maudhui, ambao walishangazwa na takwa jipya la kisheria la kulipa kiasi cha dola za Marekani 900 [16] ili kupata leseni. Takwa hili pia lilimhusu yeyote anayetayarisha na kurusha mubashara matangazo ya televisheni au radio mtandaoni.

Giza kubwa lilitanda kwenye mitandao ya kijamii kufuatia takwa hili la ghafla la ada ambapo wanablogu wengi na wazalishaji wa maudhui waliamua kuachana na shughuli zao kwa sababu ya gharama hizo kubwa. Wanasiasa wa upinzani na watumiaji wa mitandao ya kijamii walikosoa vikali kanuni hizi [17] kwa kupoka uhuru wa mitandao ya kijamii pamoja na asasi za kiraia.

Mwaka 2020, Tanzania ilitoa marekebisho mapya ya kanuni za maudhui ya mtandaoni [18], chini ya kifungu cha 103 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta, 2020, na kuanza kutumika Julai 2020, na kuzitangaza kupitia Tangazo Na 538 katika Gazeti la Serikali.

 Baadhi ya tofauti kubwa kati ya toleo la 2018 na 2020 [19] la Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni o (EPOCA) ni kama ifuatavyo:

Kwanza, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitengeneza upya makundi ya ada [20] na kuongeza makundi madogo chini ya maudhui ya mtandaoni yaani: taarifa & habari, burudani na elimu au dini, na kuendelea kuzuia watu binafsi kutoa maudhui.

Kanuni ya Maudhui Mtandaoni ya 2020, Sehemu VI, Kifungu cha 116:

Mtu yeyote anayetoa huduma za mtandao bila kupata leseni muafaka, anafanya kosa na adhabu yake ni hukumu ya kulipa faini isiyopungua Shilingi za Kitanzania milioni 6 [dola za marekani 2,587] au kifungo cha jela kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja.  

Pili, TCRA iliongeza orodha ya “maudhui yasiyoruhusiwa” na kujumuisha, pamoja na mambo mengine, maudhui yanayohamasisha kurekodi simu za watu, kupeleleza mawasiliano, kuiba data, kufuatilia mawasiliano, kurekodi na kuingilia mawasiliano au mazungumzo bila ruhusa.

Tatu, Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni (EPOCA 2020) pia zimepunguza kipindi ambacho mwenye leseni anaweza kufanyia kazi ukiukwaji wa kanuni za maudhui kwa kusimamishwa au kufutiwa akaunti. Chini ya kanuni za 2018, mwenye leseni alikuwa na saa 12 za kufanya hivyo. Lakini kwenye kanuni za 2020, chini ya Sehemu ya III, kifungu cha 11, muda wa kushughulikia ukiukwaji wowote wa maudhui ulipunguzwa na kuwa saa 2. Kushindwa kuheshimu muda huu kunaipa mamlaka ruhusa ya kuingilia, ama kwa kuifungia au kuiondoa akaunti husika.

Global Voices ilizungumza na baadhi ya wataalam wa sheria na haki za binadamu ambao walikosoa marekebisho ya Kanuni za Maudhui ya 2020, wakisema yanabana haki za kidijitali na haki za asasi za kiraia. Walisema kuwa kanuni hizi zinabana haki za kidijitali na kuwazuia wanablogu na waandishi kumiliki maudhui ya mtandaoni.

Tatizo kubwa hapa ni kwamba hakuna tahadhari zimeweka kuzuia mamlaka haya yasitumike vibaya, na kwa hali ilivyo hivi sasa, mamlaka haya yana madhara kwenye uhuru wa kujieleza kwa haki nchini Tanzania, alisema mmoja wa wataalam wa haki za binadamu aliyeomba asifahamike.

Baada ya Magufuli: Mustakabali wa haki za kidijitali Tanzania

Chini ya utawala wa Magufuli, asasi za kiraia, vyombo vya habari na haki za kidijitali zimekuwa zikizorota kwa kasi  [21]kufuatia kubanwa, hatua kwa hatua, kwa uhuru wa maoni mtandaoni.

Baada ya kifo cha ghafla cha Magufuli, wengi sasa wanajiuliza kuhusu mustakabali wa haki za kidijitali nchini humo  — baada ya miaka sita ya uongozi ulioendelea kuonesha dalili za mabavu.

Global Voices iliongea na baadhi ya maafisa wa serikali kwa sharti la kutokutajwa majina kuhusu kanuni mpya na  hali ya haki za binadamu na uhuru wa maoni mtandaoni. Mtaalam mmoja wa haki za biandamu nchini Tanzania aliiambia Global Voices, kwa sharti ya kutokutajwa:

The regulations are not fair as anyone can be criminalized, because not many citizens understand the implications of these regulations.

Kanuni hizi si za haki kwa sababu yeyote anaweza kutiwa hatiani, kwa kuwa si wananchi wengi wanaelewa tafsiri ya kanuni hizi.

Mwingine alifikiri kwamba serikali inachukulia mitandao ya kijamii kama “kero.” Aliwatahadharisha wananchi kuchukua tahadhari wanapozungumza kwenye majukwaa ya wazi kwa sababu serikali ina nguvu za kisheria kupata taarifa zao zote kupitia wamiliki wa majukwaa hayo.

Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni za mwaka 2020 zinafanya “isiwezekane kabisa” mtu kutokufahamika unapokuwa mtandaoni, chini ya Kanuni ya 9(e), “watoaji wa huduma ya vyumba vya kuuza mtandao wa inteneti (internet café) wanalazimika kujisajili kwa kutumia vitambulisho vinavyotambulika, kuweka utambulisho pekee wa mtandaoni kwa kila kompyuta (IP address) na kufunga kamera za usalama kurekodi shughuli zote zinazoendelea kwenye maeneo yao ya kazi,” kwa mujibu wa uchambuzi huu uliofanywa na Baraza la Habari la Tanzania.  [19]

Kanuni hizi zinachangia vitendo vya jinai vya kuchafua heshima za watu, kuzuia haki ya kutokufahamika, kutoa adhabu kali kwa kukiukwa kwa kanuni hizi na kukabidhi mamlaka makubwa mno ya kuondoa maudhui [22] kwa TCRA na vyombo vingine vilivyo chini yake.

Kanuni za Maudhui ya Mtandaoni (EPOCA) zinapingana [23] na viwango vya kimataifa vilivyokubalika vya haki za kidijitali. Jumla ya yote, kanuni hizi zinabana uhuru wa maoni na uhuru vya vyombo vya habari nchini Tanzania.

Hata hivyo, serikali ya Tanzania inawajibika kuheshimu na kutunza haki za watu kujieleza na kukusanyika  — ikiwa ni pamoja na wanahabari, wanachama wa asasi za kiraia, na wanasiasa wa upinzani, kwa mujibu wa katiba ya Tanzania pamoja na mikataba ya kimataifa na ile ya jumuiya za kimaeneo. Haki hizi ni muhimu kwa minajili ya kuwezesha haki ya kupiga kura [13].

Tanzania iko kwenye mtanziko wa haki za kidijitali.

Chini ya Rais Hassan aliyeapishwa hivi karibuni, swali la kujiuliza ni ikiwa Chama Cha Mapinduzi kitaendelea kunyamazisha na kubana haki za kidijitali nchini humo?

Dokezo la Mhariri: Mwandishi wa makala haya ameomba jina lake lisifahamike kwa sababu za kiusalama.