- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Kubadilika kwa Utawala Nchini Tanzania: Kutoka Rais Magufuli mpaka Rais Hassan

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania, Haki za Binadamu, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza, Utawala, COVID-19

Kuipeleka Tanzania mbele halikuwa jambo lililowezekana kirahisi sana, Rais John Magufuli alipoingia madarakani mwaka 2015. Kauli mbiu yake ilikuwa “Hapa Kazi Tu,” ikionekana kwenye kofia ya kijani na njano, rangi za chama kinachotawala nchini Tanzania, Chama cha Mapinduzi, kilichoongozwa na Magufuli. Picha na Pernille Baerendtsen, imetumiwa kwa ruhusa.

Maelfu ya watu wanakusanyika kwenye viwanja vya michezo, viwanja vya ndege na pembezoni mwa barabara, katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, maeneo ambayo mwili wa hayati Rais John Pombe Magufuli ulisafirishwa  kutoka Dar es salaam kuwawezesha wananchi kumuagwa kwa heshima kwa juma zima [1] jijini Dodoma, yalipo makao makuu ya serikali, visiwa vya Zanzibar, Mwanza na Chato, nyumbani kwake, pembezoni mwa Ziwa Victoria, ambako atazikwa.

Magufuli alitangazwa kufariki dunia [2] akiwa na umri wa miaka 61, mnamo Machi 17, katika hotuba ya aliyekuwa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, iliyorushwa kwenye kituo cha televisheni ya taifa, tangazo lililomaliza majuma kadhaa ya uvumi kuhusu hali ya afya ya rais na mahali alipo. Inadaiwa alifariki kwa maradhi ya moyo:

Kifo cha ghafla cha Magufuli, hata hivyo, kimewaacha wa-Tanzania, na watu wengine, wakidadisi hatma ya siasa na utawala [5] katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

Siku ya Ijumaa, Hassan aliapishwa [6] kuwa rais wa sita wa Tanzania, akiandika historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Tanzania, Rais wa pili kuzaliwa kwenye visiwa vya Zanzibar ambavyo ni sehemu ya Tanzania, na mwanamke wa kwanza mwislamu kuchukua nafasi ya juu kabisa ya utumishi nchini humo.

Chini ya katiba ya Tanzania, Hassan atatumikia kipindi chote kilichobaki cha muhula wa miaka mitano wa urais wa Magufuli uliokuwa uende mpaka 2025.

Katika video hii fupi, [7] inayosambaa sana kwenye mitandao ya kijamii, Hassan anapuuza mashaka yoyote kuhusu uwezo wake wa kuongoza kama mwanamke:

Kwa wale wote wenye mashaka kwamba mwanamke huyu ataweza kuwa rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ningependa kuwaambia kuwa huyu aliyesimama hapa ni rais [makofi] … ningependa kurudia kwamba aliyesimama hapa ni rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwenye maumbile ya kike.

Wakati wa-Tanzania wangali wakimwombolezea Magufuli na kuendelea kutafakari mabadiliko haya ya ghafla, wengi wanaonekana kuwa na matumaini makubwa na Hassan.

Mwanasiasa wa upinzani Zitto Kabwe, kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, ana matumaini na historia ya Hassani katika harakati na kazi kama “mwanachama wa asasi za kiraia.”

Wakati Hassan akifahamika zaidi kama mtu mpenda maridhiano [11], akitoa wito wa umoja na utulivu katika kipindi hiki cha mpito, Magufuli anafahamika kama “bulidoza,” [12] jina la utani alilolipata kama Waziri wa Ujenzi kutambua ufanisi wake wa kuhakikisha barabara zinajengwa.

Kumkumbuka Magufuli

Kanga ikimkumbuka marehemu John Magufuli, rais wa tano wa Tanzania, aliyefariki mnamo Machi 17, 2021. “Buriani baba yetu mungu akulaze pema / Tutakukumbuka daima shujaa wetu”

Wa-Tanzania wengi  — na Waafrika  kwa ujumla— wanamkumbuka Magufuli kwenye mitandao ya kijamii kwa “mabaya na mazuri.”

Mabaya na mazuri ya Magufuli hayawezi kupingika kwa uzito unaofanana, na hiyo ina maana kuwa kumbukumbu anayoiacha nyuma ina utata wake lakini yenye maana kubwa. Kambi za wanaomwuunga mkono Magufuli na wanaompinga Magufuli hazitakaa zikubaliane na mjadala utaendelea kwa miaka mingi.

Magufuli alijipatia umaarufu katika siku za mwanzo za urais wake kwa ahadi zake za kupambana na ufisadi kwa nguvu. Jitihada zake za kuanzisha miradi mikubwa inayolenga kuimarisha miundombinu na maendeleo ya viwanda ilikuza matumaini ya wa-Tanzania wengi kujitegemea baada ya miongo mingi ya kutegemea misaada ya kimataifa.

Mwezi Aprili mwaka jana, mathalani, Magufuli alikataa mkopo wa dola bilioni 10 [14] (dola za Marekani) kutoka China kwa ajili ya mradi wa bandari kubwa unaopendezwa kutekelezwa Bagamoyo karibu na jiji la Dar es Salaam, akisema, “ni mlevi pekee anayeweza kukubaliana na masharti haya.”

Kanga hii ikimnadi Rais Magufuli kuelekea kwenye uchaguzi wa mwaka jana. Inasomeka: “Uliahidi Umetenda Tunatushukuru.”  Inapambwa na picha za mafanikio ya Magufuli kwenye  ujenzi wa barabara, ununuzi wa ndege, ujenzi wa madaraja na reli ya kisasa. Picha na Pernille Baerendtsen, imetumiwa kwa ruhusa.

Msimamo wake dhidi ya ufisadi pia ulizivutia nchi za Magharibi, na vyombo vya habari  mwanzoni viliandika msimamo wake [15] kwa mtazamo chanya.

Kwa baadhi, Magufuli anakumbukwa kama “mwana wa Afrika kweli kweli” [16] na mtetezi wa Afrika aliyetanguliza maslahi ya Afrika [17]. Wengine wanamkumbuka kama rais “aliyependa  umaarufu” akitanguliza uzalendo kuliko kitu kingine chochote: 

Nimekuwa nikifuatilia Tanzania inavyomwombolezea John Magufuli. Tulipinga njia zake za kidikteta na kumkosoa kwa tabia yake ya kupuuza sayansi, lakini ni wazi, kwa kutazama watu wanaosimama barabarani [kumuaga], huyu jamaa alikuwa maarufu.

Hata hivyo, utawala wa Magufuli alikuwa wa kimabavu [5]na hivyo kuathiri sana haki za binadamu na uhuru wa kujieleza. 

Kwa zaidi ya miaka sita, mashirika ya Human Rights Watch, Amnesty International, Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ), Global Voices na mengineyo  yamekuwa yakifuatilia kuzorota kwa ulinzi wa haki za kiraia na haki za binadamu [21].

Tanzania ilishuka nafasi sita kwenye kipimo cha Uhuru wa Kujieleza [22] kilichopima demokrasia na uhuru kati ya 2020 na 2021.

Wakati Bunge lilipokuwa likijadili Sheria ya Vyama vya Siasa Januari 2019, sheria iliyokosolewa kwa kuvibana zaidi vyama vya siasa, hiyo ilitafsiriwa kama dalili mbaya hasa bundi alipoonekana ndani ya jengo la bunge. [23]

Utawala wa Magufuli mara kadhaa ulitumia sheria mbalimbali kama ile Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya Mtandaoni) [24] (EPOCA), au  Sheria ya Makosa ya Mtandao [25]kubana sauti pinzani na maoni huru. Mabadiliko ya kanuni mbalimbali ya mwaka 2020 yalilenga kuwazuia wananchi kusambaza habari “zinazoweza kusababisha uvunjivu wa amani au uchochezi” na “maudhui yenye habari zinazohusu magonjwa ya mlipuko au magonjwa hatari” bila kuithibitishwa na serikali kupitia kwa maafisa wake wa juu [26].

Raia hawakuweza kuzungumza chochote kuhusu tetemeko lililoyakumba maeneo ya pwani [27] mwezi uliopita, mbali na habari za mlipuko nchini humo uliotokea miezi kadhaa baadaye.

Na wakati wa majuma mawili ya uvumi kuhusu alipo hasa Magufuli pamoja na afya yake mapema mwezi Machi, watu wasiopungua wanne walidaiwa kukamatwa [28]kwa kosa la kutwiti kuhusu ugonjwa wa rais.

‘Au alifariki kwa Korona?’

Magufuli anasemekana alifariki kwa maradhi ya moyo— ambayo inasemekena amekuwa akipata matibabu yake kwa miaka 10. Lakini kifo cha ghafla cha Magufuli kiliwaacha wengi wakihoji kama huenda aliambukizwa  [29]virusi vya Korona (UVIKO-19).

Kwa wengi — hasa nchi za ki-Magharibi — Magufuli atakumbukwa kwa kukana uwepo wa ugonjwa wa Korona nchi mwake.

Wakati ugonjwa huu unaingia Tanzania, serikali ilichukua tahadhari pamoja na kutoa miongozo [30] ya namna ua kupambana na kusambaa kwa ugonjwa huu, lakini baadae, mara kwa mara, Magufuli amekuwa alilichukulia zuio la  watu kuendelea na shughuli zao kama tishio kubwa  [31]la uchumi kuliko virusi vya ugonjwa huu.

Mara nyingi alipinga mwongozo wa kimataifa kuhusu kanuni za afya kama kuvaa barakoa, kuepuka misongamano na chanjo — akiwasihi wananchi kutegemea maombi na tiba za asili [32] kama hatua mbadala.

Baada ya Magufuli kuzuia kutangazwa kwa takwimu za maambukizi ya Korona mwaka jana mwezi Aprili, alisisitiza kwamba Korona imeshindwa kwa nguvu za maombi. [33]Baadae kidogo, alitangaza kwamba Tanzania  “haina ugonjwa wa Korona [34].”

Ingawa haiwezekani kusema ni kwa kiwango gani Korona iliiathiri Tanzania, tunachofahamu ni kwamba Korona haikuondoka.

Mlipuko mpya wa Korona ulipotokea Januari, wa-Tanzania wengi walizungumzia shuhuda zao kwenye mitandao ya kijamii wakisimulia vile walivyougua ugonjwa wenye dalili kama Korona. Kwa kufahamu kuwa wangeweza kukamatwa kwa kosa la kujadili Korona, mijadala hiyo ilikwenda kwa jina la nimonia mpya [35] na “changamoto za upumuaji.”

Lakini Magufuli aliendea na msimamo wake wa kupinga chanjo katika hotuba [36] aliyoitoa nyumbani kwake Chato, mnamo Januari 27:

Kama mzungu anaweza kuja na chanjo, basi angeshagundua chanjo ya UKIMWI; angeshagundua chanzo cha kifua kikuu; na sasa hivi angeshajua chanjo ya malaria; angeshapata chanjo ya kansa.

Kauli hii inaweza kuchukuliwa kama kumrudisha nyuma mtangulizi wa Magufuli, Rais Jakaya Kikwete, aliyewahi kuhudumu kama balozi wa dunia kwa kinga mwanzoni mwa 2016 [37].

Mwezi uliopita, Magufuli hatimaye alikiri [38]kwamba nchi yake ina tatizo la korona, akiwasihi wa-Tanzania kuvaa barakoa walizotengeneza wenyewe. Wadadisi wa mambo wanasema hatua hii ya Magufuli kubadili mtazamo kuhusu korona ilichangiwa na kifo cha Makamu wa Zanzibar  Seif Sharif Hamad [39].

Maafisa kadhaa wa ngazi za juu  [40]kutoka kwenye tabaka la wanasiasa maarufu walio karibu na Magufuli wamefariki kwa ugonjwa huo.

Wakati makundi ya watu wengi yakiendelea kukusanyika kutoa heshima zao za mwisho kwa hayati rais, kwa upande mwingine kifo chake kimeleta ahueni fulani.

Muda mfupi baada ya kifo cha Magufuli, mwandishi Elsie Eyakuze alijitokeza kwenye mitandao ya kijamii kuzungumza wazi wazi kuhusu maisha yalivyokuwa katika kipindi cha mlipuko wa Korona nchini Tanzania, pale rais alivyoonesha kupuuza kwa makusudi virusi vya Korona.

Katika uzi mrefu kwenye mtandao wa Twitter, alisema:

Sasa. Kwa simulizi halisi nililoshindwa kulisema kwa muda mrefu. #uzi.

Mwezi Machi mwaka 2020, mlipuko wa Korona ulianza kushika kasi duniani kote. Tanzania haikuachwa. Lakini mwezi Aprili ya 2020 tuliachana na juhudi zozote za pamoja kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huu nchini.

Kwenye twiti zake za mwisho, akasema:

“Hivi alifariki kwa Korona?” Ndio, bila shaka. Huyu na yule. Na wao. Wa-Tanzania. Na kwingineko. Lakini sio wale unaotaka kuwazungumzia sio? Wao sio Simulizi lenyewe.

Ni sehemu ya simulizi. Rafiki anakutafuta. “Unaweza?” Naam…tunaweza kulifanya jambo hili likawa baina yetu? “Tafadhali fanya hivyo.”

Nitafanya hivyo. Kesho.

Katika barua ya wazi kwa Magufuli,   [44]Eyakuze anaeleza kubadilika badilika kwa misimamo ya Magufuli, lakini anatumia mbinu ya kuelewa hisia za mwingine, mbinu ambayo inaonekana kumshinda Magufuli mwenyewe  mara nyingine — na kumsamehe.

Wa-Tanzania wanakubaliana na utata na uzito wa kifo cha Magufuli na kumbukumbu anayoiacha nyuma yake — wakati huo macho yao yakiwa yamefungwa yakitazama mbele.