Wanafunzi na Mwalimu Wao Watekwa Huko Kaduna Naijeria, Wakati Maharamia Wenye Silaha Wakifanya Vurugu na Mauaji

Wanafunzi katika Jimbo la Kaduna, Nigeria. Picha na  Jeremy Weate, Januari 15, 2010 kupitia  Flickr / CC BY 2.0.

Maharamia wakiwa na silaha walivamia shule ya sekondari huko Kaduna, Kaskazini Magharibi mwa Nigeria hapo Agosti 24 na kumuua mtu mmoja na kuwateka wanafunzi wanne na mwalimu kiliripoti chanzo cha habari za mitandaoni, SaharaReporters.

Watu hao wakiwa na silaha walifika na kushambulia kijiji cha Damba-Kasaya katika serikali ya mtaa wa Chikun, jimbo la Kaduna mnamo saa 1.45 asubuhi wakiwa kwenye pikipiki na  iliripotiwa kuwa walimuua Benjamin Auta, ambaye ni mkulima, kulingana na taarifa ya gazeti la mtandaoni la Premium Times.

Watu hao wenye silaha walielekea katika shule ya sekondari ya Prince ambapo walimteka  mwalim Christianah Madugu na wanafunzi wanne ambao ni Favour Danjuma, 9, Miracle Danjuma, 13, Happy Odoji, 14, na Ezra Bako, 15.

Baba yake Happy,  Isiaka Odoji,  aliiambia  Daily Trust, gazeti la kila siku la Naijeria kwamba watekaji hao wanadai fedha kiasi cha Naira milioni 20(sawa na Dola za Marekani $53,000) ili waweze kuwaachilia huru watoto wao, lakini kamwe hawana uwezo wa kukusanya kiasi hicho.

Wanafunzi waliotekwa walikuwa wakifanya mtihani wao wa kumaliza elimu yao ya msingi. Kwa sababu ya mlipuko wa gonjwa la Korona, wanafunzi wanaomaliza shule pekee ndio waliruhusiwa kurudi shuleni.

Serikali kuu na ile ya jimbo la Kaduna zimebaki kimya  kuhusu majaaliwa ya wanafunzi hao waliotekwa pamoja ma mwalimu wao.

‘Ni Siku Ya Kawaida Nchini Nigeria’

Mtumiaji wa Twitter, Ndi Kato alisema tukio hili ni la kufadhaisha Taifa:

Lakini bado ni “siku ya kawaida Naijeria” alilalama mtumiaji wa Twitter,  Chima Chigozie:

Jaja anazilaumu siasa kwa kusababisha umma kukosa huruma na hasira dhidi ya utekaji huu wa wanafunzi:

Goodluck Ebele Jonathan (GEJ) alikuwa Rais, wakati wasichana 276 kutoka katika shule ya serikali walipotekwa na wanamgambo wa  Boko Haram, kutoka Kaskazini Mashariki mwa mji wa Chiboko mnapo mwezi Aprili 2014. Utekaji huu ulisababisha kuwepo kwa mchakato ulioenea dunia nzima kukiwepo na hashtagi ya #WarudisheniMabintiZetu iliyoitikiwa na mamilioni ya watu mitandaoni.

Pia Februari 19, 2018, Boko Haram waliwateka wanafunzi wa kike 110 kutoka katika shule ya wasichana ya sayansi na ufundi huko Dapchi, jimbo la Yobe, Kaskazini Mashariki mwa Naijeria.

Utekaji wa wanafunzi wa Damba-Kasaya na mwalimu wao ni tukio la kutisha lililojirudia.

Tofauti pekee ni kwamba kwa sasa wale ambao wanahusika na tukio hili la kutisha sio Boko Haram bali ni maharamia wenye silaha.

Ukatili wa Maharamia wa Kaduna

Vurugu za kiharamia zililipuka Kaskazini Mashariki mwa Naijeria katika majimbo ya Zamfara, Kaduna, Niger, Sokoto, Kebbi na Katsina.

ACAPS ni shirika huru linaloshughulika na masuala ya kibinadamu, lilithibitisha kwamba vurugu hizi “hazihusiani na uasi wa Boko Haram huko Kaskazini Mashariki”:

The banditry violence began as a farmer/herder conflict in 2011 and intensified between 2017 to 2018 to include cattle rustling, kidnapping for ransom, sexual violence and killings. By March 2020, more than 210,000 people have been internally displaced.

Vurugu hizi za kiharamia zilianza kama mgogoro baina ya wafugaji na wakulima mwaka 2011 na kukua zaidi kati ya mwaka 2017 na 2018 zikihusisha wizi wa mifugo, utekaji kwa ajili ya kujipatia fedha, ubakaji na mauaji. Mpaka mwezi Machi 2020 zaidi ya watu 210,000 wamekuwa wakimbizi wa ndani.

Jamii za vijijini zimebaki kuishi kwa hisani ya maharamia ambapo kati ya Januari na Juni mwaka huu wameshauawa watu wapatao 1,126 kutoka Kaskazini mwa Naijeria.

Vijiji vya Kusini mwa Kaduna ndivyo vinavyoshambuliwa zaidi ambapo wameshauawa watu 366 katika nusu ya kwanza ya mwaka 2020, lilisema Shirika la Kimataifa la Haki za Binadamu.

Chikun LGA, nyumba ya wanafunzi waliotekwa imekuwa ikikumbana na mashambulizi kutoka katika vikundi vya wanamgambo ambayo yameambatana na utekaji na vifo pamoja na “ jamii 45 kukimbia makazi yao ambapo yaliporwa tangu mwaka 2019,” kulingana na taarifa ya muungano wa watu wa Kusini mwa Kaduna.

Watu wa Kusini mwa Kaduna wanadai kuwa maharamia hao ni wafugaji wa kabila la Fulani ambao wana mkakati wa kupora ardhi, wakisaidiwa na kutokuchukuliwa kwa hatua na serikali kuu na ile ya jimbo.

Lakini gavana wa jimbo la Kaduna,  Nasir El-Rufai alikataa uharamia huo kuhusishwa na mpango wa kupora ardhi au kuchochewa na itikadi za kidini.

Agosti 22, serikali ya jimbo la Kaduna iliamuru watu kutokutoka ndani kuanzia saa 12 jioni  mpaka saa 12 asubuhi, ambapo katika baadhi ya maeneo inasadikika kuwa ni sehemu ya mkakati wa  serikali kukomesha uharamia.

Hata hivyo, msemaji wa Umoja wa watu wa Kaduna Kusini, Luka Binniyat, alilalamika kwamba “njaa pia inatuua kwa sababu watu hawaendi mashambani mwao, watu wetu wamekosa tumaini kabisa.”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.