Waandishi Wa Habari wa Msumbiji Waachiwa Huru Baada ya Kukaa Kizuizini Kwa Miezi Kadhaa Bila Kufunguliwa Mashtaka

Mwandishi wa Habari  Amade Abubacar. Picha na:  caiccajuda/Youtube.

Waandishi wa Habari Amade Abubacar na  Germano Adriano, ambao waliokamatwa mapema mwaka huu wakati wakikusanya habari za mgogoro wa kijeshi  katika ukanda wa Kaskazini mwa Msumbiji, wameachiliwa huru bila kushtakiwa mnamo tarehe 23 April,  2019.

Amade, ambaye amekuwa akichangia habari katika vyanzo mbali mbali vya habari vikiwamo Zitamar News na A Carta, aliwekwa kizuizini tarehe 5 Januari wakati akifanya mahojiano na wakimbizi wa ndani kutoka katika wilaya ya Macomia katika jimbo la Kaskazini mwa nchi, Cabo Delgado. Germano, ambaye ni mwandishi wa habari wa kituo cha redio ya jamii cha Nacedje, alipotea tangu Februari 6 na alipatikana akiwa kizuizini tarehe 18, Februari.

Kulingana na taarifa kutoka kwa Shirikisho la Vyombo Vya Habari Kusini Mwa Afrika(MISA), Amade na Germano walishtakiwa kwa “kueneza habari za kuwachafua baadhi ya viongozi wa Jeshi la Wananchi wa Msumbiji kupitia kurasa zao za Facebook ambapo walitangaza kuanza kwa mapigano yaliyotokea katika vijiji vya wilaya ya Macomia.”

Wanahabari hao waliachiliwa huru kutoka katika gereza la  Mieze huko Pemba, makao makuu ya Cabo Delgado na wapo katika kipindi cha uangalizi wakati wakisubiri kushtakiwa katika mahakama ya hakimu mkazi huko Cabo Delgado. Kesi imepangwa kusikilizwa kwa mara ya kwanza hapo Mei 17.

Tangu mwaka 2017, makundi ya watu wenye silaha kama vile visu wamekuwa wakifanya mashambulizi katika vijiji vya Cabo Delgado, wakichoma nyumba  na kuwachinja wakazi. Zaidi ya watu 90 wameshauwa tangu kuanza kwa mashambulio hayo kulingana na taarifa za polisi. Mpaka leo hakuna kikundi ambacho kimejitokeza hadharani kukiri kuhusika na mashambulio hayo.

Hapo Disemba 2018 gazeti la  A Carta de Moçambique lilidhihirisha uwepo wa ukurasa wa Facebook, yenye jina ambalo inaonekana ni la kughushi ambapo ukurasa huo unasifu mashambulio ya vikundi vya watu wenye silaha huko Cabo Delgado

Haifahamiki kama mashtaka dhidi ya Amade na Germano yanahusishwa na ukurasa huo. Timu ya utetezi wa wanahabari hao inasema kuwa hakuna uhusiano wowote baina yao na ukurasa huo au vitendo vingine vya uhalifu vinavyofanyika katika kurasa za Facebook.

Mashtaka dhidi ya wanahabari hawa yamegubikwa na sintofahamu nyingi. Baada ya Amade kuwekwa kizuizini, polisi walimweka chini ya ulinzi wa Jeshi la Wananchi. Aliwekwa katika gereza la Kijeshi ambapo alikaa siku 12 bila kufanya mawasiliano yoyote na kisha kuhamishiwa katika gereza la kiraia.

Wanahabari hawa walishtakiwa tu ilipofika tarehe 16 Aprili, ikiwa ni ukiukwaji wa utaratibu wa mwisho wa siku 90, kinyume na sheria ya ukamataji na kuwekwa kizuizini ya Msumbiji, katika kesi ya Abubacar.

Katika muendelezo wa kesi katika kipindi chao cha kuwa kizuizini wandishi wote kwa pamoja walituhumiwa kwa makosa ya “uhalifu wa kuvujisha siri za serikali kupitia mitandao ya kijamii na kuchochea jamii kwa kutumia njia za kidigitali.”  Mashtaka haya yanapishana na mashtaka ya awali yaliyotolewa dhidi yao, ambapo MISA waliyatafsiri kama ” kueneza ujumbe wa kuchafua baadhi ya viongozi wa jeshi la wananchi wa Msumbiji kupitia ukurasa wa Facebook ambao ulingaza mashambulio ya watu katika vijiji vya wilaya ya Macomia.”

Katika kipindi cha siku 106 alizokaa gerezani, Abubacar alikumbana na ukosefu wa chakula na kunyimwa huduma za matibabu, kulingana na taarifa ya Shirika la Haki za Binadamu (Amnesty International). Familia yake  waliliambia gazeti la @Verdade kwamba walizuiwa kumtembelea  Abubacar katika kipindi chote alichokuwa kizuizini.

Kilichotokea kwa waandishi hawa wa habari ni sehemu ya muendelezo  wa unyanyaswaji dhidi ya wafanyakazi wa vyombo vya habari Kaskazini mwa Msumbiji. Mwandishi wa Habari za Uchunguzi wa kujitegemea Estácio Valoi aliwekwa kizuizini  mwezi Disemba 2018,  pia huko Cabo Delgado kwa sababu za kisheria zisizoeleweka. Baadaye aliachiliwa huru bila mashtaka, lakini vifaa vyake vya kufanyia kazi vilibaki mikononi mwa jeshi.

Wito wa Haki

Cídia Chissungo, ambaye ni mwanaharakati na mhamasishaji wa kampeni ya #AmedeAwekweHuru alisherehekea taarifa hizo kwa kusema:

Angela Quintal, msimamizi wa  Mradi wa Kamati ya Kuwalinda Wanahabari (CPJ), ukanda wa Afrika alisema:

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.