- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Serikali ya Zimbabwe yaendelea kutumia habari za mtandaoni kama silaha ya kukandamiza haki za raia

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Zimbabwe, Haki za Binadamu, Maandamano, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza, Vyombo na Uandishi wa Habari, GV Utetezi
[1]

Waandamanaji wakishinikiza kuondolewa kwa aliyekuwa rais Robert Mugabe (ambaye sasa ni marehemu) kutoka madarakani mnamo Novemba 18, 2017. Picha na mtumiaji wa Flickr Zimbabwean-eyes (Huru kutumika).

Mapema asubuhi ya Novemba 15, 2017, raia wa Zimbabwe waliamka na habari zilizoenea kwamba aliyekuwa mbabe, marehemu Robert Mugabe, alikuwa ameng’olewa madarakani katika mapinduzi ya serikali, na alikuwa nguvuni kwenye makazi yake, Ikulu, pamoja na familia yake.

Meja Jenerali Sibusiso Moyo, ambaye kwa sasa ni waziri wa mambo ya nje, alitangaza [2] kwenye runinga ya taifa kuwa rais huyo alikuwa salama chini ya ulinzi wa serikali na kwamba “hali ya mambo iko katika ngazi nyingine.”

Mara tu baada ya tangazo hilo la Jenerali Moyo, raia wa Zimbabwe walimiminika kwa msisimko mkubwa kwenye mitandao ya kijamii – hasa WhatsApp, Twitter na Facebook – ili kupata taarifa mpya kuhusu hali hiyo. Kwa mara ya kwanza, umaarufu mpya wa mitandao ya kijamii kuwezesha kupata habari na kuhamasisha maandamano ulimea mizizi miongoni mwa raia wa Zimbabwe, wakati waandamanaji walipoingia mitaani [3] na kusaidia kushinikiza kuondolewa kwa Mugabe madarakani.

Serikali mpya, iliyoongozwa na Emmerson Dambudzo Mnangagwa,iling’amua mara nguvu ya  mitandao ya kijamii. Kama waziri wa zamani wa usalama wa nchi, Mnangagwa pia alitambua umuhimu na nafasi ya  upotoshaji taarifa katika nyanja za kisiasa za Zimbabwe.

Mnamo mwezi Machi, 2018, kwa kutambua mara na ili kujitwalia mamlaka ya kisiasa yaliyojianika mbele yake na ili kuhakikisha ushindi katika uchaguzi wa rais na wabunge katika mwaka uliofuatia, Mnangagwa aliamuru [4] umoja wa vijana wa chama tawala cha  ZANU PF (Zimbabwe National Union-Patriotic Front) “kujimwaga katika mitandao ya kijamii na mtandaoni na kuwachafua na kuwashambulia wapinzani”.

Katika Zimbabwe baada ya Mugabe, mpango wake huu umeimarisha mgogoro wa upotoshaji na utoaji taarifa zisizo za kweli, na hivyo kuwaacha Wazimbabwe na vyanzo vichache tu vya kuaminika vya kupata habari na kujua kuhusu yanayoendelea katika kipindi cha mpito na maandamano ya kupinga serikali.

Wakati ambapo serikali mpya ilijidai kulaani [5] “habari za uongo”  kwa taarifa zilizosambazwa kwenye mitandao ya kijamii na ambazo waliziona kuwa tishio utawala ulio madarakani,  pia ilifanya hila ilikuupotosha [6] umma kuhusu namna ilivyoshughulika na maandamano ya kuipinga serikali.

Kero ya uhuru wa kujieleza mtandaoni

Zimbabwe imeshuhudia ongezeko kubwa la matumizi ya intaneti kwenye simu za mkononi na mitandao ya kijamii katika miaka michache iliyopita. Kiwango cha kuenea kwa intaneti kiliongezeka [7] kwa asilimia 41.1, kutoka asilimia 11 ya idadi ya watu hadi asilimia 52.1 kati ya 2010 na 2018, wakati kuenea kwa simu za mkononi kuliongezeka kwa asilimia 43.8 kutoka asilimia 58.8 hadi asilimia 102.7 kwa kipindi hicho hicho. Hii inamaanisha kuwa nusu ya idadi ya watu sasa imeunganishwa na intaneti, ikilinganishwa na asilimia 11 tu katika mwaka 2010.

Hata hivyo, upotoshaji na utoaji taarifa za uongo nao vimepata mazingira ya kushamiri kwa sababu kadhaa: mgawanyiko mkubwa katika vyombo vya habari, mapendekezo ya serikali kudhibiti [8] mitandao ya kijamii, njia hafifu za mawasiliano rasmi na na elimu duni miongoni mwa watumiaji wa intaneti.

Wakati wa maandamano dhidi ya serikali ya Januari 2019, kipindi vikosi vya usalama vya serikali vilipowakamata [9] na kuwashambulia mamia ya waandamanaji [10], habari za ukandamizaji huu zilishindana na madai ya serikali kwamba zilikuwa “habari za uongo” au pale ilipokanusha kabisa kuwepo kwake.  Serikali ilizuia [11] upatikanaji wa huduma za intaneti ili kuvuruga mtiririko wa habari na hivyo kuleta mkanganyiko mkubwa. Viongozi wa serikali na wafuasi wao pia walitumia mbinu ya kupotosha taarifa kuhusu maandamano hayo na kupenyeza mashaka katika taarifa zozote zilizokuwa za weli kwa kuzipachika jina la “habari za uongo”.

Kwa kawaida, nchini Zimbabwe,  raia huzichukulia taarifa zozote zitolewazo na mawaziri wa serikali kama ndio sahihi. Kwa mfano, Naibu Waziri wa Habari Energy Mutodi alijitokeza kuwashawishi [12] watu kuwa kila kitu kilikuwa shwari na kwamba video na picha za wanajeshi waliokuwa wakipiga doria mitaani zilitengenezwa na “wahuni wachache.” Mutodi alizidi kupotosha taifa pale alipodai [6] kwenye runinga ya taifa kwamba hakukuwepo na uzimwaji wa intaneti bali kulikuwa na “msongamano” katika mtandao.

Katika kisa kingine kinachoshukiwa kuwa ni upotoshaji habari unaoungwa mkono na serikali, mamilioni wa watu walizimiwa mitandao ya kijamii wakati wa maandamano ya Januari. Wengine walipakua zana za  huduma ya kubaki hewani kwa ushirika inayojulikana kama Virtual Private Network (VPN) ili kuendelea kuhabarika, hata hivyo taarifa ilisambazwa [13] kwamba kupakua zana kama hizo kungesababisha kukamatwa, hali iliyozidi kusababisha hofu na taharuki.

Mwezi Machi 2019, wakati Shirika la Haki za Kibinadamu (HRW) lilichapisha kwa twiti ripoti iliyolaani matumizi ya “ukatili wa kutisha” wa serikali kudhibiti maandamano ya Januari 2019, wafuasi wa serikali walitumia Twita kulichafua na kulishambulia shirika hilo la HRW.

Mtumiaji mmoja alituma ujumbe [14] wa twita kuwa shirika hilo lilikuwa ”linaeneza uongo wa waziwazi” na kuliita kuwa lilikuwa”shirika la ukoloni mamboleo … lililopewa kazi ya kuzishinikiza nchi zisizo na hatia ili zitetee malengo ya kibeberu Marekani.” Mwingine alirejelea madai [15] ya serikali na kulalama kuwa vurugu hizo zilitokana na “wahuni ambao walikuwa wanajaribu [sic] kumchafulia rais “.

Na upotoshaji kuhusu sera za serikali na matukio mengine yenye maslahi ya umma zimeendelea kukithiri baada ya maandamano ya Januari.

Hivi karibuni, wanachama wa chama tawala cha ZANU PF walitumia mtandao wa Twita kuupotosha umma kuhusu kutoweka kwa Dk. Peter Magombey, ambaye ni kaimu Rais wa Chama cha Madaktari wa Hospitali za Zimbabwe (ZHDA). Alitekwa [16] nyara Septemba 14, 2019, kufuatia kutangazwa kwa mgomo katika sekta ya afya. Katibu wa ZANU PF wa masuala ya vijana alimuelezea [17] Magombey kuwa mtu ”mpumbavu” na “mwenye kuidhalalisha taaluma hiyo.” Akaunti yenye jina la ZANU PF Patriots ilisema [18] kuwa taarifa za kutekwa kwake zilikuwa za “uongo”. Wengine walisambaza madai ya uongo kwamba madaktari “waliwauwa wagonjwa wengi [19]” kufuatia mgomo huo, ikiwemo zaidi ya watu 500 [20] katika hospitali moja.

Kizungumkuti cha historia ya Zimbabwe

Udhibiti wa vyombo vya habari nchini Zimbabwe una chimbuko katika sera za kikoloni za karne ya 20, ambao ulitiwa doa kwa matumizi ya nguvu ili kunyong’onyeza mbele ya mamlaka za kisiasa. Serikali ya Rhodhesia iliyoongozwa na Ian Smith [21] ilijikita katika propaganda na kudhibiti habari kama silaha yake bora zaidi, sio tu kuunga uhalali wa serikali hiyo bali pia kueneza taarifa potovu kuhusu vita.

Serikali ya kikoloni ilipitisha idadi kubwa ya sheria za kukandamiza kujieleza au kupinga sera za kibaguzi za Smith na ilitekeleza sheria hizi kwa ukatili mno kuwalenga viongozi wa ukombozi. Udhibiti wa habari ilikuwa hali ya kawaida kabla ya uhuru mwaka wa 1980, na hali hii iliweka mfano wa serikali katika suala la sera za mawasiliano na usimamizi wa vyombo vya habari kwa miaka mingi iliyofuatia.

Kama alivyoandika mwanahabari na mwandishi wa Afrika Kusini mashuhuri, marehemu Heidi Holland, katika kitabu chake, “Dinner with Mugabe: The Untold Story of a Freedom Fighter Who Became a Tyrant”: [22]

So many in ZANU PF's hierarchy have lived with similar appalling violence woven into everyday life as if it were normal. The bush war, or Second Chimurenga [23], has never really ended in Zimbabwe.

Watu wengi katika hiyarakia ya ZANU PF wameishi katika ukatili uliofumwa katika maisha yao ya kila siku kiasi cha kuonekana ni kama  jambo la kawaida. Vita vya msituni, au vita vya Pili vya Chimurenga [23], havijawahi kumalizika kabisa nchini Zimbabwe.

Leo hii, Mnangagwa anaendeleza urithi huu, kukandamiza sauti za wakosoaji kupitia mbinu za taarifa potovu mtandaoni na uzimaji wa mtandao.


Makala haya ni sehemu ya mfululizo wa machapisho yanayochunguza kuingiliwa kwa haki za dijitali kupitia mbinu kama vile ufungwaji wa mtandao wa intaneti na upotoshaji habari wakati wa matukio muhimu ya kisiasa katika nchi saba za Afrika: Algeria, Ethiopia, Msumbiji, Nigeria, Tunisia, Uganda, na Zimbabwe. Mradi huu unafadhiliwa na Mfuko wa  Africa Digital Rights Fund [24]wa The Collaboration on International ICT Policy for East and Southern Africa [25] (CIPESA).