- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Papa Francis Kutembelea Msumbiji Mwezi Septemba, Kipindi cha Kampeni ya Uchaguzi Mkuu

Mada za Habari: Msumbiji, Dini, Habari Njema, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uchaguzi
Papa Francisco | maelezo na ShareAlike ya 2.0 (CC BY-SA 2.0) [1]

Papa Francisco | Gabriel Trujillo – maelezo na ShareAlike ya 2.0(CC BY-SA 2.0)

Papa Francis atatembelea Msumbiji Mwezi Septemba 2019, wiki kadhaa kabla ya uchaguzi ambao utamchagua Rais mpya, Wabunge na Magavana wa majimbo.

Papa amealikwa na Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi mwezi Septemba 2018. Matembezi hayo yalitangazwa na kuthibitishwa tarehe 26 Machi katika hafla ya ibada iliyojumuisha viongozi wa kanisa la Roma Katoliki katika nchi hiyo.

Rais Nyusi alisema matembezi ya Papa yataimarisha mazungumzo ya amani na RENAMO ambacho ni chama cha upinzani kilichosimamisha mapigano ya kijeshi na serikali mwaka 2017 kama sehemu ya mchakato wa kutafuta amani ambao bado umejaa wasiwasi. Aliongeza kwamba itakuwa pia ni muda wa kufanya tathmini juu ya mgogoro na makundi ya wanamgambo [2] waliopo hasa katika jimbo la Cabo Delgado kaskazini mwa nchi.

John Paul II alikuwa ni Papa wa mwisho kutembelea Msumbiji mwezi Septemba 1988.

Uthibitisho wa matembezi ya papa ulikuwa tayari umetegemewa katikati ya mwezi wa Februari. Msumbiji itakuwa na uchaguzi mkuu mwezi Oktoba [3] ingawa haijapata ahueni kutokana na kimbunga cha Idai [4], ambacho kilisababisha vifo vya zaidi ya watu 500 na wengine zaidi ya milioni kukosa makazi ya kuishi. Papa ameonesha mshikamano na waathirika:

Nina maumivu na ninaungana na wapendwa wananchi wa Msumbiji, Zimbabwe na Malawi walioathirika na kimbunga cha Idai. Ninawakabidhi katika rehema za Mungu wote walioathiriwa pamoja na familia zao.

Balaa lilisababishwa na mojawapo ya vimbunga vibaya sana vilivyowahi kupiga katika eneo la kusini, lilipiga mji wa Beira katikati ya Msumbiji tarehe 14, Machi na halafu katika nchi jirani za Zimbabwe na Malawi. Zaidi ya watu 300 walikufa katika nchi hizi mbili.

Tangu balaa hilo, nchi ipo katika hali ya hatari ambalo limeifanya serikali kupitia tena kalenda ya uchaguzi na kuahirisha muda wa uandikishaji wa wapiga kura.

Ukweli ni kwamba uchaguzi kufanyika baada tu ya kutembelewa na Papa kumeibua maswali kutoka kwa wananchi ambao wanaona kuwa kutakuwa na athari katika mchakato wa kupiga kampeni:

Ni wazi kuwa ujio wa Papa Francis mwezi Septemba unampendelea Filipe Nyusi na Frelimo. Matembezi yake yanaweza kumfaidisha kisiasa moja kwa moja au la. Ingekuwa vizuri kama ungeahirishwa hadi mwezi Novemba baadala ya mkanganyiko wa uchaguzi mkuu ulipangwa tarehe 15 Oktoba.