Kwa nini Cuba Iliamua Kuwaondoa Madaktari Wao 8,000 Kutoka Nchini Brazili

Kulingana na serikali ya Cuba, madaktari wapatao 20,000 waliwahudumia Wabrazili milioni 113 kwa kipindi cha miaka mitano. Picha na: Agência Brasil, CC BY 3.0

Maelfu ya Wabrazili wanaweza kubaki bila huduma za afya kwa sababu Cuba imeanza kuwaondoa zaidi ya madaktari 8,400 ambao walikuwa wamepangiwa kazi katika miji midogo ya mbali na ya ndani sana ya nchi kwa miaka mitano.

Katika taarifa ya rasmi ya Novemba 14, Havana ilitangaza kuwa itakatiza makubaliano yake na Brazili kutokana na maoni ya wazi ya Rais Jair Bolsonaro kuhusu mpango huo ambapo wanadhani kuwa yanaonesha “vitisho na uonevu.”. Mara kadhaa katika kampeni za Urais, Bolsonaro alikosoa utandaji wa madaktari kutoka Cuba na kuukosoa mpango huo.

Mpango huo ulizinduliwa mwaka 2013 na rais wa zamani Dilma Rousseff, ukiwa na jina “Mais Médicos” (Madaktari zaidi) ukiwa na lengo la kupanua upatikanaji wa huduma za afya katika maeneo duni zaidi nchini Brazili ambapo baadhi yake hayajawahi kuwa na mganga mkazi. Ilifungua mlango wa ajira katika maeneo hayo ikitoa mshahara wa karibu dola 3,500 kwa mwezi pamoja na posho kwa ajili nyumba na chakula (ukilinganisha na kima cha chini cha mshahara wa Brazili ambapo ni chini ya dola 300 kwa mwezi)

Mpango huo ulitoa upendeleo kwa madaktari wa Brazili lakini baada ya kuajiriwa kwa asilimia sita tu ya ajira zilizokuwepo, nafasi nyingine zilijazwa na madaktari wa Cuba ambao waliletwa kwa mkataba uliosainiwa na Wizara ya Afya ya Brazili na Havana kwa usimamizi wa shirika la afya duniani chini ya taasisi yake ya Pan American Health Organisation. Kwa makubaliano ya mkataba huo, Brazili haiwaajiri madaktari wa Cuba moja kwa moja badala yake inailipa serikali ya Cuba ambayo iliwapa mafunzo, kuwaongoza na kuwafidia madaktari hao kama watumishi wa umma kwa mshahara wa asilimia 25 ya kile Brazili ingewalipa kama ingewaajiri wenyewe.

Madaktari wa Cuba wakiwahudumia Wabrazili wenye hali mbaya kabisa…hawa ndio watu Bolsonaro aliowafukuza kwa tamko lake la kikatili. Picha na Araquém Alcântara

Mpango huo ulikumbana na ukosoaji mwingi tangu walipofika madaktari wa awali. Walizomewa katika viwanja vya ndege na umati wa watu na waliitwa “watumwa” katika maandamano yaliyoongozwa na chama cha Madaktari wa Brazili.

Bolsonaro mwenyewe wakati akiwa mbunge katika chemba ya Wasaidizi, alikwenda Mahakama Kuu akitaka mpango huo usitishwe. Katika nyakati zote mbili kama mbunge na katika kampeni zake za uraisi alirudia kusema kuwa mpango huo “ulikuwa kazi ya utumwa”. Aliahidi kuwarudisha madaktari Cuba kwa “mkwaju wa kalamu” wakawasaidie “wanachama wa chama cha wafanyakazi ambao watapelekwa huko Guantanamo hivi karibuni”. Katika mahojianio kwenye Tv hapo Julai 2018, alisema kuwa “hakuna mtu mwenye ushahidi kuwa [madaktari wa Cuba] wana ujuzi wa utabibu”.

Katika taarifa yake rasmi ya kujitoa, Havana ilisema:

El pueblo brasileño, que hizo del Programa Más Médicos una conquista social, que confió desde el primer momento en los médicos cubanos, aprecia sus virtudes y agradece el respeto, sensibilidad y profesionalidad con que le atendieron, podrá comprender sobre quién cae la responsabilidad de que nuestros médicos no puedan continuar prestando su aporte solidario en ese país.

Watu wa Brazili walioufanya mpango wa “Madaktari Zaidi” kufanikiwa, waliowaamini madaktari wa Cuba tangu awali, waliothamini na kuiheshimu huduma hii nyeti na ya kitaalamu wataelewa ni nani anawajibika kwa madaktari wetu kushindwa kuendelea kutoa huduma kwao.

Bolsonaro alijibu katika mitandao yake ya kijamii kuwa Havana haikutaka kufuata masharti mapya: hawakutaka mshahara wote wapewe madaktari na Diploma zao za udaktari kuhakikiwa nchini Brazili kupitia mitihani. Aliuita uamuzi wa Cuba kuwa “uamuzi usio wa kuiajibikaji wa dikteta wa Cuba” kwa kutokujali madhara yatakayotokea katika maisha ya Wabrazili.

Kama mwanahabari Leonardo Sakamoto alivyoandika, hili litaleta “mgogoro wa kwanza wa kijamii katika utawala wa Bolsonaro” na hili lilijionesha hata kabla hajachukua ofisi.

Cuba hutengeneza asilimia 45 ya watu wenye taaluma ya utabibu. Karibu asilimia 28 ya miji ya Brazili huudumuwa na mpango ambapo kuna mganga mkazi mmoja tu wa Cuba. Karibu asilimia 90 ya madaktari wanaofanya kazi katika maeneo ya vijijini huko Brazili ni Wacuba.

Matatizo ya Brazili, suluhu kwa Cuba.

Miaka mitano iliyipita, Brazili ilikuwa na upungufu wa madaktari 54,000 katika hospitali zake za umma. Nchi ilikuwa na daktari 1,8 kwa wakazi 1000. Kwa kulinganisha na wastani wa sasa wa 2,5 kwa Marekani na 7,5 kwa Cuba.

Miji midogo ya Brazili imekuwa ikipambana kuwavutia watu wenye taaluma ya utabibu, ambao hulalamika kuhusu ukosefu wa miundo mbinu. Pia Brazil haisomeshi madaktari wa kutosha kuhudumia idadi wa watu Milioni 200.

Kwa upande mwingine, Taifa dogo la kisoshalisti lina daktari wa kutosha. Kwa sasa Cuba ina madaktari elfu 50,000 waliosambazwa katika nchi 67. Kukodisha madaktari ndio biashara kubwa ya Cuba: hutengeneza  dola za Marekani bilioni 11 katika pato la Taifa kwa mwaka, ni zaidi ya unavyofanya utalii.

Madaktari wa Cuba wakiwasili nchini Brazili mwaka 2013. Picha na Valter Campanato/Agência Brasil, CC BY 3.0

Cuba ilituma nje kikosi chake cha kwanza cha madaktari mwaka 1963, baada ya vita vya uhuru uko Algeria. Kuanzia hapo, kupitia simulizi za Radio Ambulante, karibu matabibu 500,000 wa Cuba wameshafanya kazi Afrika, Asia na Marekani.

Baada ya miaka mingi, Wacuba wachache wameweza kuviambia vyombo vya habari vya Brazili kuwa walijisikia “kunyonywa”. Baadhi yao wamefungua mashtaka dhidi ya serikali na WHO. Wengine wametoa taarifa za vitisho kutoka katika serikali yao. Hata hivyo, wengi wamesema katika  mahojiano na Radio Ambulante kuwa, pamoja na Havana kuchukua asilimia 75 ya mishahara yao, hawaoni kama mshahara huo haukuwa wa haki.

Matokeo

Utafiti uliofanywa na Chuo cha Federal cha Minas Gerais, ambapo waliohojiwa wagonjwa elfu 14 katika miji 700 mwaka mmoja baada ya mpango wa “Madaktari Zaidi” kuanza ilionyesha kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na mpango huo ambapo, asilimia 85 walisema kuwa huduma za afya katika miji yao ilikuwa “nzuri” au “nzuri sana”. Washiriki walionesha upungufu wa miundombinu na ukosefu wa dawa kama matatizo ambayo bado hayajapata ufumbuzi.

Utafiti mwingine kutoka Fundação Getúlio Vargas (FGV) unaonesha kuwa mpango huu uliiwezesha serikali kupunguza theluthi ya matumizi yake ya watu kulazwa Hospitali. Débora Mazetto, mmoja ya wachumi walioongoza utafiti huo aliiambia BBC Brazil:

Houve uma melhora na qualidade do atendimento à população. Imagine uma comunidade que não tinha médicos? Com o aumento das consultas em áreas desassistidas, foi possível identificar e tratar doenças com agilidade, evitando internações que poderiam ser de fato evitáveis

Kumekuwa na maboresho ya huduma zinazotolewa kwa jamii. Je unaweza kuifikiria jamii ambayo haijawahi kuwa na daktari kabisa? Kuongezeka kwa waajiriwa katika maeneo ambayo yalikuwa yametelekezwa kwanza, imekuwa rahisi kugundua magonjwa na kuyatibu haraka na kuepuka kulazwa kusipo na sababu.

Ni nini kitafuata?

Tangu Novemba 14, zaidi ya madaktari 200 wamesharudi Cuba. Ifikapo Disemba 12, Wataalamu wote wa Taasisi ya Pan American Health Organization watakuwa wamesharudi.

Katika kliniki nyingi za umma, watu wamejikuta wapo wenyewe bila msaada wa kitabibu  kwa wiki nzima iliyopita au waliambiwa daktari atakuwepo kwa wiki mara moja kuanzia sasa. Ingawa serikali ya Brazili inadai kuwa asilimia 92 ya nafasi zilizoachwa wazi na Wacuba zimeshazibwa, gazeti la Folha de S. Paulo lilisema kuwa mwisho wa siku, namba hiyo inaweza isimaanishe chochote:

Em 2017, o Ministério da Saúde abriu concurso para selecionar brasileiros para o Mais Médicos. Ao todo, 6.285 se inscreveram para 2.320 vagas, mas só 1.626 apareceram para trabalhar. Cerca de 30% deixaram seus postos antes de um ano de serviço.

Mwaka 2017, Wizara ya Afya ilifungua mlango wa kuchaguwa waBrazili kwa ajili ya mpango wa Madaktari Zaidi. Kwa ujumla watu 6,285 waliomba kazi katika nafasi 2,320 zilizokuwepo lakini ni 1,626 ndio walioripoti katika vituo vyao. Karibu asilimia 30 waliacha kazi kabla ya kumaliza mwaka mmoja katika nafasi zao.

Kama mipango mingi ya kijamii ilivyo nchini Brazili, Madaktari Zaidi ulikuwa na kasoro zake lakini pia ilibadilisha haraka huduma za afya kwa umma katika maeneo ambayo yalikuwa yamesahauliwa kabisa na serikali ya Brazili. Labda changamoto kubwa ambayo serikali ijayo inapaswa ijifunze wapi ilikosea na pale ilipofanya sawa. Ni kwa namna gani, na ikiwa serikali ya Bolsonaro itahakikisha huduma za afya katika maeneo hayo zinapatikana na zinaonekana.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.