- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Polisi wa Nigeria Wamkamata Mwandishi wa Habari na Kaka Yake kwa Makala ya Gazeti Ambayo Hata Hivyo Hawakuiandika

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Naijeria, Haki za Binadamu, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza, Vyombo na Uandishi wa Habari, GV Utetezi
[1]

Maafisa wa polisi wa Naijeria waliomaliza mafunzo yao mwaka 2015. Picha na AMISOM, imeachiliwa kwa matumizi ya umma.

Daniel Elombah ni mchapishaji wa  elombah.com [2]. Kulingana na Premium Times [3], akina Elombah walikamatwa nyumbani kwao Nnewi, huko kusini Mashariki mwa Naijeria:

Daniel Elombah alikamatwa mnamo saa 10:30 alfajiri nyumbani kwake huko Nnewi siku ya mwaka mpya kulingana na taarifa za kaka yake Paul. Alisema walipokea taarifa kutoka kwa maafisa waliomkamata kaka yake kuwa alikamatwa kwa sababu ya makala ya hivi karibuni ambayo wanadhani ilimzungumzia vibaya Kamanda Mkuu wa Polisi Inspekta Ibrahim Idris. Kaka yake alisema kuwa, awali Bwana Elombah alipelekwa kwenye kizuizi cha SARS huko Anambra lakini baadaye alihamishiwa huku Abuja muda wa saa moja asubuhi.

Daniel Elombah aliiambia Kamati ya Kuwalinda Wanahabari [4] kuwa polisi walisema kuwa makala iliyochapishwa na Opinion Nigeria ndiyo chanzo cha kukamatwa kwake. Makala hiyo iliyochapishwa hapo Disemba 22, 2017 na Opinion Nigeria [5] ambayo haikuandikwa na yeyote kati ya ndugu hao, ilionesha kuwa Inspekta Mkuu wa Polisi alihusika na “mambo mengi tata yasiyoisha.”

Katika mahojiano na Daily Post [6], Inspekta mkuu Ibrahim Idris alipotezea maswali ya moja kwa moja aliyoulizwa kuhusu sababu za kukamatwa kwa Elomba, alisema kirahisi tu kuwa “wakati wowote ukifanya uhalifu ni jukumu letu kuhakikisha kuwa tunawajibika.”

Daniel Elombah, ambaye anaishi Uingereza lakini alikuwa akitembelea familia yake Nigeria wakati wa kukamwatwa kwake, anafahamika kwa habari zake makini dhidi ya Boko Haram na Raisi Buhari.

Daniel Elombah akiwa hospitali. [Picha ziliwekwa Facebook na wakili wa Elomba, ndugu Obunike Ohaegbu]

Mwandishi wa habari wa Naijeria Daniel Elombah na kaka yake Timothy Elombah, walikamatwa na polisi wa Naijeria siku ya mwaka mpya.

Mwanahabari huyo aliachiliwa huru baadaye siku hiyo baada ya kulazwa hospitali [7] huko Abuja. Ingawa hakuna maelezo rasmi yaliyotolewa kuhusu kulazwa kwake, inaonesha mwanahabari huyo alipokea huduma za kitababu baada ya ‘kufungwa pingu kama muhalifu na kusafirishwa kwa basi kupitia barabara mbovu sana kama maili 700 mpaka Abuja.” Wakati wa safari hiyo, ndugu hao wa Elombah “walishambuliwa, walipigwa makofi na ngumi” na polisi wa Naijeria na hii ni kutokana na taarifa kutoka kwa gazeti la Vanguard [8] .

Polisi bado hawajamuachilia kaka yake Timothy. Hapo Januari 2, 2018, Mahakama ya Hakimu ya Abuja [9] ilitoa kibali cha kuendelea kushikiliwa kwa Timothy. “Hii itatuwezesha kufanya uchunguzi wa awali kabla hatujamfungulia shauri la jinai,” alisema msemaji wa polisi.

“Mamlaka za Nigeria lazima zimuachilie huru Timothy Elombah haraka sana na kutupilia mbali masuala ya kisheria yanayoendelea na kumruhusu kaka yake Daniel kurudi nyumbani,” alisema hayo Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kamati ya kutetea Wanahabari ndugu Robert Mahoney, huko New York-Marekani.

Polisi  hawawezi kuvamia nyumba za wanahabari na kuwakamata na kuwaweka kizuizini kwa sababu tu Ofisa hakupenda kitu kilichoandikwa kwenye gazeti. Kwanza haioneshi wazi kama mtu aliyeko kizuizini ana lolote la kufanya na makala wanayodhani ni ya kumkashifu Inspekta wa jeshi.

Daniel Elombah amemshitaki Inspekta Mkuu wa polisi wa Nigeria katika Mahakama kuu huko Abuja kwa kuvunja haki zake msingi. Anataka afidiwe Naira bilioni 2 [10] (karibu dola milioni $5.5) kwa kuwekwa kizuzini kinyume cha sheria. .

Vile vile, mawakili watatu wanaotoka Uingereza walitoa hoja [11] kwa Mbunge wa Uingereza, Lyn Brown, Waziri Mkuu, Theresa May na Waziri wa Mambo ya Nje Boris Johnson kuhusu kukamatwa kwa Daniel Elombah kinyume na sheria.