Eissa Muhamad, kutoka Niger, amesema kuwa amekwama katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole kwa miezi miwili katika eneo la wasafiri kuanzia Novemba 6, 2018. Muhamad mwenye miaka 24, alisafirishwa kutoka Israel ambapo aliishi huko kwa miaka nane kama muhamiaji haramu.
Nilikutana na Muhamad mwezi Disemba 12, 2018 kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole nikiwa eneo la wasafiri Addis Ababa.
Muhamad aliniambia kwa mwaka 2018, ameshasafirishwa mara mbili kutoka Israel. Aliporudi Niger kwa mara ya kwanza, nyaraka zake za kusafiria za Israel bado zilikuwa halali hivyo alikata tiketi nyingine na kurejea Israel. Alipofika Israel, mamlaka walichukua nyaraka zake za kusafiria na kumsafirisha tena kumrudisha nyumbani kwao Niger. Muhamad aliporudi Niger kwa mara ya pili, mamlaka za huko walihitaji uthibitisho wa uraia wake lakini alishindwa kuthibitisha kwa nyaraka halali za Ki-Israel au za Ki-Niger zinazoonesha uraia wake.
Muhamad alibaki mikononi mwa mamlaka za Niger kwa siku nane kabla hajasafirishwa tena kuelekea Israel kupitia Ethiopia kwa ndege ya shirika la ndege la Ethiopia. Alipofika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bole huko Ethiopia, mamlaka za Ethiopia kwa kushirikiana na serikali ya Israel walimzuia kupanda ndege ya kuunganisha kuelekea Israel. Walimwambia kuwa, serikali ya Israel haipo tayari kumpokea na kuanzia hapo amekwama ndani ya uwanja wa ndege na amebaki njia panda kati ya Israel na Niger.
Nilikuwa nalala kwenye viti, wakati mwingine nalala msikitini na sikuoga kwa miezi miwili kwa sababu ndani ya uwanja wa ndege hakuna sehemu ya kuogea, niliosha uso wangu, mikono na miguu pekee.
Muhamad anasema alishajaribu kuwasiliana na ubalozi wa Niger huko Addis Ababa lakini kwa sababu hakuweza kuonyesha nyaraka halali kuthibitisha uraia wake, walishindwa kumsaidia.
Kwa ilivyokuwa mwaka 2018, kwa sasa Israel ina wahamiaji wa Kiafrika 34,000 ambao walichukua safari za hatari wafike Israel kutafuta maisha bora. Lakini Israel inalalamika kuwa wengi wao ni wahamiaji wa kiuchumi ambao wanakwamisha uchumi wa Israel. Kuchagua kubaki inamaanisha kifungo gerezani au chaguo hafifu la makazi.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na chama cha mrengo wa kulia cha Likud wamebaki kuwalenga wale wambao wanahisiwa kuwa “wamejipenyeza.” Utafiti wa Taasisi ya Demokrasia ya Israel unasema kuwa asilimia 66 ya Waisraeli wanaunga mkono utaratibu wa serikali wa kuwarudisha makwao wahamiaji wa Afrika.
Muhamad anadai kuwa alikuwa akiishi Israel kihalali na alikuwa akifanya kazi kwenye kiwanda na anadai kuwa serikali ilimnyang'anya hadhi yake ya kupata makazi na kumtupa nje ya nchi.
Mamlaka za Ethiopia haijamkamata Muhamad na imekuwa ikimpatia chakula kwa kipindi chote alichokaa ndani ya uwanja wa ndege. Kitaalamu, Ethiopia ni moja ya watia saini wa azimio la 1951 kuhusu hadhi ya wakimbizi na Protokali ya 1967 na pia 1969 Azimio la Umoja wa Afrika kuhusu utawala wa mambo ya msingi kuhusu matatizo ya wakimbizi barani Afrika na karibu wakimbizi wote wanaoingia Ethiopia hupewa hifadhi kwa msingi wa prima facie, lakini Muhamad aliniambia kuwa hana mpango wa kuomba hifadhi nchini Ethiopia.
Katika mahojiano ndani ya video hii, Muhamad ananieleza jinsi anavyojisikia baada ya kukwama uwanja wa ndege huku akiwa hajui mustakabali wa maisha yake ya baadaye: