Bundi Agoma Kuondoka kwenye Bunge la Tanzania. Maana yake nini?

Viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma, makao makuu ya Tanzania, lilipo bunge. Picha ya Pernille Bærendtsen, imetumiwa kwa ruhusa.

Mnamo Januari 29, wakati Bunge la Tanzania likiendelea na kikao chake jijini Dodoma, huu ukiwa ni mkutano wake wa kwanza kwa mwaka 2019, bundi alitua kwenye jengo hilo, akijishikiza kwenye paa na kulitazama bunge akiwa kwa juu.

Tukio hili lilivutia hisia za watu wengi nchini humo na kuibua maswali hasa katika mitandao ya kijamii na magazeti. Swali kubwa likiwa: je, kutua kwa bundi kwenye jengo la bunge kulibeba maana yoyote? 

‘’Ishara mbaya?’’ gazeti la kila wiki, The East African, lilipendekeza.

Mwanablogu wa Uingereza na mchambuzi wa vyombo vya habari, Ben Tylor, alidadisi zaidi:

Bundi kuingia bungeni kumeashiria ujio wa kifo cha demokrasia ya Tanzania?

Katuni imechorwa na Samuel Mwamkinga (Joune), imetumiwa kwa ruhusa.

Mchora katuni wa Tanzania, Samuel Mwamkinga (Joune), aliliweka tukio hilo katika mchoro akilifananisha na neno la Kiingereza “kundi la bundi” likibeba maana ya Kigiriki kwamba bundi wana hekima (picha imetumiwa kwa ruhusa).

Bundi, hata hivyo, anaonekana kama ishara ya kifo na mikosi nchini Tanzania. 

Inavyoonekana — bundi huyo alikusudia kukaa Bungeni, kwa mujibu wa gazeti la The Citizen:
 

Bundi, ndege anayependa kuruka usiku, hakuondoka…pamoja na majaribio kadhaa ya maafisa wa bunge kumtoa.

Bundi ni ndege maarufu nchini Tanzania, na si ajabu ndege hawa kuhusishwa na masuala ya ushirikina. Mwaka 2010 utafiti uliwahi kuonesha kuwa asilimia 93 ya wa-Tanzania wanaamini ushirikina.

Kikao kisicho cha kawaida

Kikao hiki cha Bunge, uwepo wa bundi ulikuwa alama isiyo ya kupuuza, hata kwa wasioamini ushirikina

Agenda ya kikao cha kwanza cha Bunge cha mwaka 2019 ilikuwa ni mapendekezo ya marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa, iliyotanguliwa na mjadala mzito ulioendelea kwa takribani mwezi mzima katika mazingira ya kisiasa yanayoonekana kuendelea kuwa tete.

Tanzania iliweka historia mwaka 1992 kuwa miongoni mwa nchi za mwanzo barani Afrika kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa, ulioruhusu kuundwa kwa vyama vya upinzani. Sheria ya Vyama vya Siasa (hapa ikiwa na mabadiliko yanayopendekezwa) ilitungwa mwaka 1992 na imekuwa ikirekebishwa mara kwa mara na mabadiliko ya mwisho kabla ya haya yalifanyika mwaka 2009.

Wakati bundi akiwa ametua kwenye jengo la Bunge, wabunge wa Tanzania walikubali kurekebisha sheria hiyo — hatua ambayo wakosoaji wanaiona kama itadhoofisha sana mfumo wa vyama vingi nchini Tanzania, na hivyo kuathiri mwenendo wa demokrasia nchini.

Kwa kifupi, mabadiliko ya sheria yanampa mamlaka makubwa zaidi msajili wa vyama vya siasa aliyeteuliwa na serikali si tu kuvifutia usajili vyama vya siasa lakini pia kutoa adhabu ikiwa ni pamoja na kifungo jela ikiwa chama cha siasa, kwa mfano, kitatoa elimu ya uraia kwa wapiga kura na kuendesha shughuli nyingine zenye mrengo wa kisiasa, kwa mujibu wa Reuters.

Vyombo kadhaa vya habari vimemnukuu Zitto Kabwe, kiongozi wa chama cha upinzani ACT-Wazalendo, ambaye mwezi Agosti 2017 alinukuliwa akikosoa mabadiliko hayo ya sheria, akidai kuwa yangefifiisha haki za kisiasa nchini humo. Kabwe aliifananisha sheria hiyo na Muswada wa Huduma za Habari wa 2016, ambao unadaiwa kurudisha nyuma uhuru wa vyombo vya habari. Sasa, Kabwe anaangazia mkanganyiko unaosababishwa na mabadiliko hayo ya Sheria ya Vyama vya Siasa:

“Huwezi kuwa na katiba inayoruhusu uhuru wa watu kukusanyika na kisha uwape mamlaka baadhi ya watu kupokonya uhuru huo.”

Dying democracy?

Kuzorota kwa demokrasia Tanzania chini ya utawala wa Rais Magufuli imekuwa mada isiyoisha na hujirudia mara kwa mara kwenye vyombo vya habari, na pia imekuwa ikijitokeza mara kwa mara kwa waandishi wa kejeli.

Mnano Januari 30, Fatma Karume, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), alitwiti katuni ya mchora katuni maarufu wa Kenya Gado (Septemba 22, 2017)akionesha wajibu wa Rais wa Tanzania, Magufuli na kifo cha demokrasia:

Habari za asubuhi ndugu zangu. Muwe na siku njema

Katika miaka ya karibuni, Tanzania imegeuka kwa kasi kuwa nchi yenye sheria za kiimla  zinazosababisha kuminywa kwa fursa kwa wanasiasa wa upinzani kufanya siasa sambamba na vyombo vya habari. Sasa, wakosoaji wanasema Sheria ya Vyama vya Siasa itafanya iwe vigumu zaidi kwa wanasiasa kufanya siasa za kumkosoa Rais na Chama cha Mapinduzi kilichoshika dola tangu mwaka 1977.

Upinzani ni muhimu kwa demorasia hai. Upinzani imara huisimamia serikali na kuipa changamoto. Katika mazingira ambayo upinzani haupo, ni wazi mahitaji tofauti ya raia hayawezi kuwakilishwa ipasavyo.

Kwa kutumia twiti 15, mwanafunzi wa udaktari Rachel McLellan aliwapitisha wasomaji wake kwenye ucmabuzi unaoangazia hali inayoweza kujitokeza kufuatia sheria hii mpya, na anaonesha mazingira ambayo chama cha upinzani kinachoonesha uhai kinaweza kujikuta kikibanwa: 

Hawawezi tena kufanya mikutano kuwashawishi wapiga kura, wamewekewa mazingira ya kufungwa jela kwa kufanya mikutano na waandishi wa habari. Muswada huu unazuia vyama vya siasa kutoa elimu ya uraia na shughuli za kuwajengea wananchi uwezo shughuli ambazo ni muhimu kwa vyama vya siasa. Inawalazimisha kupata idhini ya serikali ili kupokea misaada ya nje.

Kwa hiyo njia za kuwashawishi wapiga kura wenu zimezibwa. Unafanyaje unapokuwa mpinzani? Nenda ubaoni na uje na mbinu mpya, sivyo? Muswada huu unampa nguvu kubwa zisizodhibitiwa Msajili wa Vyama vya Siasa inayofanya ubunifu huo uwe mgumu

Iwe ni ushirikina au la — wale wanaokosoa mwelekeo wa Tanzania kuwa nchi ya kiimla walitafsiri vibaya uwepo wa bundi bungeni hasa iliposhindikana kumfukuza. 

Bundi alibaki. Spika wa Bunge, Job Ndugai, alijaribu kuondoa imani hiyo kwa maelezo chanya:

“Waheshimiwa Wabunge, tumekuwa tukimwona bundi hapa bungeni tangu asubuhi lakini kwa mila ya watu wa Dodoma, bundi anayeonekana mchana hawezi kuwa na madhara yoyote. Maana yake ni kwamba tusiogope uwepo wa bundi huyu.”

Kwa wakosoaji, hata hivyo, hakuna maelezo mengine chanya ya sheria hiyo mpya.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.