- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Wakombozi wa Kizungu, Shule za ki-Liberia

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Marekani ya Kaskazini, Liberia, Marekani, Elimu, Maendeleo, Mahusiano ya Kimataifa, Sheria, Uandishi wa Habari za Kiraia, The Bridge

Mwanzilishi wa More Than Me, Katie Meyler, nchini Liberia, Septemba 19, 2016, Wikimedia Commons. Picha hii imechukuliwa kutoka ukurasa rasmi wa Flickr wa More Than Me.

Wiki chache zilizopita, mradi wa ProPublica ya Marekani wa uandishi wa habari za uchunguzi ulichapisha habari iliyoitwa Unprotected [1] (Bila Kinga) iliyohusu kashfa kubwa ya unyanyasaji wa kingono katika taasisi isiyo ya kiserikali ya More Than Me (MTM), ambayo inamiliki shule kwa lengo la kuwasaidia wasichana walio hatarini zaidi nchini Liberia huko West Point, Monrovia. Ufichuaji wa kashfa hiyo umewaacha wengi wakijiuliza kuwa iliwezekana vipi kwa jambo hilo kuendelea kwa muda mrefu pasipo kujulikana, lakini shule za binafsi zinazomilikiwa na asasi zisizo za kiserikali kama MTM zinaendelea kuchipuka kila uchwao kote barani Afrika [2], kila moja ikiwa ni njozi ya kutoa misaada ya hisani kwa watu.

Asasi hiyo iliyoanzishwa 2008 na Katie Meyler, raia wa Marekani, na Macintosh Johnson, raia wa Liberia, imani ya Meyler iliyokuwa mithiri ya uenezaji Injili katika kazi za MTM ilimfanya akusanye Dola za Marekani milioni 8 kutoka kwa wafadhili wa kimataifa, watu maarufu na matajiri ambao hutenga sehemu ya fedha zao ili kusaidia jamii. Tangu kuanzishwa kwake, MTM ilipanua idadi ya shule zake kutoka moja hadi 19 zikihudumia zaidi ya wanafunzi 4,000.

Meyler na Johnson hawakuwa na uzoefu katika masuala ya elimu wala maendeleo, lakini nchini Liberia, ambako asilimia 60 ya watoto wenye umri wa kwenda shule hawahudhurii masomo, Meyler alijitokeza kama ‘mwokozi’ wao ambaye angeweza kuendeleza kutokea pale ambapo mfumo wa elimu wa Liberia, ulio katika hali mbaya, ulipokuwa umekomea.

Mwaka 2013, Rais wa Liberia, Bi. Ellen Johnson Sirleaf, alisema kwamba mfumo wa elimu “ulikuwa taabani” [3]baada ya wanafunzi wote 25,000 waliofanya mtihani wa taifa kuanguka. Huku nchi ikijinasua kutoka katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na mgogoro wa Ebola, serikali ilikuwa ikihitaji ufumbuzi kwa udi na uvumba na hivyo kuwageukia wahisani wa kimataifa na wahisani wengine waliotaka kutenda mema.

Katika siku ya ufunguzi wa masomo katika MTM, Rais Sirleaf alitangaza hadharani kumwunga mkono Meyler, akisema kwamba kile alichotaka sana kitokee katika nchi yake ni “kueneza mradi wa Meyler hadi kwenye jamii nyingi kadiri inavyowezekana.”

Huku akikabiliwa na vikwazo vichache vya kisheria, masharti au vizingiti, Meyler alianzisha MTM kama shirika lililosifika kwa kueneza simulizi za kusisimua za ukombozi kupitia mitandao ya kijamii.

Kutiwa hukumuni pasipo kuleta matunda sahihi

Hata hivyo, hadi mwishoni mwa mwaka 2012, minong’ono ya shutuma za unyanyasaji wa kingono dhidi ya Johnson ilikuwa imekwishaanza kuenea katika jamii ya MTM. Lakini hadi wakati huo, sifa ya Meyler ilienea kote katika ulimwengu wa matajiri wahisani akichukuliwa kama  “nyota wa hisani”, akijishindia tuzo kubwa ya dola milioni 1 kutoka kwa JPM Morgan Chase na kutambuliwa katika jarida maarufu laTime kama Mwanadamu wa Kipekee wa mwaka 2014 [4] kwa kazi yake kubwa ya kutoa mwitikio dhidi ya Ebola. Kwa mujibu wa ProPublica, Meyler alikuwa na mashaka tangu 2011 kuhusu mwenendo wa John kupenda wasichana wadogo, lakini wawili hawa walikuwa katika uhusiano wa kimapenzi usio madhubuti sana, na alishindwa kuchukua hatua za haraka na uamuzi wa mwisho dhidi yake. Wengine waliotilia shaka mwenendo wa Johnson walisita kujitokeza na kufichua tabia hiyo wakihofia kwamba Meyler angalichagua upande wa mpenzi wake dhidi ya wale wasichana, alieleza nesi wa shule ya MTM Iris Martor.   

Uchunguzi uliofanywa na The ProPublica unathibitisha kwamba Johnson aliwanajisi na kuwanyanyasa kingono takribani theluthi tatu ya wasichana hapo shuleni, wengine wao wakiwa na umri kinda tu wa miaka 10. Hatimaye, mwaka 2014, wafanyakazi wa MTM walipiga ripoti za vitendo vya Johnson polisi. Naye alitiwa nguvuni huku uchunguzi wa makosa ya jinai ukianzishwa na kufuatiwa na kesi kusikilizwa mahakamani. [5] Meyler aliendelea kuwasiliana na Johnson wakati akiwa mahabusu, lakini hakufika mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi. Johnson aliishia kufa kwa UKIMWI kabla kesi yake haijafika mwisho. ProPublica linathibitisha kwamba wasichana wengi ambao Johnson aliwanajisi au kuwabaka alikuwa pia amewaambukiza VVU.

MTM ilikana kuwa na hatia yoyote ukiachilia mbali kumwajiri Johnson. Wajumbe wa bodi ya MTM wanadai kwamba MTM “ilijenga mazingira salama” kwa ahadi ya dhati kabisa ya kulinda haki za watoto na kuwapa kinga. Meyler alijitosa mwenyewe katika suala hili na kudai kwamba hata yeye alikuwa mwathirika wa vitendo vya Johnson [6] na aliwapongeza wasichana waliojitokeza, huku akiapa kupambana zaidi ili kuwalinda. MTM iliwapa udhamini wa masomo na nyumba baadhi ya waathirika wa vitendo vya Johnson, lakini wengine walihamishwa na walau mmoja alirejea katika maisha mabaya ya mitaani.

‘Wakombozi’ wazungu, mataifa yaliyojaa unyonge

Leo, MTM inaendelea kufanya kazi zake ikishirikiana moja kwa moja na serikali ya Liberia. Mwaka 2016, Wizara ya Elimu ilizindua Shule za Ushirika za Liberia chini ya Programu ya Maendeleo ya Elimu ya Liberia [7], ikiruhusu takribani shule 100 kuendeshwa na mashirika yasiyo ya kiserikali, yakiwemo MTM, Bridge International Academies (ambalo pia linachunguzwa [8] kwa vitendo visivyo vya kufaa), Rising Academies

Vyama vya walimu nchini Liberia na hata nje, na pia wataalamu wa maendeleo wanaopinga ubinafsishaji wa shule barani Afrika, walilaani sana mradi huu. Hata hivyo, pamoja na kutoa matokeo mkanganyiko katika mwaka wa kwanza [9], serikali inapanga kuongeza mara mbili idadi ya shule zinazohamishiwa katika mikono ya mashirika yasiyo ya kiserikali ifikapo mwaka 2019, mpango ambao unazidi kushika kasi kote barani Afrika. Utafiti [10] mmoja unakadiria kwamba mtoto mmoja katika wanne barani Afrika—watoto milioni 66—atasoma katika shule binafsi ifikapo mwaka 2021.

Katika makubaliano ya ushirikiano wa aina saba nchini Liberia, zaidi ya nusu yameanzishwa na wazungu, wanaosukumwa na nia ya kutenda mema kuliko kuzingatia ukweli wa hali halisi katika muktadha maarifa. Asili, jinsia na fursa vyote hivi vilikuwa na nafasi katika uanzishaji wa MTM na mashirika mengine kama hayo. Kama mwanamke mzungu raia wa Marekani, Meyler alipata fursa nyingi ambazo pengine raia mweusi wa Liberia asingepata, mjumbe mmoja wa zamani wa MTM Chidegar “Chid” Liberty aliliambia ProPublica.

“Kulikuwa na umbumbumbu mwingi wa namna gani mambo yangaliweza kwenda kombo kama kusingalikuwa na mifumo sahihi ya utawala,” anasema Liberty, mtu mwenye uraia pacha wa Liberia na Marekani ambaye muda mwingine huishi Monrovia.

Ujinga wa kujitakia wa Meyler unaenda sambamba na ‘tatizo la mkombozi mzungu’, maelezo yanayoonyesha wazungu wanaosukumwa na nia ya kutaka kuwasaidia watu wasio wazungu, tabia ambayo ina asili yake katika historia ya ukoloni na ubaguzi wa rangi ambayo inatazama kila kitu kwa dhana potofu ya Waafrika weusi “wasio wastaarabu”. Mwandishi Teju Cole anaiita hali hii Tatizo la Kujiundia la Mzungu Mkombozi [11] –kwa sababu kuna fursa ya kutengeneza fedha kwa kuingilia kati katika maisha ya watu wengine.. 

Liberty, ambaye alijitoa katika bodi ya MTM mwaka 2015, aliliambia ProPublica akisema kwamba aliamini kwamba shirika “lilikuwa na nafasi yake kubwa katika uhalifu wa kitaasisi dhidi ya wasichana hao walioathirika.” 

“Kokote duniani, mtu mwingine yeyote ambaye kwa namna moja au nyingine alishiriki basi angewajibishwa,” alisema Liberty, akimaanisha kwamba Meyler na fursa walizopata watu weupe katika shirika hilo ndiyo walioweka msingi wa kimaadili wa MTM na vitendo vyake.

Kupanua au kusinyaza

Mpango ya Liberia ya kupanua ushirikiano wa shule za binafsi na za umma ni wa aina yake [12]kote barani Afrika. Kuanzia Bill Gates hadi Mark Zuckerberg, matajiri wahisani ambao ProPublica limewataja kama walio katika kikundi cha “watatua matatizo ya dunia wachache wanaozunguka kila pahali” wamekuwa wakizikwaza serikali kwa mitindo yao ya uvamizi angamizi. Kundi hili linatambua uharaka uliopo wa kuwekeza katika elimu barani Afrika, na jinsi gani jambo hili linavyoweza kufichwa nyuma ya usamaria wema.

Watetezi wa ubinafsishaji wa shule wanasisitiza kwamba shule za binafsi zinafanya vizuri zaidi kuliko zile za serikali. Lakini kama kisanga hichi cha MTM kinavyoonyesha, kung’ang’ania kwao kusisitiza juu ya upanuzi—jambo ambalo linawaingizia faida ya haraka katika uwekezaji wao kihisia na kifedha—ni jambo linaloweza kusababisha ukiukwaji wa haki za binadamu katika viwango vya kushangaza.

Ikiwa mataifa kama Liberia yanashindwa kuitazama elimu kama haki ya binadamu [13] inayopaswa kutolewa na dola, mapambano yao ya kuupangua mfumo wa elimu yataendelea kutegemea mashirika kama MTM kujazia ombwe hilo.

Mnamo Oktoba 14 kupitiabarua [14]iliyowekwa kwenye wavuti ya MTM, Meyler alitangaza kwamba angejiuzulu kwa muda kama ofisa mtendaji mkuu wa shirika ili taasisi hiyo ifanye uchunguzi wake wa ndani kuhusu tuhuma zilizoibuliwa na ProPublica.

Hakuna ubishi kwamba, vitendo vya jinai vya hali ya juu vilifanyika katika mazingira ya shule ya MTM pasipo uwajibikaji wa aina yoyote. Meyler aliwaaminisha wasichana waliokuwa hatarini kabisa wa Monrovia katika ndoto ya mchana ya “ukombozi” wa uinjilishaji ulioishia kuwa dude lililokosa udhibiti na kuwadhulumu mno, kwa utumia udanganyifu wa maendeleo ya “kutenda mema”.

Lakini, mtu yeyote anayetokea kukaa barani Afrika japo kwa muda fulani tu kwa vyovyote atamjua walau mtu mmoja wa aina ya Meyler, na hata pengine anatambua fikra zake za kinjozi katika miradi yao. Licha ya ukosoaji wa waziwazi, vuguvugu la kujitolea lenye thamani ya dola bilioni 173 [15] linazidi kukua barani Afrika, likiwapa vijana wenye njozi uhuru [16] wa kuishi ndoto zao za kuwa wakombozi kwa gharama ya jamii za wanyonge. Kuanzia katika Instagram [17] hati kwenye mihadhara ya TED, kuna kwaya ya dunia ambayo iko tayari kutoa mahubiri yafuatayo.

Mchanganyiko madhubuti wa fursa ya kupendelewa na kukosa weledi husababisha kutokea kwa makosa makubwa. Mimi mwenyewe nimewahi kufanya makosa kiasi na ninawafahamu marafiki, wenzangu na wanafunzi wa zamani nao pia wameangukia katika mtandao mgumu wenye mambo mengi wa miradi ya maendeleo ambamo hawakuwa na uzoefu nayo wala kuijuia kwa undani. Maendeleo ya kweli huchukua muda—hakuna njia rahisi.  

Si kila mradi unafanya vibaya kama ilivyokuwa kwa MTM, na si kila mzungu anayefanya kazi Afrika ni mtu mwovu. Bila shaka, suala la weledi, halifungwi na asili ya mtu, daraja na jinsia. Lakini simulizi kuhusu Meyler linaashiria wito wa kuchukuliwa hatua za haraka, mshikamano, uwajibikaji na uadilifu pale linapokuja suala la maendeleo—ikiwa ni lazima sana kuendelea kufanya kazi kwa jinsi hii.