Ungana na Global Voices Julai 9 Kupinga Kodi ya Mitandao ya Kijamii Nchini Uganda

Bango la kampeni ya kupinga kodi ya mitandao ya kijamii [#NoToSocialMediaTax] limetengenezwa na Innocent Amanyire / @NinnoJackJr

Ungana na Waandishi wa Global Voices ukanda wa Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara (@gvssafrica) kushiriki majadiliano yatakayofanyika kwa lugha mbalimbali kushinikiza kusitishwa kwa kodi ya mitandao ya kijamii nchini Uganda.

Mnamo Julai 1, serikali ya Uganda ilianza kutekeleza sheria mpya inayotoza kodi ya shilingi 200 za Uganda [US$0.05, £0.04] kila siku kwa watu wanaotumia majukwaa ya mtandaoni, pamoja na upinzani mkubwa kutoka watetezi wa uhuru wa kujieleza ndani na nje ya nchi hiyo.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, inalenga kuimarisha bajeti ya taifa na kudhibiti “tabia ya umbeya” inayoendekezwa na wa-Ganda kwenye mitandao ya kijamii. Kodi hiyo pia inaonekana kukubalika kwa makampuni yanayotoa huduma za simu, ambayo hapo awali hayakuwa yanapata faida moja kwa moja kwa matumizi ya “mitandao ya nje” kama vile Facebook, Twitter, na WhatsApp.

Jeshi la polisi limepewa nguvu ya kusajili SIM kadi zote kwa msaada wa Kituo cha Taifa cha Takwimu za Kidijitali. Hatua hiyo pia inawalazimisha wa-Ganda kutumia akaunti zao za huduma ya fedha kwa njia ya simu ili kuongeza salio na hivyo kufanya iwe lazima kulipa kodi ya asilimia moja ya kiasi kinachohamishwa kwa kila muamala unaofanyika.

Sera hizi mpya zinafanya iwe gharama kwa wa-Ganda -hususani wale wanaoishi kwenye umasikini – kuwasiliana na kufanya shughuli zozote kwa kutumia simu au vifaa vinavyofanana na hivyo.

Mnamo Julai 2, asasi za kiraia na mawakili wa kisheria nchini Uganda walifungua kesi mahakamani kupinga sheria hiyo, wakisema inapingana na katiba ya nchi.

Mwandamanaji akionesha upinzani wake sheria ya mitandao ya kijamii nchini Uganda kwenye mkusanyiko uliofanyika mnamo Julai 6, 2018.

Mnamo Julai 6, raia walioguswa na mwenendo huo na mambo kwa kushirikiana na mawakili wa asasi za kiraia walitoa tamko la pamoja kwa vyombo vya habari [tazama chini ya makala hii] wakizungumzia masuala kadhaa ikiwemo kuwataka wa-Ganda kuepuka kulipa kodi hiyo; kutumia mbinu mbadala za kufanya miamala ya fedha pamoja na kuunganishwa na mitandao ya kijamii; na kuunga mkono “Siku ya Taifa ya Maandamano Dhidi ya Kodi ya Dhuluma” mnamo Jumatano, Julai 11, 2018.

Jumuiya ya Global Voices na mtandao wetu wa marafiki na washirika tumeona vyema kuunga mkono juhudi hizi na nyingine zinazolenga kudai kusitishwa kwa kodi hii. Tunaamini kwamba kodi hii ni mpango wa kuwadhibiti wa-Ganda na kunyamazisha sauti zao.

Tunaamini mitandao ya kijamii inapaswa kupatikana kwa uhuru kwa watu wote, wakiwemo wa-Ganda. Sheria ya kodi ya mitandao ya kijamii nchini Uganda lazima ikomeshwe!

Kwa maana hiyo siku ya Jumatatu, Julai 9, kuanzia saa 8:00 mchana kwa Saa za Afrika Mashariki, tunapanga ku-twiti tukiwalenga viongozi wetu wa jamii, serikali na wanadiplomasia, watumiaji mashuhuri wa mitandao ya kijamii kwa madhumuni ya kuongeza uelewa wa watu kuhusu suala hili. Tunawaomba wanablogu na watumiaji wa mitandao ya kijamii duniani kote kuungana nasi.

#NoToSocialMediaTax: Mazungumzo ya kwenye mtandao wa twita kupinga kodi ya mitandao ya kijamii nchini Uganda

Tarehe: Jumatatu, Julai 9, 2018

Muda: 8:00 – 11:00 Saa za Afrika Mashariki / 11:00 – 14:00 GMT / Tazama hapa kujua muda kwa eneo lako

Alama ishara itakayotumika: #NoToSocialMediaTax

Mwandaaji: Global Voices Afrika ya Kusini mwa Jangwa la Sahara

Twiti unazoweza kuzitumia:

  • Uhuru ni bure, hautozwi kodi. Huwezi kuzuia uhuru wa kujieleza nchini Uganda. Tunapinga kodi ya mitandao ya kijamii #NotoSocialMediaTax https://goo.gl/Ljjzmy
  • Haki za watumiaji wa mitandao ni haki za binadamu pia! Tunapinga kodi ya mitandao ya kijamii nchini Uganda #NotoSocialMediaTax  https://goo.gl/pEZtMu
  • Mitandao ya kijamii ni bure, acheni iendelee kuwa huru nchini Uganda! #NotoSocialMediaTax
  • Msiubane uhuru wa kujieleza. Tunapinga! #NotoSocialMediaTax
  • Enzi za Giza nchini #Uganda… Kodi mpaka kwenye visivyofaa kutozwa kodi! #NotoSocialMediaTax
  • Serikali ya Uganda lazima ilinde ustawi wa wananchi wake na sio kuwatoza kodi mpaka wafe! #NotoSocialMediaTax
  • Tunapinga kodi ya mitandao ya kijamii nchini Uganda. Utaratibu huu haukubaliki #NotoSocialMediaTax

 

TAMKO LA PAMOJA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU MAREKEBISHO YA SHERIA KWA MINAJILI YA KUTOZA KODI MATUMIZI YA MITANDAO YA KIJAMII NA MIAMALA YA FEDHA KWA NJIA YA SIMU ZA KIGANJANI

Imetolewa mnamo Ijumaa,Julai 6, 2018 saa 8.00 alasiri.

Mnamo Jumanne, Julai 3, 2018, sisi vijana na viongozi vijana kutoka serikali mbalimbali za wanafunzi, wanamuziki, wasanii, wafanyabiashara wadogo na wa kati na Bunge la Uganda tulifanya mkutano na waandishi wa habari ambapo tulionesha masikitiko yetu makubwa kuhusu mabadiliko ya sheria ya Sheria ya Kodi inayoelekeza kutozwa kodi kwa matumizi ya mitandao ya kijamii na kulipwa kwa tozo ya asilimia moja kwa kila muamala unaofanyika kupitia huduma za fedha kwa njia ya simu za kiganjani.

Tulimwomba Spika wa Bunge kukatisha kikao cha Bunge na kumwelekeza Kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni kuwasilisha hoja ya kusitisha marekebisho hayo Ijumaa, Julai 6, 2018. Muda tuliokuwa tumempa umeisha masaa kadhaa yaliyopita na tuko hapa kutangaza hatua tunazochukua:

i) Tunatoa wito kwa raia na watoaji wa huduma kuacha kufanya miamala yoyote kwa hutumia huduma za fedha kwa njia ya simu na ikibidi kufanya miamala kutumia njia mbadala zisizopitia kwenye simu zao ili kukwepa kulipa kodi hiyo;

ii) Tunawahamasisha wananchi kutumia mbinu mbadala zilizopo kuwawezesha kuendelea kuwepo mtandaoni bila kulazimika kulipa shilingi za Uganda 200 kila siku ili kupata huduma za mitandao ya kijamii;

iii) Tunawaomba Wabunge wa Bunge la Uganda kuharakisha mchakato wa kuliomba bunge kuchukua hatua lakini pia kufanya mashauriano na wapigakura wao kuhusu suala hili;

iiii) Mwisho, tunatangaza kuwa Jumatano, Julai 11, 2018 kuwa Siku ya Taifa ya Maandamano ya Amani Kupinga Kodi hiyo ya Dhuluma. Kwa mukhtadha huu, tunawaomba wananchi kuwasilisha saini zao kuonesha kupinga kodi hii kwa wabunge wao na wavae nguo nyekundu wanapokwenda kwenye shughuli zao. Tumelijulisha Jeshi la Polisi Uganda na nakala ya taarifa tuliyowapa inapatikana.

Tutaendelea kuyashirikisha majimbo yetu na viongozi katika kupinga, kukataa na kuendelea kugomea mpaka kodi hiyo iliyoanzishwa bila kufikiriwa vizuri itakapoondolewa. Kama viongozi vijana, tumefanya utafiti na mashauriano na tuko tayari kushauri maeneo muafaka zaidi ya mifumo sahihi zaidi ya kodi ambayo itakuwa endelevu na yenye manufaa kwa wananchi na serikali.

KAMATI KUU
HARAKATI ZA KITAIFA ZINAZOENDESHWA NA WANANCHI KUPINGA KODI YA DHULUMA

Makala mbalimbali za Global Voices kuhusu mitandao ya kijamii nchini Uganda:

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.