Baada ya blogu kadhaa huru na kurasa za mitandao ya kijamii, sasa tovuti maarufu zaidi ya habari huru nchini Tanzania inayoendeshwa kwa kutumia maoni yanayowekwa na watumiaji wake, Jamii Forum, imetoweka hewani kufuatia “kodi ya blogu” inayotarajiwa kuanza kutekelezwa hivi karibuni.
Ifikapo Juni 15, 2018, wanablogu wote Tanzania watalazimika kuwa wamejiandikisha na kulipa kiasi cha dola za Marekani 900 kwa mwaka ili kuweza kuchapisha maudhui mtandaoni. Baada ya Juni 15, ikiwa blogu na aina nyingine ya maudhui ya mtandaoni, kama vile idhaa za YouTube, zitaendesha shughuli zake bila kuwa na leseni, zinaweza kuadhibiwa kwa kutozwa faini ya “si chini ya shilingi milioni tano (kama Dola 2,500) au kifungo jela “kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja.”
Ingawa ada ya kujiandikisha pamoja na faini zinazoambatana nazo ni kubwa, wanablogu wengi wanasema tatizo sio fedha peke yake bali ugumu na utata uliopo katika kufuata kanuni hizo mpya.
Tangu maelekezo yatolewe awali na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) mnamo Machi 16, 2018, wanablogu wa Tanzania na taasisi za kiraia wamekuwa na maoni mbalimbali dhidi ya kanuni hizo mpya.
Kituo cha Sheria na Kutetea Haki za Binadamu na mashirika mengine ya kiraia ikiwa ni pamoja na Watetezi wa Haki za Binadamu, Baraza la Habari Tanzania, Jamii Media, Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania na Jukwaa la Wahariri Tanzania walifungua pingamizi lililowekwa kupitia Mahakama Kuu kanda ya Mtwara mnamo Mei 4. Hata hivyo, Jaji aliwataka kufungua tena malalamikio yao kwa sababu za kiufundi, na pingamizi lao la muda lilidumu mpaka Mei 28. Hata hivyo, kesi yao hatimaye ilitupiliwa mbali jaji akidai kwamba “mashirika hayo yalishindwa kuthibitisha namna gani yangeathirika na kanuni hizo.”
Wanablogu wa Tanzania wamepinga kanuni hizo mpya kwa mbinu zenye ubunifu, huku wakitumia mitandao ya kijamii kutoa maoni yao waziwazi kuhusu kanuni hizo za kublogu. Aikande Kwayu, ambaye amekuwa akiblogu hususani kuhusu siasa za Tanzania na uchaguzi wa 2015 (na pia huandika mapitio ya vitabu na masimulizi) alisimamisha blogu yake mnamo Mei 1 kupinga kanuni hizo.
Mtega, blogu ya teknolojia na maendeleo inayomilikiwa na Ben Taylor anayeishi Uingereza, aliwakaribisha wanablogu wa Tanzania kuandika makala za wageni kupitia blogu yake. Chambi Chachage alihamisha umiliki wa blogu yake ya Udadisi mnamo Aprili 27 kwenda kwa Takura Zhangazha, anayeishi Zimbabwe. Na Elsie Eyakuze alisitisha blogu yake ya The Mikocheni Report, akiamua kumpumzika awe “mkimbizi wa kidijitali”:
Yes. Am taking a break, and as a digital refugees will depend on the kindness of others until I can figure out the answer to the What Next question.
— Elsie Eyakuze (@MikocheniReport) June 12, 2018
Katika siku za hivi karibuni wanablogu wa Tanzania wamepinga kanuni mpya za kublogu -lakini kwa mbinu mbalimbali, sivyo?! @aikande, siku hizi unablogu kupitia @mtega? @Udadisi, umebadili umiliki? @MikocheniReport, umefunga ya kwako? Sahihi? Wengine vipi?
Elsie Eyakuze anajibu: Ndio. Nimeamua kupumzika, na kama mkimbizi wa kidijitali nitategemea ukarimu wa wengine mpaka hapo nitakapopata jibu la swali la ‘Nini Kinafuata’
.
Mnamo Juni 11, tovuti maarufu zaidi ya Jamii Forum — ambayo imepachikwa majina ya utani kama vile “Reddit ya Tanzania” na “Swahili Wikileaks” — ilifungwa, na kusababisha tahayaruki kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii.
Mwezi Desemba 2016, Jeshi la Polisi nchini Tanzania lilimkamata Maxence Melo, mwanzilishi mwenza, na mkurugenzi wa Jamii Forums, kwa kukataa kutoa taarifa za wanachama wake, kama alivyotakiwa kufanya hivyo kwa mujibu wa Sheria ya Makosa ya Mtandao.
Mnamo Juni 12, Elsie Eyakuze alitwiti kuelezea namna gani mitandao ya kijamii imewaunganisha watu hata nje ya mitandao nchini Tanzania, pamoja na nafasi kubwa ya mtandao wa Jamii Forums kama jukwaa la wanaharakati wanaovujisha nyaraka zinazohusiana na ufisadi:
I mean. People were leaking documents like whoa all through the forum. Way pre Mange Kimambi. Never imagined I would end up meeting Mike and Max. They smiled more easily then. We were all so much younger! Then I met you all. Akina @mtega and @Dunia_Duara
— Elsie Eyakuze (@MikocheniReport) June 12, 2018
Kwa hiyo nilimfuatilia yeye na blogu yake [Chambi Chachage.] Hoja maridhawa ni jambo la kupendeza. Na baadae nikaanza kuvutiwa na blogu ya Makamba inayoitwa Taifa Letu. Kisha nikajiandikisha kama mwanachama kwenye mtandao wa Jamii Forums…nyie jamaa, katikati ya miaka ya 2000 mlikuwa moto!
Ninamaanisha. Watu walikuwa wanavujisha nyaraka kama nini vile kupitia jukwaa hilo. Zilikuwa enzi za kabla ya akina Mange Kimambo. Sikuwahi kuwaza ningekuja kukutana na watu kama Mike na Max. Walikuwa wepesi sana kutabasamu kipindi hicho. Sote tulikuwa wadogo sana! Kisha nikaonana na nyie wote. Akina @mtega na @Dunia_Duara
Kwenye mahojiano, mwanzilishi wa Jamii Forums, Maxence Melo aliliambia gazeti la The Citizen: “Ni dhahiri kuwa jukwaa letu lilikuwa mlengwa mkuu wakati kanuni hizi zinatengenezwa.”
Kodi ya dola za Marekani 900 kwa mwaka ni kiasi kikubwa cha fedha katika nchi ambayo karibu theluthi moja ya watu bado wanaishi kwenye umasikini wa kutupa. Kutaka majukwaa yote yajiandikishe na kupata cheti cha mlipa kodi inaweza kuleta usumbufu mkubwa kwa sababu wanablogu wengi ni watu wa kawaida wasio na makampuni yaliyoandikishwa. Wamiliki wa blogu na majukwaa ya habari mtandaoni yanalazimika kwanza kupata leseni, na kisha, kufanya hali kuwa ngumu zaidi kwao, watalazimika kuheshimu mlolongo wa kanuni nyingi ngumu.
Mnamo Juni 12, Aikande Kwayu alieleza kwenye twiti hii:
I also think the problem is not the payment as much as the subsequent responsibility following the license (if granted). It is not only a self-censorship license but a way to become the state's tool to censor others (contributors) civic right to express.
— Aikande C. Kwayu (@aikande) June 12, 2018
Ninadhani tatizo sio malipo kivile kuliko ule wajibu unaofuatia baada ya leseni (ikiwa itapatikana). Hii sio tu leseni ya kujidhibiti mwenyewe lakini pia namna ya kuwa nyenzo ya serikali kuwadhibiti haki ya kiraia ya wengine (wachangiaji) kujieleza.
Mnamo Aprili 12, Ben Taylor alifafanua baadhi ya masuala tata, akibainisha kuwa kanuni hizi zinamtaka mmiliki wa blogu “awe na uwezo wa kumbaini kila anayebandika chochote”, na mmiliki wa blogu “lazima atoe ushirikiano na maafisa wa polisi” pale atakapohitajika kwa mujibu wa kanuni hizo.
Taylor anafikiri kwamba takwa hilo linaweza kumaamisha “kukutaka kutoa utambulisho wa mtu yeyote anayechapisha kitu kwenye blogu yako, na hivyo kumfanya mtu yeyote anayetoa maoni kwa kuficha utambulisho wake iwe kwenye blogu, tovuti ya gazeti au jukwaa la tovuti kuwa hatarini kufahamika.”
Nchini Tanzania, joto la kisiasa limepanda katika kipindi cha miaka michache iliyopita. Tangu uchaguzi wa rais wa mwaka 2015, upinzani nchini Tanzania umebanwa na zuio la mikutano yao ya kisiasa sambamba na kubanwa kwa vyombo huru vya habari, ukamataji, vitisho na kuadhibiwa kwa raia wanaomkosoa Rais John P. Magufuli wa chama tawala cha Chama cha Mapinduzi (CCM).
Sheria ya Makosa ya Mtandao nchini humo, iliyopitishwa mwaka 2015, imetumika kwa kiasi kikubwa kufanya mambo yawe magumu. Madhalani, mwaka 2015 na 2016 pekee, wa-Tanzania wasiopungua 14 walikamatwa na kushitakiwa kwa kutumia sheria hiyo, kosa lao likiwa ni kumtukana rais kwenye mitandao ya kijamii.
Tanzania si nchi pekee inayojaribu kudhibiti wananchi wake kutumia mitandao ya kijamii katika miezi ya hivi karibuni. Uganda na Kenya nazo zimetoa kanuni mpya zinazoongoza uzalishaji na udhibiti wa maudhui ya mtandaoni.