Taka za Plastiki ni Tatizo Kubwa Nchini Uganda

Picha ikionesha mchanganyiko wa mboji na taka za plastiki katika mitaa ya Kampala. Picha na Enno Schröder. CC BY 2.0

Siku ya Mazingira duniani huadhimishwa Juni 5, kila mwaka tangu mwaka  1974. Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Shinda Uchafuzi wa Mazingira kwa Plastiki” ukiwa ni wito ambao ni muhimu sana kwa Uganda, ambapo ni kawaida sana kwa watu kutupa chupa na mifuko ya plastiki mitaani.

Takataka za plastiki zikikusanyika katika mifumo ya maji taka, huongeza mafuriko mjini na huishia katika maziwa na baharini, ambapo samaki hula na kusababisha matatizo ya afya kwa viumbe vya majini na binadamu. Katika maeneo ya vijijini, plastiki nyingi huishia mashambani na hata kwenye bustani ambapo huathiri ukuaji wa mimea kwa sababu huzuia mtiririko mzuri wa maji na hewa.

Uganda imeshajaribu kuzuia mifuko ya plastiki (ambayo ni maarufu kama kaveera), lakini utekelezaji marufuku hiyo umekuwa mgumu kwa sababu ya ushawishi wa wazalishaji wa mifuko, kutokuafikiana miongoni mwa wanasiasa na jamii kukosa ufahamu juu ya zuio hilo.

Katika tovuti ya Dunia Yaikuta Uganda, mwandishi Baz Waiswa mwaka 2016 aliandika:

Lakini hapo Aprili 2015, pamoja na migomo ya wanachama wa sekta binafsi, ikiwamo kupelekana mahakamani, Wizara ya Maji na Mazingira chini ya Mamlaka ya Uangalizi wa Mazingira Nchini (NEMA) ilipitisha zuio la kuagiza, kuzalisha na kutumia mifuko ya plastiki yenye kiwambo chini ya makroni 30.

Hata hivyo utekelezaji haukuwa mzuri kwa kuwa biashara zilizoathiriwa na katazo hilo na baadhi ya taasisi za serikali likiwamo baraza la mawaziri walipigana dhidi ya zuio hilo wakitaka liondolewe. Kwenda mbele na kurudi nyuma huko kuliuchanganya umma. Baadhi ya wafanyabiashara wameacha kutumia kaveera wakati wengine wameendelea kufungashia wateja wao bidhaa katika mifuko ya plastiki pamoja na tishio la kuchukuliwa hatua za kisheria na NEMA.

Katika siku ya Mazingira mwaka huu, Rais Yoweri Museveni aliamuru viwanda 45 vya plastiki kuacha kutengeneza mifuko ya plastiki kwa mara nyingine tena akijaribu kulipa zuio meno. Kilichobaki ni kuangalia kama wakati huu zuio hilo litafanikiwa.

Ndani ya Kampala, mji mkuu na mkubwa zaidi wa Uganda, taka za plastiki zinaweza kuzuia mtiririko wa maji taka. Mamlaka ya Jiji la Kampala (KCCA) limefanya jitihada za kuweka vyombo vya taka mitaani, na kufanya ukusanyaji wa taka wa mara kwa mara na kuhamasisha urudiaji wa bidhaa kwa kusaini mkataba wa maafikiano Coca Cola wa kuongeza pato wanalopata watu kwa kuokota taka za plastiki kutoka dola $0.05 kwa kilo mpaka dola $0.13.

Watu binafsi nao wanapambana na uchafuzi wa mazingira kwa plastiki kwa mfano mwaka 2017 CGTN Africa waliandika kuhusu wajasiriamali vijana ambao walikusanya taka za plastiki na kuzigeuza matofali ya kujengea.

Katika siku ya mazingira mwaka huu, kikundi cha uhifadhi mazingira cha Mikono Midogo Yageuka Kijani kilitembelea shule tofauti tofauti Mashariki mwa Uganda na kuwafundisha watoto hatari ya kutumia mifuko ya plastiki:

Meneja Mkuu wa Mikono Midogo Yageuka Kijani pia aliandika katika ukurasa wake wa twita kwa hashitagi ya #PambanaNaUchafuziWaPlastiki akihamasisha wasafiri kuhifadhi vyema chupa zao za maji za plastiki:

Plastiki sio chanzo pekee cha kutia hofu kwa mazingira nchini. Kwa mfano uchimbaji wa mchanga uliopitiliza pembezoni mwa Ziwa Viktoria unaleta hofu kwa viumbe wa majini kwa vile samaki hutumia mchanga kama makazi yao na sehemu ya kuzaliana. Pia maeneo oevu  hutumika kama eneo la kukingia maji na kupambana na mafuriko. Uganda ina kazi ya kufanya katika kuhakikisha mazingira ni safi na salama kwa afya za wananchi wake.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.