Riwaya Hii ya Kidigitali Yasimulia Vurugu Dhidi ya Waindonesia Wenye Asili ya China Walioandamana Nchini Indonesia Mwaka 1998

Kitabu cha digitali cha riwaya kinachoelezea hadithi za Wachina wenye asili ya Indonesia ambao walishambuliwa wakati wa maandamano yaliyoiangusha serikali ya Indonesia hapo mwaka 1998

Mnamo Mei 1998, maandamano yenye vurugu yaliibuka nchini Indonesia kumtaka Rais Suharto aliyeitawala nchi hiyo kwa miongo mitatu ajiuzulu. Maandamano haya yaliletea mabadiliko katika serikali lakini maelfu ya raia haswa Waindonesia wenye asili ya China wakijeruhiwa, wakibakwa na kuuawa. Waorang Tionghoa wengi (ndivyo WaIndonesia wenye asili ya China wanavyoitwa) waliikimbia nchi kwa sababu vurugu zilizoenea ziliwalenga wao.

Taarifa ya serikali iliyatolewa Oktoba 1998 ilionesha kuwa wakati baadhi ya vurugu dhidi ya Waindonesia wenye asili China zilikuwa za hiyari, lakini mikasa mingi ilionekana kupangwa kiufundi na wahuni wa mjini wakiungwa mkono na mamlaka zenye nguvu kisiasa na kijeshi. Taarifa hiyo pia iliandika kuhusu visa vya ubakaji ambapo waathirika walikuwa ni wanawake Waindonesia wenye asili ya China.

Baada ya miongo miwili, wahanga wa mashambulio hayo na familia zao wameendelea kutafuta haki.

Ikiwa imeandikwa na msanii anayeishi Melbourne Rani Pramesti, riwaya ya ‘Minong'ono ya Wachina’ inasimulia jinsi janga hilo lilivyomlazimisha kuikimbia nchi yake aliyoipenda hapo mwaka 1998. Pia kitabu hicho kimebeba simulizi za wanawake walioshuhudia maandamano hayo ya mwaka 1998.

Global Voices ilimuhoji kuhusu riwaya hiyo na kichocheo cha kuanzisha mradi huu:

Minong'ono ya Wachina ilichochewa na uzoefu wangu binafsi wa jinsi vurugu za kibaguzi za Mei 1998 zilivyoathiri maana ya utambulisho wangu pamoja na mazingira ya tukio hilo la kihistoria la Mei 1998.

Nilitambua jinsi suala la 1998 lilivyokuwa muhimu lakini lisilozumgumziwa miongoni mwa Waindonesia wenye asili ya China wanaoishi Australia.

Siwezi kuzungumzia uzoefu wa watu wengine lakini naweza kuzungumzia uzoefu wangu. Mimi na familia yangu tulisalimika katika ubakaji, uporaji na vurugu za 1998 lakini tumeishi katika kipindi ambacho tulikabiliwa na ubaguzi uliochochewa na siasa. Nikiwa nimelelewa kama Muindonesia kamili mwenye kujivunia nchi yake, vurugu za 1998 zilileta maswali juu ya utambulisho wangu.

Kupitia Minong'ono ya Wachina, nataka kuweka wazi jinsi ubaguzi unaochochewa na siasa unavyoweza kuwafanya watu (na) haijalishi imepita miaka mingapi tangu itokee. Ubaguzi unaochochewa na siasa unagharama kubwa kwa binadamu na sio tu kwa Indonesia bali kwa dunia yote leo.

Alifafanua ni kwa nini alichagua jina la riwaya yake kuwa ‘Minong'ono ya Wachina':

Wakati wa shughuli za usanifu na jamii, tulizungumza kuhusu mambo mengi na kila kitu. Lakini bado nilipoibua tukio lililotokea 1998 na kuhusu wapi na nini sicho, sauti ndani ya chumba zilififia na kuwa minong'ono.

Kama mwanafunzi wa sanaa za maonesho, nimejifunza kuchunguza sauti, lugha na ishara za mwili. Nilichokumbana nacho wakati wa mikutano na semina za sanaa za maonesho ni kwamba mwaka 1998 umeshika nafasi muhimu katika jamii

Wengi walisema kuwa vurugu za 1998 ni kitu ambacho ni mwiko kukizungumzia. Limebaki kuwa jambo nyeti, ambalo ni vigumu kulizungumzia lakini mwiko halitoshi kuwa neno la kulielezea jambo hilo.

Na hiki ndicho anachoamini kazi yake itafanya:

Siku moja nilihudhuria usomaji wa mashairi wa Mark Gonzales na moja ya shairi lake lilisema “Hatuwezi kupona kile tusichokabiliana nacho”. Na hiki kilikuwa ukweli kwangu.

Ni miaka 20 sasa na mwaka 1998 ni vigumu kuukubali. Kuna mambo mengi sana ya kufaywa kwa ajili ya uponyaji na kupata aina fulani ya haki. Sizungumzii kuhusu kupona katika ngazi ya mtu binafsi pekee bali kwa Taifa pia.

Nataka wasomaji wangu wakumbuke mwaka 1998 unahusu nini na pia kuguswa na uzoefu wa waliyoyapitia watu wengine.

Katika kazi yangu, muhusika wangu mmoja mwenye miaka 12 alikumbana na mkasa wa utambulisho wake kuchanwa chanwa na siasa za kibaguzi.

Napenda jinsi sanaa za maonyesho zilivyochangia kusimulia habari zangu binafsi. Hata hivyo, pamoja na simulizi ndogo ndogo tunazozisikia kila mahali, mwisho wake ni kuwa wote tu wanadamu na kila mmoja ana simulizi yake ndogo na hivyo ndivyo tunavyounganishwa katika ngazi kubwa zaidi kutoka mtu mmoja kwenda kwa mtu mwingine.

Ukurasa mmojawapo wa riwaya ya Minong'ono ya Wachina. Imetumika kwa ruhusa.

Kwa sasa Minong'ono ya Wachina inapatikana Indonesia. Tolea kwa lugha ya Kiingereza itapatikana mwishoni mwa mwaka 2018. Kazi ya Rani inapatikana katika tovuti yake na unaweza kumpata kupitia ukurasa wake wa Facebook na Instagram.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.