Serikali ya Ufilipino Yapanga Kukifunga Kisiwa cha Kitalii cha Boracay na Kutishia Kuhamisha Maelfu ya Wakazi

Pwani ya mchanga mweupe ya Boraca. Picha kwa hisani ya Alexey Komarov. CC BY 3.0

Wakazi wa kisiwa cha Boracay kikichopo katikati mwa mji wa Alkan uliomaeneo ya kati ya Ufilipino, wanashirikiana kupinga mpango wa serikali wa kukifunga kwa miezi sita kisiwa maarufu duniani kwa utalii kwa kile kinachoelezwa kuwa ni kwa sababu ya “uboreshaji” wa mazingira, huku ujenzi wa makasino mawili makubwa ukiendelea.

Wakihofia kupoteza ajira kwa maelfu ya wafanyakazi na kuharibiwa kwa uchumi unaotokana na shughuli za kitalii kwenye kisiwa cha Boracay, wakazi wake wameunda UmojaWaKuteteaKutokufungwaKwaBoracay kwa lengo la kulinda mustakabali wa maisha yao pamoja na kupinga hatua ya kubadilisha kisiwa hicho kuwa cha mkusanyiko wa makasino makubwa:

Tunamtaka Rais Rodrigo Duterte atengue kauli yake ya kufunga kisiwa muhimu kabisa nchini humu kwa kuwavutia watalii. Tunaitaka pia serikali kuu ije na mkakati madhubuti na wa kisayansi wa kuendeleza Boracay na ambao hautapelekea kuharibu hali ya uchumi kwa kuwashirikisha ipasavyo wadau wake wote.

Kwa kipindi kirefu Boracay imekuwa ikipokea hati zisizoridhisha kutoka kwa wanamazingira, lakini, suala hili lilikuja kutiliwa mkazo zaidi mapema mwezi Februari 2018. Kisiwa hiki cha watalii ambacho kimekuwa kikifahamika kwa jina la “shimo la maji taka,” Duterte aliweka wazi kuwa angekifunga baada ya miezi sita kama changamoto hizi za uhifadhi wa mazingira zisingalitafutiwa ufumbuzi mapema iwzekanavyo.

Boti na watali huko Boracay. Picha na: Wikimedia Commons.

Tamko la Duterte linakuja kufuatia uchunguzi uliofanyika visiwani humo na wakala wa serikali wa masuala ya utalii na mazingira mapema January. Na ndipo Duterte alipolitaka baraza la Mawaziri kufanya maandalizi ya kukifunga kisiwa hiki hadi kufika Aprili 26, bila hata ya kushauriana na wadau wakaazi na bila ya uwepo wa mpango kazi wowote wa kuendeleza na kuboresha kisiwa wala kuwepo kwa mpango wa muda mrefu wa maisha ya watu na utoaji wa makazi mapya kwa wale walioathirika.

Sekta mbalimbali ziliingiwa na mashaka kuhusu maamuzi ya Duterete mara baada ya taarifa kuvuja kuwa serikali imetoa kibali kwa Kampuni ya Burudani ya Galaxy (GEG) yenye maskani yake huko Macau cha kujenga kasino lenye thamani ya dola milioni 500 za Kimarekani kwenye kisiwa hiki muhimu mno kwa kuvutia watalii.

Ikulu ilitangaza kusitisha mkataba huu, lakini Shirika la Burudani na Michezo la nchini Ufilipino (PAGCOR) lilikuwa tayari limeshatoa kibali kwa GEG na mshirika wake mkaazi, Kampuni ya Sherehe na Burudani (LRWC). Kampuni hii ilikanusha madai yaliyotolewa na serikali kuwa wanatafuta sehemu nyingine ya kujenga kasino.

Duterte alikanusha kufahamu mpango wa kujenga kasino kwenye kisiwa cha Baracoy, pamoja na uwepo wa picha rasmi za serikali zinazoonesha mkutano wa Rais na wawakilishi wa kampuni ya GEG , ulioongozwa na Mwenyekiti wake Lui Che-Woo na Naibu Mwenyekiti Francis Lui Yiu Tiung, wakiwa katika makazi ya Raid mapema tarehe 6 Disemba, 2017.

Duterte akutana na wawakilishi wa kampuni ya masuala ya Burudani inayofahamika kama Galaxy yenye maskani yake huko Macau mapema tarehe 6 Disemba, 2017. Picha kutoka Serikali ya Ufilipino

Wawakilishi wa PAGCOR pia walisema kuwa kasino kubwa la pili linaendelea kujengwa huko Boracay, mara baada ya kupatiwa kibali cha kufanya burudani kufuatia muungano wa pamoja kati ya mfanyabiashara mkubwa Andrew Tan na Kampuni ya Malaysia ya Genting kwenye hoteli ya Savoy, inayopatikana kwenye eneo la mpango wa maendeleo ya fukwe wa Boracay wa kampuni ya inayojihusisha na mali zisizo hamishika inayofahamika kama Megaworld.

Kama namna ya kuwanyamazisha wananchi waliochukizwa kufuatia makanganyiko wa kati ya lengo lililokubaliwa la kufanyia maboresho ya mazingira na ujenzi wa kasino kubwa kisiwani humo, Duterte alitamka kuwa kisiwa cha Boracay kitawekewa mpango mpya wa matumzi ya ardhi . Hata hivyo, watu wengi wamegundua kuwa kauli hii inakosa mashiko, kutokana na ukweli kuwa hakuna tena ardhi ya kutosha kwenye kisiwa hiki cha mapumziko, maeneo mengi yameshajengwa kwa ajili ya makazi pamoja na majengo ya biashara.

Malalamiko ya wakazi wa Boracay kuhusu hatua ya Duterte ya kukifungia kisiwa hiki yanafafanuliwa kwenye filamu fupi iliyoandaliwa na Jason Magbanua iliyopakiwa kwenye ukurasa wa Facebook, na kisha kufafanuliwa kwa undani kupitia maelezo yafuatayo:

Malefu kwa maelfu ya watu wataathirika ikiwa kisiwa hiki kitafungwa moja kwa moja. Watu halisi, wanaopumua, siyo takwimu. Tunawaongelea watoto, akina mama, akina baba, familia yote kwa ujumla – siyo “kushuka kiduchu kwa kiwango cha ukuaji uchumi (GDP).
UKWELI
Kuna namna nzuri zaidi za kutatua changamoto za Boracay. Suluhisho ambalo halitawadharau kabisa wakazi wa kisiwa hicho, jamii ya watu ambao ndio wa muhimu kabisa kuliko kitu kingine chochote.

Mwanablogu wa Blogu ya Ilonggo Samot Tallana, anasema kuwa namna suala la Boracay linavyoshughulikiwa linaanika namna Rais Duterte alivyokosa hoja kwa kujidai hadharani kuwa yeye ni mwanamazingira.

Idadi kubwa ya wafanyakazi wa sekta ya utalii wameanza kuachishwa kazi kisiwani humo kama namna ya wafanyabiashara kukabiliana na madhara ya kufungwa kwa kisiwa hicho. Bili za umeme katika maeneo yote ya Aklan inategemewa pia kuongezeka kwani msambaza umeme jimboni hapo anatarajia kuokoa kiasi cha Pesosi milioni 99 (sawa na dola za kimarekani milioni 1.9), kiasi kitakachopotezwa kwa kufungwa kisiwa hicho.

Watu wengi pia wanahoji taratibu za kikatili za ulinzi zilizowekwa na serikali, kama vile kuwatumia polisi wa machafuko, kuweka vizuizi vinavyozuia watu kufika maeneo mengi ya Boracay, na kuzuia vyombo vya habari kufuatilia mwenendo wa mpango wa uboreshaji wa kisiwa hiki.

Raia walioguswa wameanzisha matandao wa Marafiki wa Boracay kama namna ya kusaidia kuendesha kampeni ya kuzuia kufungwa kwa kisiwa hiki. Picha imetumiwa kwa ruhusa.

Wakati watu wengi wakikubaliana na uhitaji wa kukabiliana na changamoto ya hali mbaya ya mazingira ya Boracay, anguko la kiuchumi linalosababishwa na sintofahamu na uharaka wa kufunga kisiwa cha Boracay kumepelekea makundi mbalimbali ya watu kuungana pamoja na wakazi na wafanyakazi waliothiriwa.

Marafiki wa Boracay ukurasa wa Facebook umeanzishwa kwa lengo la kukusanya matamko yenye lengo la kuunga mkono kampeni ya kisiwa hiki ya kuwasaidia wafanyakazi na vikundi vidogo na vya kati vya wafanyabiashara. Kadiri ya siku za kufunga kisiwa hiki zinavyokaribia, wanawaomba wananchi kuwa na msimamo thabiti kwa ajili ya Boracay na kuwaunga mkono watu ambao watahamishwa ikiwa kisiwa hiki kitafungwa.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.