Je, WanaBlogu wa Tanzania Wataridhia Kulipa au Watagomea ‘Kodi ya Blogu'?

Mwanaume akiwa amesimama katika mtaa wa Mji Mkongwe, Zanzibar, akiperuzi simu yake ya kiganjani. Picha ilipigwa na Pernille Bærendtsen na kutumiwa kwa ruhusa yake.

Kwa zaidi ya muongo mmoja uliopita blogu zimekuwa maarufu nchini Tanzania, zikiwawezesha waandishi na wanahabari wa kujitegemea kutoa maoni yao na kuchapisha habari ambazo, kwa kawaida, zisingeweza kupata nafasi katika vyombo vikuu vya habari. Lakini mpaka kufikia mwezi uliopita, shughuli ya kublogu zitaanza kuambatana na gharama.

Tarehe 16 Machi 2018, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilitangaza Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Maudhui ya habari za mtandaoni) zinazowataka wanablogu wote kujiandikisha na kulipa zaidi ya dola za Kimarekani 900 ili kuweza kuchapisha habari mtandaoni.

Kanuni hizi zitahusu maudhui ya habari za mtandaoni pamoja na : (a) maombi ya leseni ya kutoa huduma; (b) Wanablogu; (c) maduka ya kutolea huduma za intaneti; (d) Wamiliki wa maudhui ya habari za mtandaoni; (e) Majukwaa mtandaoni; (f) Matangazo Redio au runinga za mtandaoni; (g) Vyombo vya habari; (h) Wateja na watumiaji wa maudhui ya habari za mtandaoni na; (i) Maudhui yoyote yanayohusu maudhui ya habari za mtandaoni.

Kanuni hii mpya ina athari kubwa kwa uhuru wa kujieleza pamoja na haki za binadamu. Wanablogu wanalazimika kujaza fomu rasmi za kutoa huduma na kutakiwa kuepuka kuchapisha maudhui yaliyokatazwa ikiwa ni pamoja na picha za uchi, matamshi ya chuki, picha za ngono, vurugu, “madhui yanayosababisha maudhi”, habari za uongo na, “lugha chafu” miongoni mwa makatazo mengine.
Sheria mpya inaipa nguvu Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kuruhusu na kufunga huduma. Chini ya SEHEMU YA II, Namba 4, TCRA ina mamlaka pia ya:

(a) kutunza orodha ya wanablogu, majukwaa mtandaoni, Redio na television mtandaoni;(b) Kuchukua hatua dhidi ya wanaovunja sheria hii, pamoja na kuamuru kuondolewa kwa maudhui yaliyokatazwa

iAfrikan News inaeleza zaidi:

Wachapishaji wa maudhui ya habari za mtandaoni (blogu, matangazo ya sauti, video,) sasa wataomba leseni kwa ada ya shilingi za Kitanzania 100,000, kulipa ada ya awali ya leseni sh. 1,000,000 (sawa ya dola za kimarekani 440) na ada ya mwaka ya leseni kiasi cha sh. 1,000,000 (sawa ya dola za kimarekani 440). Hii ina maana kuwa kuendesha blogu binafsi ya kawaida tu ukiwa unaishi Tanzania inakuhitaji kutumia Dola za Kimarekani 900 kwa ajili ya kulipia ada za leseni.

Mojawapo ya mambo yanayoleta wasiwasi kuhusu kanuni hizi mpya ni utata wa tafsiri zake. Katika makala ya hivi karibuni, mwanablogu Ben Taylor alichambua maudhui ya kanuni hizi, akibainisha kukosekana kwa fasili iliyowazi:

Kitu cha kwanza cha kuzingatia ni kwamba sheria hii haipo wazi kwa baadhi ya vifungu muhimu. Baadhi ya maneno – kama vile ‘mtoaji wa maudhui ya mtandaoni’ na ‘mtoaji wa huduma ya maudhui ya mtandaoni’ -kamwe hayafafanuliwa. Je, hivyo ni vitu vinavyofanana? Katika maeneo mengine, kichwa cha habari kilichopo kwenye vifungu vya sheria hakina uhusiano na maudhui yake. Kwa mfano sehemu ya saba ina kichwa cha habari mwanablogu lakini hakuna maudhui yanayohusu blogu. Pia, sheria ina makosa ya tahajia za maneno na sarufi. Na labda kioja zaidi ni kifungu cha 14 cha matumizi ya leseni za huduma za maudhui ya habari za mtandaoni ambacho hakiwahitaji waombaji kutuma maombi yao wala hakitaji mahali pa kutuma isipokuwa wanatakiwa kujaza fomu ya maombi.

Ndugu Taylor ana hoja muhimu katika uchambuzi wake. Hakuna anayejua jinsi sheria hii itakavyotafsiriwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), mahakama au polisi.

Kilicho wazi ni kwamba kuvunjwa kwa sheria hii mpya kunasababisha adhabu ya faini isiyopungua shilingi za kitanzania milioni tano” (Karibu dola za kimarekani 2,500), “au kifungo kisichopungua miezi kumi na mbili au vyote kwa pamoja”.
Umoja wa Sera ya Teknolojia ya Kimataifa ya Habari katika Afrika Mashariki ulitoa muhtasari wa sera tahadhari juu ya utata wa baadhi ya vifungu vya sheria mpya:

… Kanuni zinapaswa kurudiwa na kurekebishwa ili kuwa wazi, fasili tata na tahajia za maneno na kubatilisha masharti yanayofanana ya blogu kujisajili na watumiaji wenye majukwaa mtandaoni kujisajili pia. Ni muhimu pia TCRA isipewe nguvu kubwa kuondoa maudhui ya habari za mtandaoni, isipokuwa upatikanaji wa maudhui mbalimbali ya habari za mtandaoni uimarishwe. Wajibu uliowekwa usiwafanye watoa huduma na wachapishaji maudhui ya habari za mtandaoni kuwa viranja kwa kuwatwisha majukumu kama ya kurekebisha na kuchuja maudhui, kupitia upya maudhui kabla ya kuchapishwa na kuwa na utaratibu wa kutambua vyanzo vilivyochapisha maudhui.

Kublogu kama fursa mbadala ya habari Tanzania

Nchini Tanzania blogu zilianza miaka ya 2007 na zimejichukulia umaarufu kuwa majukwaa mbadala ya kupashana habari miongoni mwa wasomi, tabaka la watu wa kati, wanasiasa na vyama vya siasa.
Nchini Tanzania, ambapo kihistoria, vyombo vya habari vimekuwa na ukaribu mkubwa na maslahi ya serikali, blogu zilifungua mlango kwa watu binafsi kuanzisha majukwaa binafsi ya kupasha habari ambayo yameonekana kuwa na nguvu sana kwa sababu ya urahisi wake kupatikana na usomaji.
Kabla ya vitumizi vya simu za kiganjani, upatikanaji wa mtandao wa intaneti ya uhakika na kompyuta mpakato yalikuwa ni mahitaji ya lazima sana kwa wanablogu. Hii inazuia kwa kiwango kikubwa watu kushiriki ikiwa wana kipato kidogo.
Blogu ya Michuzi, ilianzishwa mwaka 2005 na Issa Michuzi ambaye anajulikana pia kama ‘mwazilishi wa blogu za kiswahili’, ilikuwa ni moja ya blogu ya kwanza ambayo ilisomwa na maelfu ya wasomaji kwa siku katika Tanzania, mara nyingi ilihabarisha juu ya siasa na habari za kawida. Michuzi alikuwa wa kwanza kuona kublogu kama biashara. Aliweza kufanya maudhui yake yapatikane kwa uhuru na lakini alibaini pia nguvu kubwa ya matangazo yanayomwongezea kipato.

Ingawa kiwango cha umaskini Tanzania ni asilimia 60 mwaka 2007 na inakadiriwa mwaka 2016 ilikuwa asilimia 47, karibia watanzania milioni 12 bado wanaishi katika umaskini uliokithiri.
Wanaopata mtandao wa intaneti bado ni idadi ndogo inayokaribia asilimia 45 kwa takwimu za mwaka 2017. Na idadi ya watu inakaribia milioni 60 na asilimia 31 wanaishi maeneo ya mjini, hata hivyo blogu hazjaweza kuwafikia walio wengi.
Kutokana na makala ya Katibu Mkuu wa Mtandao wa Wanablogu Tanzania ndugu Krantz Mwantepele, kama alivyonukuliwa katika gazeti la Citizen, wanablogu wengi wa kitanzania hawawezi kumudu ada hizo kwa sababu “maombi ya leseni na malipo ya mwaka ni makubwa zaidi ya pato la wanablogu waliowengi”.

Je wanablogu wa ki-Tanzania watagemea au watalipa gharama katika hali hii tete ya kisiasa?

Kublogu kunaendelea kuwa ‘mbinu mpya’ kwa vijana wa ki-Afrika wakisaka majukwaa mapya ili kujadili na kuchambua habari. Uwepo wa simu za kiganjani, umewafanya vijana wa ki-Tanzania kutumia mtandao zaidi mwaka 2017 takribani asilimia 60 ya vijana walitumia mtandao wa Facebook.
Masharti juu ya uhuru wa kujieleza yanaleta changamoto hasa kwa watumiaji wa mitandao ya kijamii nchini Tanzania. Wakati Katiba inaruhusu uhuru wa kujieleza, haitoi uhakikisho kuhusu uhuru wa vyombo vya habari. Kanuni nyingi za vyombo vya habari huzipa mamlaka za Tanzania uwezo wa kuzuia vyombo vya habari kwa hoja ya kulinda usalama wa taifa.
Mamlaka zimeendelea kutegemea sheria hizi tangu uwepo wa hali ya mvutano wa kisiasa zaidi ya miaka mitatu iliyopita. Tangu uchaguzi wa Rais wa mwaka 2015, upinzani Tanzania umekatazwa kufanya maandamano na vyombo vya habari vya kujitegemea vimefungiwa, kumekuwa na vikwazo, vitisho, na wananchi kuadhibiwa pale wanapomkosoa Rais John P. Magufuli wa Chama kilichoshika dola, Chama cha Mapinduzi (CCM).

Sheria ya Makosa ya Mtandao nchini Tanzania, iliyopitishwa mwaka 2015, imetea mitafaruku. Kati ya mwaka wa 2015 na 2016 tu, wa-Tanzania 14 kwa kutumia sheria hiyo, walikamatwa na kushtakiwa kwa kumtukana Rais kupitia mitandao ya jamii.
Desemba 2016, m-Tanzania Maxence Melo ambaye ni mwanzilishi na Mkurugenzi wa Jamii Forums mtandao wa kijamii wenye umaarufu mkubwa Tanzania alikamatwa na polisi. Sababu ya kukamatwa kwake ni kukakataa kutoa taarifa za wanachama wake. Madai hayo yalifanywa kwa kutumia Sheria ya Makosa ya mMtandaoni. Melo aliachiwa baada ya siku tano, lakini kukamatwa kwake kulileta wasiwasi kwa kila mtumiaji wa mtandao huo Tanzania.
Hivi karibuni, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) ambacho ni chama kikuu cha upinzani, kiliomba Umoja wa Mataifa kuingilia kati kutokana na kuongezeka vitendo vya kukamatwa viongozi wakuu wa vyama vya upinzani. Tarehe 16 Februari, 2018, mwanafunzi kijana aliuawa kwa kupigwa na kitu kilichosadikiwa kuwa ni risasi, na watu kadhaa walijeruhiwa wakati polisi ikiwatawanya wafuasi wa vyama vya upinzani waliokuwa wanaandamana jijini Dar es Salaam.
Kanuni hizi hazionekani kulenga kukusanya kodi bali ni zana muafaka na sehemu ya zoezi pana la kuminya uhuru wa kujieleza na ushiriki wa siasa za vyama vingi Tanzania.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.