Mwanamuziki Anayeimba Nyimbo za Kupigania Haki Amechaguliwa Kuwa Mbunge Nchini Uganda

Bobi Wine akiwa kwenye moja wapo ya mikutano yake. Picha ya ukurasa rasmi wa Facebook wa Bobi Wine.

Kufuatilia kampeni kubwa ya uchaguzi iliyochochewa na kukamatwa kwake kwenye mkutano wake wa mwisho, mwanamziki nyota wa Uganda Robert Kyagulanyi Ssentamu, anayefahamika zaidi kama Bobi Wine, sasa amekuwa mwanasiasa rasmi.

Wine si mgeni kwenye shughuli za harakati. Muziki wake umekuwa ukijikita kwenye masuala ya haki za raia. Lakini kuimba masuala ya kisera tu haitoshi. Mnamo Juni 29, hatimaye alifanikiwa kuvuka kihunzi na kuwa mtunga sera baada ya kushinda kiti cha ubunge kwa jimbo la Kyadondo, kwa ushindi wa asilimia 75 ya kura zote za uchaguzi huo mdogo.

Alianza kuimba masuala ya haki za raia mwaka 2005. Wakati wa uchaguzi mkuu wa 2016, aligoma kushiriki kwenye wimbo uliomtukuza na kumpigia kampeni Rais aliye madarakani Museveni — ambaye amekuwa Ikulu kwa miongo mitatu — kuendelea kubaki madarakani. Wanamuziki wengi maarufu walishiriki wimbo ambao Wine alikataa kushiriki.

Moja wapo ya nyimbo zake maarufu zaidi, “Ghetto”, unazungumzia ukatili wa polisi dhidi ya watu wanaoishi kwenye maeneo ya makazi duni jijini Kampala na kutokuwepo kwa huduma zinazokidhi mahitaji yao.

Wine anajiita “Rais wa Ghetto” na “Omubanda Wakabaka,” kumaanisha “Mfalme Nyota wa Kijiweni”. Amekuwa mtu wa tano kutoka kwenye tasnia ya sanaa kuingia kwenye siasa, akifuata nyayo za Ali Ndawula Wowoto, Sulaiman Madada, Judith Babirye na Kato Lubwama, ambao wote hivi sasa ni wabunge.

Kampeni yake ilipambwa na muziki, akiambatana na idadi kubwa ya wanamuziki, watangazaji wa radio na televisheni ambao kwa pamoja walitumia mitandao ya kijamii kusambaza ujumbe wake kwa wapiga kura, wakitumia alama ishara za #BikwaseKyagulanyi, yenye maana ya “mkabidhini kila kitu Kyagulanyi”.

Kwenye mkutano wake wa mwisho, alikamatwa na polisi, waliodai kwamba Wine alikuwa anafanya mkutano kwenye eneo lisilo sahihi karibu na mahali ambapo Rais Museveni alikuwa akimnadi mgombea wake. Video hapa chini ya NTV Uganda, kituo cha televisheni nchini humo, inamwonesha akikamatwa. Aliwasihi polisi, akisema anachokisema yeye ni kupigania haki za watu.

Hata hivyo, alishinda uchaguzi huo mdogo kwa kura nyingi. Alipata kura 25,659, alimshinda Sitenda Sebalu, mgombea wa chama tawala cha NRM, aliyeambulia kura 4,556. Ilani ya Wine iliyohusu masuala ya ukosefu wa ajira na masuala mengine yanayowagusa vijana, ambao anaamini hawapati uwakilishi wanaoustahili, ilipata uungwaji mkono mkubwa.

Bada ya kutangazwa kuwa mshindi, alitwiti kwa wafuasi wake 28,000 kwenye mtandao wa Twitakwamba jambo lisilo la kawaida limetokea kwenye siasa za uchanguzi nchini Uganda.

WATU WAMESEMA. Tarehe ya leo 29 inageuza historia kwenye siasa za nchi yetu! Historia ime..

Wa-Ganda waliingia kwenye mitandao ya kijamii kumpongeza msanii huyo maarufu mwenye miaka 35 kuchaguliwa kuingia bungeni. Orodha ya wanaomwunga mkono ilijumuisha wanasiasa, wanamuziki na watu wa kawaida kwenye majukwaa mbalimbali ya habari.

Masaa machache kabla ya tume ya uchaguzi kutangaza matokeo, Katibu Mkuu wa NRM Justine Lumumba alitwiti ujumbe wake wa kumpongeza:

Pongezi nyingi kwa watu wa Kyadondo Mashariki, hongera kwa Kyagulanyi Robert Sentamu

Na Kizza Besigye, mshindani mkubwa kwenye kampeni ya uchaguzi wa Rais wa 2016, alijitokea kufurahia ushindia wa Bobi Wine; Besigye hakuwahi kumfanyia kampeni kwa sababu chama chake kilikuwa kikimwuunga mkono mgombea mwingine kwenye uchaguzi huo:

Ushindi wa kishindo kwa Mhe Bobi Wine. Hongera sana-NGUVU YA UMMA!! Ndio maana basi watu wa jamii ya Wakiso hawakuruhusiwa kupiga kura kwenye uchaguzi wa mwaka 2016

Msanii mwenzake Jose Chameleone alimpongeza Bobi Wine kwa ushindi wake:

Tunapoamini, Tunapata. Hongera kwa Mhe Robert Kyagulanyi, Familia, Marafiki na Jimbo la Kyadondo Mashariki kwa ushindi huu muhimu.
Viongozi wanachaguliwa na Mungu. Kwa hiyo, Mungu na akulinde unapotekeleza ahadi zako kuiongoza Kyadondo Mshariki kwenda kwenye Nchi ya Ahadi.

Wanamuziki wenzake Radio na Weasel pia walimpongeza Bobi Wine kwa jitihada zake za kuhakikisha anawapa watu masikini sauti kupitia muziki wake na sasa akiwa ameingia pia kwenye siasa:

Umelinunua Ghetto Rasmi. Hongera Bro Bobi Wine

Siku za nyuma, Bobi Wine alikuwa anafahamika kwa kutumia bangi na kugombana na mwanamuziki mwenzake Bebe Cool. Hata hivyo watu wa Kyadondo Mashariki walikuwa tayari kupuuza mambo hayo na kumchagua kuwa Mbunge. Changamoto kwake ili aendelee kufanikiwa ni kuhakikisha anafanya kazi kwa bidii afanane na wabunge wenzake ambao wamekuwa bungeni kwa zaidi ya mwaka mmoja na kufikia matarajio ya watu waliomchagua na nchi kwa ujumla wake.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.