- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Hatua ya Seneta wa Ufilipino Kufanya ‘Habari Potofu’ Ziwe Jinai — Hii Haitamaanisha Kudhibitiwa kwa Habari?

Mada za Habari: Asia Mashariki, Ufilipino, Sheria, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uhuru wa Kujieleza, Utawala, Vyombo na Uandishi wa Habari, GV Utetezi
[1]

Wale wanaosambaza habari potofu kwenye mitandao ya kijamii wanaguswa na muswada unaopendekezwa. Picha ya mtandao wa Flickr na Stanley Cabigas (CC BY 2.0)

Seneta wa Ufilipino Senator Joel Villanueva amewasilisha muswada [2] mwishoni mwa Juni utakaofanya “Usambamzaji wa habari potofu” kuwa kosa la jinai. Makundi ya waandishi wa habari yameonya kwamba muswada huo unaweza kusababisha udhibiti usio halali wa habari.

Muswada wa Villanueva kwa Seneti Na. 1492 au “Sheria Inayoadhibu Usambazaji Wenye Nia Ovu wa Habari Potofu na Makosa Mengine kama Hayo” inafafanua maana ya habari potofu kuwa ni “habari ambazo ama zinakusudia kusababisha hali ya tahayaruki, mgawanyiko, ghasia, na chuki au zile zenye ujumbe wa kipropaganda kwa lengo la kuchafua au kuharibu hadhi ya mtu mwingine.”

Nuswada huo unapendekeza adhabu kwa wale watakaochapisha “habari potofu” na hata wale watakaosambaza habari hizo, na kuweka uwezekano wa kuwaadhibu watumiaji wa mitandao ya kijamii ambao wanaweza wasioelewe kikamilifu matokeo ya kusambaza makala kwa marafiki.

Hukumu ya mahakama chini ya sheria hiyo inayopendekezwa inategemea na shirika linalochapisha au kusambaza hicho kinachoitwa “habari potofu”. Mtu binafsi atakayekutwa na hatia ya kuchapisha au kusambaza habari potofu anaweza kuhukumiwa kifungo cha mpaka miaka mitano jela. Hukumu kwa maafisa wa serikali itakuwa mara mbili ya ile ya watu binafsi. Na chombo cha habari au jukwaa la mtandao wa kijamii utakaohusika na kusambaza habari potofu wanaweza kufungwa hadi miaka 20.

Villanueva alieleza [3] nia ya adhabu hizo:

Madhara ya habari potofu yasichukuliwe kirahisi. Habari potofu zinajenga mitazamo na imani zinazotokana na dhana zinazoweza kusababisha mgawanyiko, kutokuelewana na kuharibu mahusiano ambayo tayari ni mabaya.

Aliongeza kwamba kupitishwa kwa muswada huo “kutawahamasisha wananchi hasa maafisa wa serikali, kuwajibika zaidi katika kutengeneza, kusambaza na/au kueneza habari.”

Profesa wa Uandishi wa Habari Danilo Arao alichambua muswada huo wa kurasa nne na kuandika muhtasari [4] wa kuukata muswada huo:

Tafsiri ya “habari au taarifa potofu” kwenye kifungu cha 2 ni pana kiasi kwamba inahusisha chochote kinachoaminika kusababisha, pamoja na mambo mengine, tahayaruki na chuki (jambo ambalo ni gumu kulitafsiri)…

Mashirika ya habari yanaweza kujikuta kwenye mazingira ya kudhibitiwa chini ya kifungu cha 3 cha sheria inayopendekezwa kwa sababu hata maoni ya haki au taarifa za kiuchunguzi zinaweza kuchukuliwa kama kuharibu sifa ya maafisa wa serikali na kupachikwa jina la “habari potofu”.

Arao anapinga hitaji la sheria maalum inayowataja maafisa wa serikali, akidai kwamba tayari watu hao wanafuata sheria za maadili ya kazi.

Kwenye mahojiano ya televisheni, msemaji kutoka Kituo cha Uhuru na Wajibu wa Vyombo vya Habari alisema sheria hiyo haina ulazima [5] kwa sabbau sheria ya uhuru Ufilipino tayari inashughulikia masuala yanayoibuliwa na seneta.

Mbunge wa Bunge la nchi hiyo alipendekeza kwamba badala ya kufanya habari potofu ziwe jinai, Baraza la Seneti lifanyie kazi Muswada wa Uhuru wa Habari ambao bado haujafanyiwa kazi akidai kwamba ungesaidia kupambana [6] na usambazaji holela wa taarifa zisizo sahihi kupitia vyombo vya habari na mtandao wa intaneti.

AlterMidya, mtandao wa makampuni huru ya habari, ulilaani [7] muswada wa Villanueva na kusema “ni wa hovyo, usiohitajika na ni hatua za hatari kutengeneza mazingira ya kudhibiti uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari.”

Unatofautishaje kati ya taarifa ya uongo iliyotokana na kosa la kibinadamu na ile inayosambazwa kwa nia mbaya kupitia magazeti, matangazo au mtandaoni?

Inaweza kutengeneza urasimu wa kimadaraka unampa mtu mamlaka ya kutangaza chombo cha habari kilichoandika habari zilizo kinyume cha maslahi ya serikali kuwa ni habari potofu, wakati huo huo kuunga mkono kwa sauti au vinginevyo, uandikaji wa habari mbaya zinazoandikwa na vyombo vya habari vya serikali au binafsi almuradi ziwe zinalinda maslahi ya utawala ulioko madarakani.

Mwandishi nguli Luis Teodoro alimkumbusha [8] seneta kwamba kuna namna bora zaidi za kupambana na habari potofu:

Uwajibikaji kwenye zoezi la haki ya kuwasiliana ufanyiwe kazi, sio na Serikali, lakini na jamii ya waandishi wa habari wenyewe ikiwa ni pamoja na wasomi wa vyombo vya habari vya umma wenye uwezo wa kugundua na kuacha kusambaza habari potofu.

Mwandishi wa makala kwenye gazeti la Philippine Star Jarius Bondoc alionya kwamba kama muswada huo utakuwa sheria, unaweza kutumiwa vibaya [9] na mamlaka za serikali zinazotaka kuwanyamazisha wakosoaji wake:

Muswada huu unatengeneza uwezekano mkubwa wa kutumiwa vibaya. Utawala wa kifisadi unaweza kuutumia kuunyamazisha upinzani. Kwa kuwafungulia mashtaka wakosoaji wake kwa madai ya kutengeneza habari potofu, serikali inaweza kunyamazisha habari za kweli isizokubaliana nazo. Wafuatiliaji wa utendaji wa serikali, sio wapenzi wa serikali, watafungwa na kupigwa faini kwa kuthibutu kusema. Waandishi wa habari za kiuchunguzi wataozea jela.

Hii si mara ya kwanza kwa mtunga sheria wa Ufilipino kuonesha nia ya kupelekea muswada unaojaribu kushughulikia madhara ya habari potofu. Mapema mwaka huu, Spika wa Baraza la Wawakilishi alipendekeza kudhibiti [10] mitandao ya kijamii ili kuzuia kusambaa kwa akaunti bandia na taarifa bandia.