Picha ya kambi ya Wakimbizi Rwanda. Picha na©Elisa Finocchiaro Creative Commons – leseni – BY
Kuna watu wapatao milioni 65 duniani kote kwa sasa ambao wameyakimbia makazi yao. Kamishna Mkuu kwa wakimbizi (UNHCR) anasema hii ni idadi kubwa sana tangu vita ya pili ya dunia. Hali ikiwa ya kutisha hivyo, inavunja moyo zaidi kwa kutambua kuwa wengi wa watu hao wamepoteza mawasiliano na familia zao.
Lakini msaada unaweza kuwa njiani.
Kaka wawili wa Kidenish na wajasiriamali wa mtandaoni David na Christopher Mikkelsen wamepata suluhu ya changamoto hii. Jukwaa lao, REFUNITE, kifupi cha Muungano wa Wakimbizi, limesajili zaidi ya wakimbizi nusu milioni pote duniani na kuwaunganisha na familia zao walizopotezana nazo. Video hii hapa chini inaeleza kwa kifupi kanuni za mradi huu:
Mapema mwaka huu, vijana wa Mikkelsen walitambulishwa kama wajasiriamali wa mtandaoni wa mwaka na Jukwaa la Uchumi Duniani (WEF)kwa jitihada zao. Wakati wa tamko hilo, tovuti yao ilichapisha ufafanuzi wa jinsi jukwaa hili
linavyofanya kazi:
Jukwaa la Kuunganisha familia linafikika kirahisi kwa kupitia ujumbe wa simu, USSD, tovuti au simu ya bure. Hata kama ni mkimbizi wa Ki-Afghanistani akiwa Pakistani au mkimbizi yeyote ndani ya Iraki, mtu yeyote mwenye uhitaji anaweza akatafuta, akaunganishwa na kuwasiliana na mpendwa wake aliyepotea – hata kama hawana uwezo wa kulipia kifurushi cha huduma za mtandao katika simu.
Pamoja na furaha ya kumleta mtu wa 500,000 katika jukwaa la REFUNITE na kuanza safari ya kuwaunganisha na familia zao, kaka hawa
bado hawajasahau kuhusu umuhimu wa jukwaa hili:
Wakati haya ni mafanikio ya kukumbuka, yanakuja na kumbukumbu ya huzuni kuwa hawa ni watu ambao hawakufanikiwa kuunganishwa na watoto wao, ndugu, wazazi na marafiki zao. Kwa bahati mbaya hili haliishii hapa: dunia bado inaendelea kuwafanya watu wengi wakimbizi zaidi ya tulivyoona wakati wa vita ya pili ya dunia. Na wakati Syria inahusishwa na watu wake wengi kukimbia na kushika vichwa vya habari vingi, pia kwa bahati mbaya kuna matukio mengine yaliyokomaa na mengine yaliyo katika hati hati ya kuibuka na kulipuka wakati wowote. REFUNITE itaendelea kufanya kazi bila kuchoka kusaidia kila mmoja kumtafuta mpendwa wake waliyepotezana na kuunganishwa tena. Kusudi letu ni kuendelea kulijenga jukwaa letu na kutoa faragha na miundombinu ya kidigitali kwa karibuni wakimbizi mamilioni.
Makao makuu ya REFUNITE yako nchini Kenya, lakini mwanzoni yalikuwa nchini Denmarki kwa ushirikiano na Ericsson. Inadhaminiwa na Mfuko wa IKEA na mashirika mengine binafsi na imekuwa na ushirika na muunganiko wa makampuni ya simu za mikononi na Facebook.
Hivyo karibu jumbe milioni 11 zimetumwa kupitia jukwaa hili na utafutaji upatao milioni 9 na usajili wa watu 600,000 kote ulimwenguni. Mpaka 2017 REFUNITE imelenga kusajili wakimbizi milioni moja.