Rais wa Tanzania Afukuza Watumishi 10,000 Kwa Madai ya Kughushi Vyeti

Raia wa Tanzania John Magufuli alihutubia mkutano wakati wa maadhimisho ya Mei Mosi 2017. Picha kutoka Ikulu ya Tanzania .

Usiku wa kuamkia Mei Mosi, siku ambayo dunia imeitenga maalum kwa ajili ya kuwaenzi wafanyakazi, serikali ya Tanzania imewafukuza maelfu ya wafanyazi nchini humo.

Mnamo Aprili 28, Rais John Magufuli aliamuru kufutwa kazi mara moja kwa takribani watumishi 10,000 baada ya uchunguzi kubaini kwamba baadhi ya watumishi wa serikali wameajiriwa kwa kutumia sifa za kughushi.

“Hawa ni wezi kama wezi wengine,” Magufuli alinukuliwa akisema. “Wangeweza kufungwa kwa miaka saba kwa mujibu wa sheria.”

Katuni ya Gazeti la The Citizen

Hatua hii inakuja baada ya serikali kubaini kwamba ilikuwa inapoteza mabilioni ya shilingi kila mwaka kuwalipa maelfu ya “wafanyakazi hewa.”

Taarifa,iliyoangazia zoezi la uhakiki wa sifa za watumishi wa serikali wapatao 450,000, iligundua kwamba Halmashauri za wilaya ziliongoza kwa idadi ya watumishi wa umma wenye vyeti vya kughushi ambavyo vilikuwa 8,718. Taasisi nyingine za umma kama Chuo Kikuu cha Sokoine kilichokuwa na watu 33 waliokuwa na sifa za kughushi na Shirika la Reli la Taifa likiwa na watu 24.

Habari za ‘Safi sana’

Haikuchukua muda mrefu kwa mtandao wa intaneti kueneza habari hizo.

Baadhi ya wtau walionesha kuwahurumia watumishi waliofukuzwa, wakimwomba Mungu kuwatia nguvu wale wenye vyeti feki.

Wengine walikuwa wakifanyia masihara suala hilo.

Kwa ujumla, habari hizi zilipokelewa kwa kauli za “poa sana”, “safi sana” kwa sababu watu wamefurahishwa kwamba hatua zimechukuliwa dhidi ya suala hilo. Hata Rais wa zamani Benjamin Mkapa aliunga mkono hatua hiyo ya Magufuli hadharani, akisema uamuzi huo ulingojewa kwa muda mrefu.

‘…wanapenda kutoa kazi kwa ndugu zao…’

Kwa kweli, kuna watu wanaochukulia suala hili kijuu juu.

Hery Ayubu alitumia mtandao wa twita akiomba iwepo tume huru ya kupokea malalamiko.

Serikali haiwezi kuhukumu kesi yake yenyewe.

Wakati huo huo, chama kimoja cha upinzani, ACT-Wazalendokilitwiti kwamba ingawa wao wanaunga mkono nia ya serikali kupambana na vyeti feki, walihoji ikiwa zoezi hilo liligusa kila anayehusika.

Chama hicho kilidai kwamba uamuzi huo ulilenga kuwalinda baadhi ya wateule wa Rais.

Felix Milinga alikubaliana na taarifa kwamba baadhi ya Halmashauri zilikuwa na idadi kubwa ya wenye vyeti feki, akidai kwamba undugu ndio unaoamua nani apate kazi.

‘Je, Mfumo unaotoa elimu chini ya viwango utashtakiwa?’

Huenda maoni yaliyopata umaarufu zaidi kwenye suala hili yalitoka kwa Profesa wa Sheria Issa Shivji aliyehoji hatua zitakazochukuliwa dhidi ya wale wenye vyeti halali lakini wenye elimu feki.

Dk Hellen Kijo-Bisimba, mkurugenzi mtendaji wa Kituo cha Haki za Binadamu, aliomba kwamba kwa siku zijazo serikali ihakikishe kwamba watu wenye vyeti feki hawaajiriwi.

“Vita dhidi ya vyeti feki lazima itazame mbele. Kuwe na mfumo wa kuhakikisha kwamba hakuna mtu anaweza kuajiriwa kama anatumia cheti feki,” Kijo-Bisimba aliliambia gazeti la Kiingereza la kila siku, The Citizen.

Kimataifa, baadhi ya watu walipongeza hatua hiyo ya Magufuli na walilifananisha tatizo la vyeti feki kwenye nchi nyingine. Baadhi ya watoa maoni kwenye ukurasa wa Facebook wa BBC Africa walipongeza hatua hiyo ya Rais wa Tanzania. “Rais amefanya kazi nzuri ya mfano,” Chimwemwe Tembo, ambaye wasifu wake unaonesha ametoka Malawi,aliandika:

Kwa kweli ni maendeleo mabaya. Nimesikia kwamba hata baadhi ya shahada ni za kughushi. Rais amefanya kazi nzuri. Hebu wale waliosota masomoni wapate kazi. Hapa Malawi kama hilo lingetokea, basi huwa ni mara chache lakini wengi wetu, tunatumia vyeti halali

Gezahegn Arebo, kutoka Ethiopia, pia alitoa sifa zilizojaa hisia:

Sasi sana Mhe Rais! Hili ni tatizo la Afrika, lakini viongozi hawana utashi wa kuchukua hatua; wao wenyewe ni feki!

Kiasi cha vyeti vinavyodaiwa kughushiwa na mwitikio wa watu unaonesha kwamba suala hili li kubwa nchini Tanzania. Inaonekana kama vile upatikanaji wa elimu na mfumo wa uajiri vikiunganisha na kujuana vimelilea suala hili kwa miaka mingi.

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.