Kutoka Naijeria “Muinjilisti wa Utamaduni” Anaeneza Lugha za Ki-Afrika Kwa Kutumia Zana Tumizi Za Simu na Usimuliaji wa Hadithi Kidigitali

Picha ya Skirini kutoka kwa Oluronbi, zana tumizi ya simu kwa hadithi za kidigitali.

“Mwinjilisti wa Utamaduni” ni jina ambalo Adebayo Adegbembo anapenda kujiita mara kwa mara, na jina hili linaendana sana na majukumu ya kazi yake anayoifanya iliyo na mchanganyiko wa teknilojia, mafundisho na makusudio ya kuendeleza lugha na Utamaduni wa Kiafrika katika mitandao ya intaneti.

Picha: Adebayo Adegbembo (imetumika kwa ruhusa).

Ikiwa na maskani yake huko Lagosi, Naijeria, lugha mama ya Adebayo ni Ki-Yoruba, ambacho kinazungumzwa na watu wapatao milioni 30. Matamanio yake katika mbinu hii ya lugha yalianza miaka minne iliyopita na ilianza pale alipokuwa anatafuta namna yakutumia teknolojia kumtia moyo mpwa wake na watoto wa jirani kujifunza lugha hiyo. Kama mwanzilishi wa Michezo ya Genii, timu yake imeweza kuvumbua zana tumizi za simu za kujifunzia na video zilizohuishwa za lugha ya Ki-Yoruba, pamoja na lugha nyingine za Ki-Naijeria na Afrika. Kulingana na Adebayo, teknolojia imekuwa mojawapo ya zana za kufanya kujifunza lugha kuwe kwa “kuvutia, kuchangamsha na kushirikisha zaidi”:

Teknolojia inatoa muundo bora wa mbinu bunifu za kuhifadhia lugha za asili. Inasaidia mchakato wa kunakili, ushirikiano baina ya wataalamu wa lugha, inatoa wigo mpana wa vifaa vya kusambazia n.k. Ukiwa na teknolojia, ni rahisi kuiweka lugha katika mazingira ya kuwafikia watumiaji wengi zaidi wakigawanyika katika makundi kulingana na umri na kiwango cha uelewa wa lugha.

Ikiwa imeundwa kwa ajili ya watoto zana tumizi hiyo ya simu iitwayo Igbo 101, ina mfumo wa “jitihada zenye hatari”. Watumiaji wanaweza kuongeza au kupanda kutoka ngazi moja hadi nyingine ya mchezo kwa kufaulu ngazi tofauti tofauti za lugha huku wakiwa na lengo la kufikia mwisho na kupata zawadi ya ” Amamiihe” ikiwa na maana ya “Ufahamu” katika lugha ya Igbo. Zana tumizi hiyo ya simu hivi karibuni imezindua toleo lililoboreshwa na inapatikana kwa simu za Android na iOS. Zana tumizi nyingine za kujifunzia lugha zinapatikana kwa lugha za ki-Yoruba na ki-Hausa.

Kutengeneza zana tumizi hizi za simu kwa ajili ya kujifunzia lugha, huhitaji timu ya watengeneza programu, wataalamu wa maumbo mfano, mafundi sanifu wa sauti, wahandisi wa sauti na waongozaji wa lugha kuunda hiki zote na kuziweka pamoja. Wataalamu wa lugha ni muhimu sana katika mchakato wa kumudu kiimbo cha hiki za lugha za Nigeria, ambazo zinaenezwa katika lahaja nyingi tofauti tofauti. Mchakato huu umehifadhiwa vyema katika maandishi na kuchapishwa katika chapisho la “Inagharimu Nini Kuunda Zana Tumizi ya Simu” kwa ajili ya blogu za Michezo ya Genii.

Kuonesha hadithi kutoka Nigeria na maeneo mengine Afrika ni ziada ya kazi za Adebayo. Akisaidia kutia moyo kizazi kijacho cha wasimulizi wa hadithi katika mtandao, amekuwa akifanya warsha na watoto wenye umri wa kuwa shule za msingi Barani pote. Hapo Machi 2016, aliongoza warsha nane kuzunguka shule za Naijeria, zilizolenga kuunda maudhui ya kiutandawazi kwa ajili ya watoto. Alishirikisha wazo la msingi la shughuli hiyo alisema:

Ni warsha ambayo tunawapitisha watoto katika mchakato wa kuunda hadithi rahisi wakitumia zana za kiteknolojia. Kwa pamoja tulikuja na mawazo mbali mbali ya hadithi kisha tukaandika miswada, tukachora, tukapaka rangi, tukarekodi masimulizi na kuziweka kwa pamoja katika zana tumizi za simu au video. Lengo letu ni kuondoa ugumu wa kuelewa mchakato wa kutengeneza maudhui. Zaidi ya hayo, lengo letu kuu ni kuwavutia watoto kuchukua umiliki wa masimulizi yao.

Kutokana na kufaulu kwa warsha hizi, aliongoza shughuli nyingine kama hizo huko Johannesburg, Afrika Kusini kwa ushirikiano na iAfrikan, Sisi ni Nani Afrika, Maabara za Macroscopia chini ya wenyeji wa Jozihub, kama sehemu ya kusherehekea Siku ya Vijana. Watoto ishirini na sita kutoka shule mbili za msingi za Soweto walichukua nafasi katika vipengele vyote vya kutengeneza video yenye urefu wa sekunde tisini kuhusu Umngqusho, chakula kikuu na maarufu kutoka Afrika Kusini. Pamoja na kuja na wazo la hadithi, pia watoto walitengeneza mifano ya wahusika pamoja na sauti zao. Matokeo ya mwisho ya kazi hiyo yanaweza kuonekana katika video ifuatayo huko YouTube:

Wakati zana tumizi za simu na hadithi za kidigitali zimepiga hatua katika kutangaza lugha za Naijeria mitandaoni, bado kuna changamoto katika kuhakikisha kuwa watoto wengi zaidi wanaweza kufikiwa na maudhui haya. Hii inahathiri zaidi watoto wa maeneo ya vijijini Barani Afrika, ambapo kuna muitikio mdogo sana wa kutumia Simu Janja. Adebayo anasema hii ni muhimu kwa sababu Simu Janja ina “vipengele ambapo lugha hizi huwasilishwa katika miundo mbali mbali, hivyo kuhamasisha ubunifu na matumizi zaidi. Ongezeko la upatikanaji wa Simu Janja kwa bei nafuu itarahisisha hili baada ya muda na nafikiri tumeanza kuona hilo likitokea.”

Anza mazungumzo

Mwandishi, tafadhali jiandikishe »

Miongozo

  • Tafadhali wape heshima watumiaji wengine. Maoni yenye lugha ya chuki, matusi na mashambulizi binafsi hayataruhusiwa.