- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Wa-Kenya Wahofia Kuzimwa kwa Intaneti Katika Uchaguzi wa Rais 2017

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Kenya, Censorship, Haki za Binadamu, Siasa, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uchaguzi, Uhuru wa Kujieleza, GV Utetezi
Wa-Kenya wakitumia mtandao wa intaneti jijini Nairobi. Creative Commons image by Flickr user krosinsky. [1]

Wa-Kenya wakitumia mtandao wa intaneti jijini Nairobi. Picha na Creative Commons kwa watumiaji wa Flickr krosinsky.

Wa-Kenya katika mitandao ya kijamii wameanza kuelezea wasiwasi wao juu ya uwezekano wa serikali kufungia mitandao hiyo hasa katika kipindi hiki ambapo kuna kinyang'anyiro cha uchaguzi wa Rais utakaofanyika mwezi wa Agosti 2017.

Mwezi Juni mwaka jana, Mpiga picha za Kiharakati nchini Kenya Boniface Mwangi alisheya na wafuasi wake wa Twitter undani wa makala iliyotoka katika gazeti la Kenyan Daily. Makala ilionesha kuwa serikali inataka kuandaa muswada wa sheria utakaoipa mamlaka ya kudhibiti matumizi ya mitandao ya kijamii nchini Kenya. Hili linafanana na maoni yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Kidigitali Ikulu ndugu Dennis Itumbi.

Wakati Itumbi alipoulizwa kuhusu muswada huo katika kipindi cha Press Pass katika Televisheni ya Taifa, alikataa uwepo wa muswada kama huo. Hata hivyo alikosoa chama cha wamiliki wa Blogu kwa kushindwa kuwadhibiti watu wao (Kumbukumbu kwa Mhariri: mwandishi naye alikuwa katika kipindi hicho pia kama sehemu ya jopo liliendesha mjadala huo na Itumbi. )

Katikati ya mwezi Disemba 2016; mfanyakazi wa idara ya ulinzi alizima intaneti pamoja na vifaa vya mawasiliano ya simu ndani ya jengo la Bunge la Kenya baada ya mgongano baina ya wapinzani na wabunge wanaoiunga mkono serikali juu ya marekebisho ya sheria kufuatia uchaguzi unaokuja.

Ndani ya mwaka 2016 pekee, wa-Kenya wapatao 60 walikamatwa [6] wakiwa ni raia wa kawaida na waandishi wa habari, wengi ikiwa ni kwa sababu ya mabandiko yao katika mitandao ya kijamii ikiainishwa kama “lugha za chuki” au zilizo kinyume na sheria enye lengo la kudharau mamlaka ya serikali au matumizi mabaya ya teknolojia.

Disemba 20, 2016, mwandishi wa habari anayefanya kazi na gazeti moja la kiraia nchini Kenya alitwiti kama ifuatavyo:

Mwandishi huyo alihalalisha kitendo cha serikali kufungia mitandao ya kijamii kwa kusema kuwa ni kwa sababu ya ‘kubandika mambo mengi yasiyo kuwa ya kiuwajibikaji au yasiyo na maana’. Mrejesho wa wa-Kenya wengi katika mtandao wa Twitter ulikuwa wa haraka:

Osman alishtushwa na wito wa kuzimwa kwa mtandao wa intaneti uliofanywa na mwandishi wa habari ambaye kazi yake ipo kwa sababu tu ya Uhuru wa habari na Uhuru vyombo vya habari:

Kenya haitakuwa nchi ya kwanza au ya pekee barani Afrika kujaribu kuzima mtandao wa intaneti hasa katika kipindi cha uchaguzi, nchi kama vile Uganda [11] na Gambia [12] ziliwahi kuzuia mitandao ya kijamii na pia kuzima huduma ya intaneti wakati wa uchaguzi.

Ndani ya makala [13] iliyotoka katika Kazi za Demokrasia, William Gumede aliandika kuwa serikali nyingi Afrika zinaongeza kubana intaneti, na hasa mitandao ya kijamii, pamoja na huduma ya kutuma ujumbe ambapo kwa ujumla wake zikiwa ni jitihada za kunyamazisha Wapinzani wa Kidemokrasia, Mashirika ya Kijamii na Wanaharakati wanaojiunga kupinga uongozi mbovu.

Katika makala yake, William aliandika kuhusu matukio ya kuzimwa kwa intaneti katika nchi za Ethiopia, Zimbabwe, Misri, Uganda, Msumbiji na Sudani. Pia yamekuwepo majaribio kadhaa nchini Naijeria na Sudani Kusini ya kukomesha kabisa Uhuru wa kujieleza mitandaoni kwa kutambulisha sheria mpya ya mitandao kwa muundo wa sheria za makosa ya mitandao na udhibiti wa mahudhui ambapo zilipingwa na mashirika ya kijamii katika nchi hizo mbili.

Wa-Kenya ni miongoni mwa watumiaji wazuri wa mitandao ya kijamii Afrika na hasa Kusini mwa jagwa la Sahara ikifuatiwa na Afrika Kusini. Mjumuiko wa wa-Kenya mtandaoni unafahamika kama Kenya Kwenye Twita (KOT- Kenya On Twitter) na hii ni kutokana na kutumia hashtagi hiyo kuwasilisha mawazo na mitazamo yao katika mada zinazogusa masuala ya kijamii, siasa na utamaduni.

Swali la iwapo serikali ya Kenya ifuatilie kwa ukamilifu au/ na kudhibiti nafasi ya mitandao ya kijamii limekuwa moja ya maswali tata sana. Na hii inazidi hasa kutokana na kuenea kwa habari za uongo nyingi, na imekuwa changamoto iliyohamasisha uwepo wa vichwa vingi vya habari tangu uchaguzi wa Marekani ufanyike.

Ni hivi karibuni, habari ya uongo [14]ikimuhusisha Raila Odinga – mtu anayeutamani Urais kwa muda mrefu na mgombea tishio katika uchaguzi ujao nchini Kenya – na mgogoro wa Sudani Kusini na ikawa mada iliyovuma sana katika mitandao ya kijamii nchini Kenya, na ni mpaka pale jina la mmiliki wa tovuti husika lilipogundulika na kuwekwa wazi ndipo iligundulika kuwa hata makala hiyo ilikuwa ya uongo.

Wa-Kenya mtandaoni wamegawanyika katika kipengele cha kimaadili na kisheria na kuhusu madhara ya mtandao wa intaneti kudhibitiwa na serikali.

Lakini wa-Kenya hawajaungana moja kwa moja katika masuala haya. Kuna wale wako kama AnnShelly Peters ambaye hatajali kufungwa kwa mtandao kukabiliana na chuki:

James Thagana anadhani kuwa wa-Kenya wamevuka mipaka ya Uhuru wa kujieleza na serikali ikifungia mtandao itakuwa muafaka wa muda mrefu:

Wakati wa uchaguzi wa 2007, serikali ya Kenya iliagiza kuzimwa kwa mitambo yote katika nyumba zote za habari wakati wa ujumuishaji wa kura katika uchaguzi uliozaa vurugu kubwa za kisiasa zilizogharimu maisha ya maelfu ya WaKenya. Lakini mitandao ya Kijamii na mawasiliano yanayotegemea intaneti yamepitia njia ndefu kufika hapo. Imebakia kuona ni madhara gani yatakayojitokeza leo kwa kufungiwa kwake.