- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Shindano Dansi la Rais wa Kenya Lakwama Baada ya Wakosoaji Kuliita Dansi ya Aibu

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Kenya, Muziki, Uandishi wa Habari za Kiraia, Uchaguzi, Vijana

Rais Uhuru Kenyatta (katikati) akicheza kwenye eneo la Ikulu ya nchi hiyo. Picha imeenea kwenye mitandao ya kijamii.

Shindano lililoanzishwa na Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, #UhuruDabChallenge, kuwahamasisha vijana kujiandikisha kupiga kura limekwama baada ya watumiaji wa mitandao ya kijamii kulitafsiri kama ishara ya kukosa kipaumbele kwenye utawala wake.

Shindano hilo linawahitaji vijana ‘kucheza dab’ —miondoko ya dansi inayofanana na kupiga chafya kwenye kiganja chako —kwenye vituo vya kuandikisha wapiga kura na kuweka picha zao wenyewe kwenye mitandao ya kijamii. Wa-Kenya watapiga kura Agosti 8, 2017.

Twiti [1] iliyokuwa kwenye akaunti rasmi [2] ya Uhuru Kenyatta kuhusu kampeni hiyo ilisema:

The winner of the Dab challenge, whether it is a group or individual with the most retweets at the end of the remaining five days of voter registration, will be rewarded for their patriotism, including visiting with me at State House.

Mshindi wa shindano la Dab, iwe ni kikundi au mtu mmoja moja atakayekuwa na twiti itakayosambazwa mara nyingi zaidi mwishoni mwa siku tano zitakazobaki za zoezi la kuandikisha wapiga kura, atatuzwa kwa uzalendo wake, ikiwa ni pamoja na kunitembelea hapa Ikulu [ya Nairobi].

Na kama sehemu ya kampeni hiyo, Kenyatta alirekodi video ya miondoko ya dab [3] akiwa Ikulu na wacheza dansi maarufu nchini humo wanaoitwa FBI.

Hata hivyo, watumiaji wa mtandao wa Twita waliohamasishwa na alama habari hiyo walianza kutuma maoni ya kukosoa kwa kutumia alama habari ya #DabOfShame. Wa-Kenya walishangazwa inakuwaje rais aliweza kupata muda wa kurekodi video ya muziki wakati nchi ikikabiliwa na matatizo makubwa ya kijamii na kisiasa kama vile njaa, ukame, kufa kwa mifugo na migomo ya kitaifa inayofanywa na wahadhiri wa vyuo vikuu [4] na madaktari [5].

Kufuatia zoezi hilo la kupinga kampeni hiyo, twiti na picha zote zinazofanana na alama ishara ya kampeni hiyo (ikiwa ni pamoja na ile iliyotajwa hapo juu) zilifutwa kwenye akaunti ya twita ya Rais Kenyata [6].

Pamoja na kufuta twiti hizo, baadhi ya watumiaji wa mtandao wa Twita kama vile Dikembe walichapisha picha za twiti hizo na kuzisambaza mtandaoni kwa kejeli.

Rais Uhuru FUTA twiti hizi! Jamani, hatuwezi kuwa na sheria ya kuzuia kitendo chochote cha kufuta kitu kwenye kumbukumbu za rais?

Akionesha kupinga shindano hilo, Master Chengo alichapisha picha mbili zinazoonesha tofauti kati ya mwondoko wa dab wa rais na mwondoko wa dab wa wananchi wa kawaida:

Mwaka huu 2017 uwe wa Ukombozi.
Linganisha mwondoko wa Dab wa Rais na Mwondoko wa Dab wa Mwananchi wa kawaida

Video ifuatayo iliyochukuliwa kwenye kituo cha televisheni cha Kenya NTV inamwonesha rais Kenyatta akicheza na kikundi cha dansi cha FBI:

Elia Muriuki alibainisha:

Shindano la Dab la Uhuru limekumbwa na dhoruba baada ya kukataliwa na wa-Kenya wenye hasira. Limegeuzwa kuwa Dab ya Aibu. Tia bidii mhe Rais

Mark Wuon Odhis alilalamika:

Wa-Kenya wanakabiliana na ukame mbaya, ambao rais ameutangaza [19] kuwa janga ;a taifa.

Silas Okumu alitania:

Dab ya aibu baada ya kucheza dansi la dab, kinachofuata ni mwondoko wa twiki…tutafanya hivyo sasa ambapo ukame ni janga la taifa

Twiki [21] ni aina ya dansi ambayo mtu hucheza muziki kwa namna ya kimapenzi.

Wakati Kibii Eliud alimwuuliza rais:

Mhe Rais, unaonaje tutumie miondoko ya dab kumaliza mapigano kwenye eneo la Kerio Valley na Laikipia?

Kumekuwa na mfululizo [25] wa mapigano [26] kwenye eneo la Kerio Valley [27] yanayohusishwa na ujambazi wa kutumia silaha na wizi wa ng'ombe na hivyo kusababisha vifo vya watu kadhaa.

Akaunti ya Twita inayotumiwa na mtu anayejiita mtoto wa Kenyatta ilitania:

Msikuze sana yale yaliyofanywa na Baba Yangu, kama Rais lazima atumie vizuri Posho ya Burudani

Hata hivyo, kuna wa-Kenya kama vile Yobra Silver aliyekuwa anaunga mkono kampeni hiyo. Aliandika:

Rais mzuri. Inapendeza kujua kuwa na yeye anawakubali vijana

Mtumiaji mwingine wa Twita aliandika:

Wera! MHE Uhuru mimi na familia yangu tunacheza dansi la Dab

Na Annie alikuwa na maoni yafuatayo:

Ni Kenya pekee ambapo rais hatakiwi kucheza dab, kucheka au kufurahia maisha