- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

China Kufungia Kutolewa kwa Huduma ya Mitandao Binafsi ya Intaneti

Mada za Habari: Asia Mashariki, China, Censorship, Sheria, Teknolojia, Uandishi wa Habari za Kiraia, GV Utetezi
The Great Firewall of China. Image from Digital Trends.

Bendera ya China. Picha ya Digital Trends.

Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Habari ya China inasema itapiga marufuku “huduma haramu” zinazotolewa na mashirika mbalimbali, ikiwemo huduma za kutoa mtandao binafsi wa intaneti (VPN), mpaka Machi 2018.

Tangazo la Januari 17 lililowekwa kwenye tovuti ya Wizara hiyo linasema: [1]

各基础电信企业应加强线路资源管理,严格审核租用方资质和用途,不得向无相应电信业务经营许可的企业和个人提供用于经营 IDC、ISP、CDN 等业务的网络基础设施和 IP 地址、带宽等网络接入资源。

Makampuni yanayotoa huduma ya Intaneti [yatalazimika] kupitia na kudhibiti matumizi ya mtandao yanayofanywa na wateja wao na lazima yasitishe huduma kwa makampuni au mashirika yasiyokuwa na leseni ya kutoa huduma ya Data za Intaneti (IDC), utoaji wa huduma ya Mtandao (ISP) na mtandao wa kusambaza maudhui (CDN) na kuendesha shughuli zinazotoa zana zinazowezesha huduma za intaneti, namba ya utambulisho (IP) na huduma ya kuunganisha wateja.

未经电信主管部门批准,不得自行建立或租用专线(含虚拟专用网络 VPN)等其他信道开展跨境经营活动。

Bila idhini [ya Wizara], hakuna atakayeruhusiwa kuunganisha au kukodisha viungo maalumu vya mtandao (ikiwemo VPN) kwa minajili ya kuendesha shughuli zinazovuka mipaka ya nchi.

Sheria hii mpya inamaanisha kwamba watoaji wa huduma za VPN wanalazimika kusajiliwa na kuwajibika kwa mamlaka za serikali. Kama watashindwa kufanya hivyo, watachukuliwa kama wahalifu na kustahili adhabu.

Mtaalam wa Teknolojia ya habari na mawasiliano (IT) anayefanya shughuli zake jijini Shanghai Li Yi alieleza kwamba hatua hiyo inalenga “kusafisha” zaidi mtandao wa ndani ya nchi hiyo.Aliliambia [1] shirika la habari lenye uhusiano na serikali Global Times:

Baadhi ya makampuni makubwa nchini China kama vile Microsoft yana mahitaji ambayo kimsingi yanaeleweka ya kuwasiliana na yalipo makao makuu ya makampuni hayo nje ya nchi kwa kutumia VPN, lakini wakati mwingine makampuni hayo au watu binafsi [waajiriwa] hufungua kurasa za mtandaoni za nje ya nchi kwa nia mbaya. Kwa sababu hiyo, sheria mpya ina umuhimu mkubwa.

“Nia mbaya” ni pamoja na kufanikiwa kupata tovuti za nje ya nchi zilizozuiliwa nchini China na kuwa na majina ya tovuti yaliyosajiliwa nje ya China.

Kwa mujibu wa Kanuni mpya za Matumizi ya Majina ya Anuani za Tovuti, tovuti zote zinazotengenezwa nchini China lazima zisajili [2] majina ya anuani zao kwa watoa huduma wa ndani waliosajiliwa ili waweze kuunganishwa na mtandao wa ndani nchini China.

Serikali ya China imefungia hudua kadhaa za VPN nchini China tangu 2015, lakini sera ya sasa inafanya VPN na huduma za utunzaji wa data za intaneti zisizosajiliwa kuwa kosa la jinai.

Kwa mujibu wa Kipimo cha Mtandao Duniani (2016 Q4):

zaidi ya watu wazima milioni 90 nchini China wametumia majukwaa ya mtandaoni yaliyofungiwa.

Majukwaa makuu ya mitandao ya kijamii ikiwa ni pamoja na Twita na Facebook yamefungiwa nchini China. Lakini vyanzo kutoka kwenye mtandao wa Twita vimesema [3] kwamba jukwaa hilo lina watumiaji hai wapatao milioni 10 nchini China, wengi wao wakitegemea mtandao wa VPN kuweza kupata tovuti ya Twita. Takwimu hizo zinamaanisha kuwa idadi ya wakosoaji wa serikali nchini China inaongezeka ingawa serikali inakusudia kutengeneza mtandao wa ndani wa intaneti unaodhibitiwa na serikali.

Wiki iliyopita kwenye Mkutano wa Uchumi Duniani [World Economic Forum], Rais wa China Xi Jinping aliapa kuwa China itaupigania utandawazi. Kama mtumiaji wa mtandao wa Twita @chowhf alivyobainisha kuwa upatikanaji huru wa taarifa hauna uhusiano wowote na utandawazi nchini China:

Jambo zito. Utandawazi hauhitaji VPN, zana inayokusaidia kukwepa udhibiti wa serikali ya China

Katika jamii ya wanateknolojia wa China, wengi walionesha wasiwasi kwamba China inafunga mlango wake kuizuia kuwasiliana na dunia:

Kanuni kama hii ina msingi wowote wa kikatiba?

Kwa kitendo cha kuitenga China na dunia. China inaelekea kuwa Korea Kaskazini.

Suala hili halihusiani na uendeshaji. Wana wasiwasi kwamba wa-China wanaiona China halisi.

Ni kweli, kanuni hiyo inafanya kazi dhidi ya “VPN zisizo halali” –teknolojia haitaweza kufutwa yote. Kwa mfano, jeshi la wananchi [6] la China litaendelea kuwa na uwezo wa kutumia VPN kueneza propaganda za kisiasa nje ya Kuta Kuu za China.

Kama mtumiaji wa Twita wentommy alivyodokeza:

MIIT imeamua kudhibiti huduma zote za VPN, ni kwa kiasi gani hiyo itaathiri makundi ya mtandaoni? Mwaka jana mnamo Januani 20 [baada ya Tsai Ing-wen kushinda uchaguzi wa Rais wa Taiwan [9]], mamilioni ya vijana walipanda kwenye ukuta kuonesha uzalendo. Kwamba wanaungwa mkono na taasisi za vyama, wanaweza kufanya lolote kwa ujasiri. Nani yuko nyuma yetu? Kiongozi wetu ni…Mwenyekiti Mao!