- Global Voices in Swahili - https://sw.globalvoices.org -

Nchini Tanzania, Kusema Msimamo Wako wa Kisiasa Mitandaoni Inazidi Kuwa Hatari

Mada za Habari: Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, Tanzania, Censorship, Siasa, Teknolojia, Uandishi wa Habari za Kiraia, GV Utetezi
A sign for an Internet cafe in Tanzania. Tanzania is one of the top 10 countries with most Internet users in Africa. Creative Commons photo by Flickr user Aslak Raanes. [1]

Maandishi ya Mgahawa wa kutoa huduma za Intaneti nchini Tanzania. Tanzania ni moja ya nchi kumi zenye watumiaji wengi wa mtandao wa Intaneti barani Afrika. Picha ya Creative Commons iliyopigwa na mtumiaji wa Flickr Aslak Raanes.

Raia watano wa ki-Tanzania, Dennis Temu, Suleiman Nassoro, Shakira Makame, Juma Mtatuu, Dennis Mtegwa, walisimamishwa kizimbani nchini humo mnamo Septemba 14 wakishitakiwa kwa kosa la kumtukana [2] Rais John Magufuli kupitia kwenye mitandao ya kijamii. Wote watano walikana mashitaka.

Inadaiwa kwamba watano hao walitumiana ujumbe wa matusi ukimlenga rais na jeshi la polisi kati ya tarehe 24 na 30 mwaka huu, kinyume na Kifungu cha 118 (a) cha Sheria ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta Namba 3 [3] ya 2010.

kifungu hicho kinamtia hatiani mtu yeyote ambaye:

kwa kujua atatengeneza, kuunda au kukubaliana au kuanzisha usambazaji wa maoni, maombi, mapendekezo au aina nyingi za mawasiliano ambayo hayana ukweli, yasiyo ya kimaadili, ya uongo, yenye kutishia au kudhalilisha kwa namna yenye lengo la kuudhi, kutukana, kutishia au kumbughudhi mtu mwingine…
Kati ya hao watano wanaoshitakiwa, waendesha mashitaka wa serikali wanadai kwamba Bw. Mtengwa alichapisha maoni yenye udhalilishaji na matusi kwenye kundi la WhatsApp liitwalo DSM 114U Movement kwa lugha ya Kiswahili. Maoni hayo yanasomeka kama ifuatavyo:

Sijui kitu gani kinaendelea kwenye kichwa cha JPM [Rais Tanzania John Pombe Magufuli]… Hajui hata kusema samahani. Tumefikishwa hapa kwa sababu ya mtu mmoja anayeamini siku zote yuko sahihi…anahitaji kuelewa kuwa siasa haihitaji hasira na Upinzani sio adui…ajifunze kushindana na upinzani kwa mjadala, sio nguvu .

Kwenye tukio jingine la hivi karibuni, Dk. Oscar Magava, mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Mkwawa mkoani Iringa Iringa, alikamatwa [4] kwa kudaiwa kumtukana rais.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa Dk. Julius Jengi Gava alisema mnamo Septemba 15 walipokea taarifa kuwa mhadhiri huyo alitumia mitandao ya kijamii kumtukana rais. Habainisha ni mtandao upi hasa wa kijamii ulitumika na kile hasa ambacho Magava alikisema dhidi ya rais.

Tangu Rais John Magufuli ashinde uchaguzi wa rais uliofanyika Oktoba 2015, watu 14 wameshakamatwa na kupandishwa kizimbani kwa kumtukana rais kupitia mitandao ya kijamii. Mpaka sasa raia mmoja tu, Isaac Abakuki Emily, ndiye aliyepatikana na hatia [5] kwa mashitaka yake. Alitiwa hatiani na Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha mwezi Juni 2016 kwa kumtukana Rais wa Tanzania John Magufuli kwa kutumia ukurasa wake wa Facebook.

Mwananchi wa Tanzania Leonard Mulokozi alishitakiwa [6] mnamo Juni 22 kwa kutumia Sheria ya Tanzania ya Mawasiliano ya Kieletroniki na Posta kwa ujumbe wake wa mtandao wa Whatsapp ambao serikali inasema ni ‘matusi’ kwa Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Mwezi Oktoba 2015, wa-Tanzania wawili walijikuta wakiwa wahanga wa kwanza [7] wa sheria hiyo mpya. Benedict Angelo Ngonyani, mwanafunzi mwenye miaka 24 wa Taasisi ya Teknolojia ya Dar es Salaam (DIT), alishitakiwa kwa kuchapisha maudhui yaliyokuwa “ya uongo na yasiyothibitika na mamlaka zinazohusika.” Inadaiwa alichapisha maandishi kwenye mtandao wa Facebook akidai kwamba Mkuu wa Majeshi wa Tanzania, Jenerali Davis Mwamunyange, alikuwa amelazwa hospitali baada ya kuwa amekula chakula chenye sumu.

Mwezi Novemba 2015, wa-Tanzania wanne — Leila Sinare, Godfrey Soka, Deo Soka na Monica Gaspary Soka — walishtakiwa [8] chini ya Kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mitandao kwa kuchapisha taarifa za uongo, zilizohusiana na uchaguzi kupitia mtandao wa Whatsapp. Waendesha mashitaka wa serikali walidai kwamba mshitakiwa huyo alichapisha taarifa iliyokuwa kwenye mfumo wa sauti kwenye mtandao wa Whatsapp wenye jina la “Soka Group”, ulikusudiwa kuupotosha uma wakati wa uchaguzi wa mkuu wa Tanzania uliofanyika Oktoba 2015, uliokuwa na ujumbe wenye madai ya wizi wa kura.

Wananchi wengi wameshitakiwa chini ya Sheria mpya ya Makosa ya Mtandao [9] inayoibua malalamiko. Mamlaka za serikali zinadai Sheria ya Makosa ya Mtandao ni zana muhimu ya kupambana na picha za ngono zinazohusisha watoto, udhalilishaji wa mtandaoni, kutumia wasifu wa watu wengine isivyo halali mitandaoni, habari zenye maudhui ya ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wageni, kusambazwa kwa ujumbe bila idhini ya wapokeaji, kuingilia mawasiliano ya watu wengine kinyume na sheria, na kuchapisha habari za uongo.

Sheria hiyo tata ilisainiwa kuwa sheria na rais wa zamani Jakaya Kikwete mwezi Mei 2015, pamoja na ukosoaji mkubwa kutoka kwa wanasiasa wa upinzani, wataalam wa mitandao ya kijamii, na wanaharakati wa haki za binadamu.